loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Marais wastaafu wammwagia sifa JPM kasi ya maendeleo

MARAIS wastaafu wamefunguka juu ya maendeleo anayofanya Rais Dk John Magufuli, wakisema wanafurahia kuona namna anavyoendesha taifa kwa aina mpya na nzuri, wakimtaka aendelee kusonga mbele.

Wastaafu hao waliweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, walipewa nafasi ya kuzungumza na kila mmoja alimsifu na kumpongeza Rais Magufuli pia kwa uamuzi wa kuwaalika katika hafla hiyo ya kihistoria. Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi alisema amefurahishwa na Magufuli anavyoendesha taifa na alimtaja kuwa ni mkarimu, mvumbuzi anayetumia kichwa chake kutafakari na kubuni mambo yanayotekelezeka.

“Sote tumefurahi kuona namna anavyoliendesha taifa letu kwa aina mpya mpya na nzuri nzuri. Ningependa na mimi nitoe shukurani za hadharani kwa Magufuli kwa yote anayoyatenda na nimalizie kwa kumshukuru tena kwa ukarimu wake, ni mtu mkarimu, mvumbuzi, anatumia kichwa chake kutafakari na kubuni sana na kwa yote anayoyabuni yanakwenda vyema,” alisema.

Mbele kwa mbele Kwa upande wake, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, alimueleza Rais Magufuli “mbele kwa mbele, endelea hivyo” na alimshukuru kwa uaminifu wake kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali, kutokana na kutekeleza vizuri Ilani ya CCM.

Mkapa alisema, “Mengi yamesemwa na yataendelea kusemwa, mazuri ambayo rais wetu anatekeleza kutimiza Ilani ya chama… katika uamuzi huo, hili la kujenga ofisi za Ikulu hapa Chamwino ni muhimu sana.”

Alisema marais wote kwa awamu zao, walipokea uamuzi wa Chama, kwamba serikali ihamie Dodoma na kwamba aliyemtangulia alifanya kila jitihada kuhamisha baadhi ya taasisi.

Alisema pia yeye aliendeleza jitihada hizo, ikiwa ni pamoja na kujenga Jengo la Pius Msekwa na aliyemfuata alifanya uamuzi mzito, ikiwa ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa Bunge na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

“Dk Magufuli amefanya mengi ya hayo na mazito zaidi,” alisema Mkapa na kupongeza mabadiliko makubwa, yaliyofanyika katika mji wa Dodoma na kusisitiza ndiyo maana alipoalikwa kushuhudia jiwe la msingi, hakusita kushiriki.

Kikwete Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alieleza historia ya uamuzi wa kuhamishia makao makuu Dodoma. Alipongeza ujenzi huo kwa kusema ni uamuzi wa busara, hekima na kusema yeye na marais wenzake wastaafu, wameshangazwa na mambo mazuri yaliyokwishafanyika. Alisema uamuzi wa makao makuu kuwa Dodoma, ulifanywa kidemokrasia mwaka 1971 na ulikuwa shirikishi kwa mikoa yote ambayo iliridhia isipokuwa Pwani.

Akieleza mchakato wa utekelezaji katika awamu yake, alisema waliamua kujenga UDOM na Ikulu kujengwa Chamwino. Alisema hiyo ilikuwa ni hatua ya fikra na utekelezaji ameufanya Magufuli.

“Hiyo ilikuwa hatua ya fikra, lakini mpango si matumizi. Sasa tumepata mtu aliyefanya mpango kuwa matumizi. Rais hongera sana. Na mimi nilipoanza kusikia kwamba wizara za serikali zinajengwa, nikasema sisemi neno, kwa maana Ikulu itabaki kuwa Chamwino,” alisema.

Katika hafla hiyo, mtoto wa Rais wa Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, Makongoro aliyezungumza kwa niaba ya mama yake, Mama Maria, alishukuru utashi wa Rais Magufuli wa kujenga Ikulu ya aina yake.

“Una utashi wa aina fulani mpaka na corona imekukimbia,” alisema Makongoro.

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi