loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Madaktari: Corona imepungua nchini

CHAMA cha Madaktari Tanzania (MAT) kimesema idadi ya wagonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (Covid-19), imepungua kwa kiasi kikubwa katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma.

MAT imesema kwa kushirikiana na wataalamu mbalimbali katika vituo vya watoa huduma, wamefanya tathmini na kugundua kuwa idadi ya wagonjwa imepungua kwa kiasi kikubwa ndani ya jamii.

Rais wa MAT, Dk Elisha Osati alisema jana kuwa tathmini yao waliangalia idadi ya simu zinazopigwa kwa kuuliza au kuomba msaada wa kitaalamu juu ya wagonjwa wenye dalili kama za Covid-19.

Pia kupungua kwa idadi ya vifo vinavyodhaniwa kusababishwa na ugonjwa huo.

“MAT tunapenda kumpongeza Rais Magufuli kwa kutuongoza Watanzania kupita vizuri katika kipindi hiki kigumu kwa Taifa, ametuongoza kutoa mwelekeo mzuri sana kwa Taifa,” alisema Dk Osati.

Alisema MAT pia inampongeza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na kamati zake zote kwa namna wanavyoongoza nchi kupambana na Covid-19.

“Tunawapongeza sana madaktari na watumishii wote wa sekta ya afya kwa kuwa askari wa mbele kupambana na Covid-19,” alisema Dk Osati na kutoa wito kwa wagonjwa walioko majumbani kwa matatizo ya Covid-19 au magonjwa mengine waende hospitali ili wahudumiwe, kwani ugonjwa wa Covid-19 umepungua kwa kiasi kikubwa na kwamba madaktari wapo tayari kuendelea kuwahudumia.

“Jambo kubwa ambalo tunapenda kusisitiza ni kwamba ugonjwa bado upo na tuendelee kuchukua tahadhari kubwa hasa wakati huu ambao wanafunzi wanarudi vyuoni,” alisema Osati.

Alisema upatikanaji wa vifaa kinga na vifaa tiba uendelee kufanyiwa kazi kwani vifaa hivyo ni muhimu kwa ajili ya kutolea huduma hata kama sio za Covid-19.

“MAT tunawasihi wadau mbalimbali tuendelee kushirikiana na Rais alivyosema misaada mbali mbali ya kupambana na Covid- 19 ielekezwe kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,” alisema.

Ni kutokana na kupungua kwa ugonjwa huo hapa nchini baada ya Mwenyezi Mungu kuliponya taifa hili dhidi ya ugonjwa wa Covid-19, Rais Dk John Magufuli akiwa Chato hivi karibuni aliwaomba tena Watanzania kupitia viongozi wa dini kufanya ibada ya siku tatu ya shukrani kuanzia Ijumaa, Jumamosi na Jumapili iliyopita kutokana na matendo makuu ambayo Mungu amelifanyia taifa hili kwa kuliponya na corona.

Rais Magufuli alitoa ombi hilo alipokuwa akishiriki Ibada ya Jumapili katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) wilayani Chato mkoani Geita hivi karibuni ambapo alisema kwa dhati kwamba ugonjwa huu umepungua kwa kiasi kikubwa.

Awali, Aprili 16, mwaka huu Rais Magufuli aliwataka Watanzania kutumia siku tatu kuanzia Aprili 17 hadi 19, kwa kufunga na kumwomba Mungu ili aliponye Taifa na watu wake dhidi ya maambukizi hayo.

Baada ya ombi hilo la Rais Magufuli, viongozi wa dini wa madhehebu yote waliwaongoza waumini wao katika nyumba za ibada kufanya maombi hayo kwa kufunga na kusali hali iliyosaidia kupunguza maambukizi kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na makisio yaliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa kuanzia katikati ya Aprili Tanzania ingekuwa na wagonjwa wengi wa Covid-19.

Pia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika sherehe za Eid el Fitr, alisema wagonjwa wengi waliokuwa katika hospitali za hapa nchini wakisumbuliwa na ugonjwa wa Covid-19 tayari wameruhusiwa kurudi makwao wakiwa wamepona na kwamba walikuwa wamebaki wachache.

Hata hivyo, viongozi hawa walisisitiza Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari kubwa ya kujikinga na ugonjwa huo kwani haujaisha ikiwemo kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka na pia kuepuka mikusanyiko isiyokuwa ya lazima huku ikilazimika, kukaa umbali wa mita moja kwa kila mmoja.

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ...

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi