loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kikwete: Wanafunzi UDSM rudini chuoni bila hofu

MKUU wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Rais mstaafu Jakaya Kikwete amewataka wasomi wa chuo hicho, waliokuwa wamerudi nyumbani, kurejea chuoni bila hofu kuanza masomo yao, kwani mazingira ni salama.

Kikwete alitoa ombi hilo jana katika Hosteli za Magufuli za chuo hicho, ikiwa ni siku chache kabla ya wanafunzi hao kuanza masomo Jumatatu ijayo. Wasafiri kutoka nje ya nchi na wale waliokuwa wanashukiwa kuwa na maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu (Covid-19), waliwekwa karantini katika Hosteli hizo za Magufuli.

Alisema ameridhika na maelezo yaliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ya kusafisha na kutakasa eneo hilo, kama walivyokubaliana kabla ya kukabidhiwa eneo hilo jana.

“Tunachukua kauli yenu kwamba pako salama na tunawahakikishia vijana kwamba pako salama lakini likitokea la kutokea tutawasiliana, tujue je wanafunzi wamekuja nao ama waliupatia hapa,” alisema Kikwete katika hosteli hizo zilizoko katika Barabara ya Sam Nujoma.

Kikwete alisema alipata wasiwasi kidogo, pale serikali ilipoamua kila anayetoka nje ya nchi akae hapo kwa siku 14, ikiwa ni pamoja na wale waliokuwa wamekutana na watu waliokuwa na maambukizi.

“Shaka yangu kubwa ilikuwa itakuaje kama hawa watu watakuwa wana maradhi, je wakiondoka hawataacha mbegu? Na vijana wetu wakija wakaja kupatia maradhi hapa? Lakini walinihakikishia kuwa serikali imechukua jukumu la kuhakikisha kuwa watafanyia usafi wa kutosha ili wakija vijana wasiwe na mashaka yoyote,” alisema.

Alisema baada ya kuelezwa hayo, alipata matumaini na kuwaambia wafanye hivyo kabla ya kukabidhi majengo hayo kwa chuo. Aliwataka waliochukua hosteli hiyo, kutangaza rasmi kwamba wameshafanya yale yote yanayotakiwa ili kuwawezesha wanafunzi kurudi bila wasiwasi.

“Maelezo hayo watoe wenyewe waliochukua hizo hosteli na waeleze walichokifanya kuwahakikishia wanafunzi na community yetu, kutuhakikishia sisi wenyewe tunaoongoza hiki chuo na jumuiya ya chuo kikuu kwamba hapa mahali pako salama,” alisema Kikwete.

Aliongeza, “Tumekusanyika hapa kwa ajili ya kupata uthibitisho kwamba hapa pametayarishwa kwa ajili ya kupokea wanafunzi baada ya kupokea watu waliokuwa wamewekwa karantini.”

Katika hatua nyingine, aliipongeza serikali kwa kufungua vyuo na kidato cha sita, kwani hali hiyo ilikuwa ikiwapa wasiwasi kutokana na ukweli kuwa kuna wanafunzi walipaswa kumaliza Mei ili wawapishe watakaoanza Oktoba. Akimwakilisha Mganga Mkuu wa Mkoa, Ofisa Lishe wa Mkoa, Neema Kweba alishukuru UDSM kwa kupatiwa nafasi katika hosteli hiyo kutekeleza majukumu yaliyokuwa yamewakabili katika kupambana na Covid- 19.

Alisema walianza kutumia majengo hayo Aprili 5 hadi Aprili 25, mwaka huu kwa ajili ya wale waliokutana na watu wenye maambukizi pamoja na wasafiri walioingia nchini kwa ajili ya kufuatilia afya zao.

“Jumla ya waliokutana na walioathirika walikuwa 426 waliishi hapo na wasafiri walikuwa 418, lakini ilipofika Aprili 25, watu hao walianza taratibu za kuondoka,” alisema Kweba. Alisema taratibu za usafi zilianza Aprili 25 mpaka 30, mwaka huu kwa kusafisha majengo yote.

“Katika ukaaji wetu hapa kuna takataka zilitengenezwa… takataka zote zilizotengene- zwa katika kipindi chote ambacho watu waliishi katika Hosteli ya Magufuli ziliondolewa. Hata hivyo, tulipomaliza shughuli kwa kuwa ugonjwa haujaisha, tumeona tuache vifaa vya kuendelea kujikinga na ugonjwa huo,” alifafanua na kuvitaja kuwa ni matangi ya kunawia mikono pamoja na kichomea taka.

“Mheshimiwa, niseme kuwa Magufuli Hosteli ni salama, kwa ajili ya watu kuja kukaa kwa sababu mara baada ya kufanya usafi katika haya majengo, tumeshakaa mwezi moja na majengo yakiwa wazi yakiwa yamefanyiwa utakasaji kila chumba, kila kitanda, kila godoro na kila sehemu iliyokuwepo katika jengo hili,” alisema.

MWITO umetolewa kwa wakulima kwenye mikoa yanayozalisha chakula kwa wingi ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi