loader
Mti mmoja haufanyi msitu

Mti mmoja haufanyi msitu

MTI mmoja haufanyi msitu. Tumeanza kuziona ishara za baadhi ya vyama vya siasa kufanywa kuwa taasisi zinazoongozwa na matakwa ya mtu mmoja, liwake jua, inyeshe mvua.

Anachotaka mtu huyo ndiwe kiwe. Hali ya kuwa na ‘Chama Mtu’ na si ‘ Chama Watu’. Duniani hapa ushindani wa kisiasa mara nyingi unahusu vyama.

Tatizo kuna wanaoingia katika ushindani wa kisiasa kupitia vyama na huku wakijua, lakini wakipuuzia dhana ya chama. Na tuanze kwa kujiuliza Je, chama cha siasa ni nini? Katika harakati za kisiasa kuna aina mbili za vyama; Chama cha Ukombozi na Chama cha Uongozi.

TANU, Frelimo, ANC ni mifano ya vyama vya ukombozi vilivyokuja kugeuka kuwa vyama vya uongozi. CCM, CUF, Chadema ni mifano michache ya vinavyopaswa kuwa vyama vya uongozi, ingawa baadhi vimeanza kubeba taswira ya ‘vyama mtu’.

Chama imara cha ukombozi kinatakiwa kijenge uwezo wa kuwa chama cha uongozi mara ile kitapotwaa madaraka. Hufanya hivyo kwa kuweka mkazo juu ya mafunzo kwa makada wake.

TANU, Frelimo na ANC viliweza kujenga uwezo huo. Kielelezo cha nguvu na umakini wa chama cha kisiasa ni wingi na ubora wa makada wake.

Chama ni makada kwa vile chama ni itikadi, malengo na shabaha na wala si nasaba na umaarufu wa mtu mmoja mmoja ndani ya chama. Chama chenye makada wengi wenye kuielewa itikadi, malengo na shabaha ya chama, huwa hakimtegemei mtu mmoja katika kuwepo kwake.

Hakimtegemei mtu mmoja katika kufanikisha ushindi wa chama. Hakimtegemei mtu mmoja katika kuhamasisha wanachama au umma. Chama hicho hujiamini.

Edward Mondlane, kiongozi wa kwanza wa Frelimo alipouawa kwa bomu la barua, Frelimo walijua watafanya nini, walijua mchakato gani utumike katika kumpata mrithi wake. Na hata Samora Machel, alipotoweka ghafla kwa ajali ya ndege, Frelimo walijua watafanya nini.

Na kama Nyerere angekufa wakati wa TANU, bila shaka, TANU walikuwa wamejiandaa vema nini cha kufanya.

TANU haikuwa na ukame wa jeshi la makada. Nguvu ya Frelimo kama ilivyokuwa kwa TANU zilikuwa ni makada wake. Na ieleweke kuwa, makada ni roho ya chama.

Chama kikianza kupungukiwa na idadi ya makada wake wakereketwa, basi, chama hicho hakina mustakabali ulio salama, kitayumba na pengine kuangukia kaburini. Tuangalie basi mfano wa chama kisichokuwa na nguvu ya makada bali nguvu ya mtu mmoja.

Wakati John Garang wa SPLM alipokufa kwa ajali ya ndege, hakuna ndani ya SPLM aliyekuwa na hakika ya nini kifanyike. Kwamba ni mke na mtoto wa John Garang waliosimama mbele ya kamera za waandishi wa kimataifa kujaribu kuelekeza nini John Garang angependa kifanyike kilidhihirisha udhaifu wa SPLM.

Kwamba SPLM ni John Garang na kinyume chake, SPLM ilikuwa ni chama mtu. Na je, siasa ni nini? Mara nyingi hatujiulizi swali hili. Kwenye kitabu chake cha mwaka 1962;

‘TUJISAHIHISHE’, Mwalimu Julius Nyerere anaandika: “Nataka kutaja makosa machache ambayo mara nyingi huzuia umoja wowote kuwa imara hata ushindwe kutimiza madhumuni yake. Ukiondoa matatizo wayapatayo binadamu kwa sababu ya mambo kama mafuriko, nzige, kiangazi, nk, matatizo yao mengi hutokana na ubinafsi”

“Swali ambalo twalisikia mara kwa mara; Hali yetu ya baadaye itakuwaje? Mtu anayeuliza anafikiri kuwa TANU iliundwa kwa faida yake yeye binafsi. Ni kama kwamba TANU ilipoundwa ilimwahidi kwamba ikiwa atakubali kuwa mwanachama au kiongozi, basi, TANU itamfanyia yeye jambo fulani kama tuzo!

Anasahu kabisa kuwa TANU inajishughulisha na haja za jumuiya kwa ujumla. Lakini, kwa mtu wa aina hiyo, hata kama TANU inatimiza madhumuni yake ya jumuiya, ataona kuwa ni umoja ambao hauna maana kwa sababu haumtimizii haja zote za nafsi yake! Huu ni ubinafsi.”

“Kama wanachama wa TANU na hasa viongozi, hawatakihukumu chama chetu kwa mahitaji ya jamii yao, bali watakihukumu kwa mahitaji ya nafsi zao wenyewe, chama hakitadumu. Wanachama wa aina hiyo ni ugonjwa katika chama.”

Mwalimu Nyerere anaendelea; “Dalili nyingine ya ubinafsi na ambayo ni ugonjwa mbaya sana, ni fitina. Kanuni moja ya TANU inasema; ‘Nitasema kweli daima. Fitina kwangu ni mwiko.’

Lakini bado tunao wanachama ambao ni wafitini wakubwa bila kujitambua.” (J.K Nyerere ‘Tujisahihishe 1962’). Siasa ni hatua za majadiliano endelevu. Majadiliano yasiyokoma.

Hakuna kitu kibaya katika siasa kama kutafuta njia za mkato katika kufikia Malengo. Njia hizi zina gharama kubwa kwa jamii. Njia za mkato uhusisha hoja za nguvu, hila na hata vitisho.

Ni kweli kuwa, demokrasia na amani katika jamii huenda isiwepo bila wachache kukubali matakwa ya wengi. Matakwa ya wengi hujulikana kwa njia ya mazungumzo ya wazi wazi, kwa mbinu za wazi kisiasa.

Vivyo hivyo, kinyume chake, yaani matakwa ya wachache. Hata baada ya majadiliano, baada ya uchaguzi, wachache walioshindwa wanapaswa kukubali kushindwa.

Wanapaswa kufanya hivyo kama kulikuwepo na uhuru na haki katika majadiliano na hata uchaguzi. Hata hivyo, kukubali kwao kushindwa hakuwanyimi haki yao ya kuendelea kuamini katika kile walichokiamini.

Hapa demokrasia inawapa haki watu hawa na ukweli unawapa wajibu wa kuyaendeleza mawazo yao hadi pale walio wengi wayakubali.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/46e98f051887ee9e490c5bad5f4685d7.png

NIPO nyumbani kwa Baba na Mama Chichi. ...

foto
Mwandishi: Maggid Mjengwa

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi