loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Malkia wa Peramiho ametutoa matopeni'

KATIKA Mkoa wa Ruvuma, jina “Malikia wa Peramiho’ ni maarufu hata kwa watoto wasiojua maana ya malkia. Hata hivyo, linapotajwa akilini mwao wote humtazama Mbunge wa Peramiho kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jenista Mhagama.

Wananchi wa kada mbalimbali jimboni Peramiho, wanamzungumzia Jenista Mhagama kwa namna mbalimbali, mradi tu, wanamkumbuka na kumshukuru kwa utumishi na uwakilishi uliotukuka alioufanya kwa kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali kutekeleza miradi ya maendeleo hasa kuimarisha huduma za afya maana afya ni mtaji wa yote.

Ilani ya Mbunge huyo ya mwaka 2015 kuhusu huduma za afya inasema huduma za afya ni haki ya kila mwananchi huku Ilani ya CCM na Sera ya Taifa ya Afya ya Mwaka 2015 -2020 ikitaka kuwapo zahanati kila kijiji na kituo cha afya kila kata.

Kuyathibitisha haya, Katibu wa CCM wa Wilaya ya Songea Vijijini, Mohamed Lawa, anasema Jenista ni mbunge na mwanamke kiongozi wa kipekee ambaye mapenzi yake kwa wananchi wake, ni ya wazi, yasiyofichika na yanayogusa hisia za wote wanawake kwa wanaume; wazee kwa vijana; wadogo kwa wakubwa; maskini kwa tajiri; wasomi kwa wasiosoma mradi tu, na kiongozi anayepigania ustawi kwa watu wake wote.

Anasema: “Kwa kweli ni kiungo kizuri sana kati ya wananchi wa Permiho, viongozi na serikali; anayependa kuona kero zikitatuliwa haraka na kwa njia bora zaidi.” Anaongeza: “Anapenda kuona wananchi wanyonge wakiondokana na umaskini na badala yake, wanaingia katika maisha ya kawaida yaliyo bora na ndiyo maana amefanikiwa kutekeleza Ilani kwa asilia 97.”

“Kwa kweli mimi na chama changu hapa Songea Vijijini tunajivuna kuwa na mbunge huyu mwanamke anayeonesha nguvu na uwezo wa wanawake katika uongozi kwani ni wa kipekee na amekuwa akijitoa sana kusaidia wananchi wanyonge na hata chama.”

Anasema sapoti ya mbunge kwa wananchi wa Jimbo la Peramiho ni kubwa na amegusa kila eneo kwa kupeleka misaada ya vifaa kwa gharama zake binafsi ili kupeleka maendeleo

MGANGA MKUU

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Songea, Dk Lucia Kafumu anasema, kwa jitihada za Mbunge huyo, Serikali imejenga Hospitali ya Wilaya ya Songea katika Kijiji cha Mpitimbi B kwa Sh bilioni 1.5.

“Tayari ujenzi wa wodi ya wazazi, OPD (wagonjwa wa nje), chumba cha upasuaji, maabara na chumba cha ufuaji umeanza,” anasema Dk Lucia.

Anasema Awamu ya Tano, zahanati 10 zimekarabatiwa na kuboreshwa na zimeanza kutoa huduma. Jimbo la Peramiho lina kata 16. Kila kata ina zahanati. Zipo zahanati 35 huku 22 zikiwa za serikali.

Mganga Mkuu huyo anamshukuru Mbunge wa Peramiho kwa kupeleka misaada ya mabati na saruji kwenye miradi mbalimbali ya afya na kwamba hivi karibuni alitoa misaada ya ndoo za kunawia mikono, vitakasa mikono kwa ajili ya kuwakinga wanachi wasipate ugonjwa wa corona.

HALMASHAURI YA SONGEA

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Songea, Rajab Mtiula, anasema: “Serikali na mbunge wetu wamejitahidi kutatua kwa karibu asilimia 87 ya changamoto nyingi za kiafya zilizokuwapo hapa jimboni; serikali imepeleka fedha za kumalizia miradi viporo ya vituo vya afya vya Nakahegwa, Lipaya, Mpingi na Lugagala na Mbunge ametoa pesa kusaidia miradi mbali mbali ikiwemo ya ujenzi wa zahanati za vijiji mbalimbali.”

Anamshukuru Mbunge Jenista kwa kujitoa kwa michango binafsi ya mabati, saruji, fedha, vifaa vya hospitali vikiwemo vitanda vya kujifungulia na mashuka kwani hakuna kata ambayo hajatoa mchango wake.

MADIWANI

Diwani wa Kata ya Mhukuru, Simon Kapinga, anasema wakati Jenista wanaingia madarakani 2015, changamoto kubwa katika Kata ya Mhukuru ilikuwa huduma za afya, lakini kwa ushirikiano wa Mbunge Jenista na Serikali Kuu, wameondoa changamoto hizo na sasa zimekuwa historia.

“Juhudi na uwezesho mkubwa wa Mbunge huyo, ndizo zimetuwezesha kupata kituo chetu cha afya Mhukuru na sasa tunapata huduma za afya na matibabu na upasuaji unafanyika. Kwa kweli Jenista Mhagama ni mbunge ambaye hatutamsahau maishani kwetu na ndiyo maana tunamwita Malkia wa Peramiho kwani amekuwa mkombozi aliyetutoa kwenye tope zito,” anasema.

Kwa mujibu wa Diwani Kapinga, awali wananchi walilazimika kusafiri umbali wa takriban kilometa 80 kufuata huduma za afya katika Hospitali ya Misheni ya Peramiho au Hospitali ya Songea Mjini.

“Hali hii ilikuwa mateso makubwa kwa wagonjwa na hata wajawazito na ugumu na umbali huu uliwafanya wagonjwa wengine wakiwamo wajawazito wengi kupoteza maisha hasa waliolazimika kuhitaji huduma za dharula za upasuaji au kuongezewa damu,” anasema Kapinga. Anapofafanua namna walivyonufaika na mwakilishi wao huyo katika Bunge, Diwani Kapinga anasema:

“Mheshimiwa Jenista Mhagama ametusaidia sana mpaka tumetatua changamoto hiyo maana ametusaidia kwa kutuchangia vitanda vya kujifungulia wajawazito katika zahanati ya kijiji; na mashuka ya wagonjwa katika kata yangu ya Mhukuru Lilai. Pesa binafsi alizochangia ni zaidi ya Sh milioni 35 katika kata yangu. Kwa kweli tunamshukuru sana. Tunataka viongozi kama huyu ‘mama.”

Anaongeza: “Kwa kweli Jenista ni mbunge pekee aliyeweza kuibadilisha Mhukuru na kuiletea maendeleo katika sekta za afya, maji, barabara na hata mawasiliano.”

Naye Diwani wa Kata ya Mpitimbi, Issa Kindimba, anasema juhudi, utumishi unaozingatia ushirikishwaji wa wananchi aliouonesha Jenista, ni miongoni mwa mbinu sahihi alizotumia Jenista kuleta matokeo chanya katika huduma za afya ambazo kimsingi, zimeboreshwa jimboni humo.

WANANCHI

Mkazi wa Mgazini katika Kata ya Kilagano, Dickson Ngonyani, anasema kuwa na Jenista Mhagama kama mbunge, ni kuwa na maendeleo jimboni Peramiho.

“Mama Mbunge anasifika sana hapa jimboni kwa kusimamia maendeleo na kila mara amekuwa karibu yetu wananchi wake licha ya kuwa na majukumu mengine ya kitaifa. Hili linatufanya tukiri kuwa ni kiongozi bora asiyesahau wananchi wake hata anapopata wadhifa mkubwa serikalini,” anasema.

Naye Athuman Ibadi anasema mbunge huyo amewsaidia kuondokana na adha ya kutumia muda na pesa nyingi kutafuta matibabu sehemu za mbali na pia, anatumia muda mwingi kuwa na wananchi na kushirikiana nao kutatua kero mbalimbali.

Anasema ili kuboresha huduma za afya, ujenzi wa Zahanati ya Lipaya iliyopo kijijini Mpitimbi inayoenda kuwa kituo cha afya unaendelea vizuri. Tayari wataalam wameshapelekwa na wakati wowote kitaanza kutoa huduma kwa wananchi.

Haya ni mafanikio makubwa. Uchunguzi umebaini kuwa, katika kuhakikisha huduma za afya zinaimarika katika jimbo lake, katika Zahanati ya Mpitimbi A, Mbunge Jenista ametoa mabati 150 yenye thanani ya Sh 4,000,000 na pesa taslimu Sh 2,800,000 ili kununua vifaa vingine ikiwemo saruji.

Kukamilika kwa ujenzi wa Zahanati ya Mpitimbi, kutawaondolea wananchi wa eneo hilo kero ya kutembea takriban kilometa 15 kutafuta huduma za afya katika maeneo ya Songea Mjini.

Mkazi wa Peramiho ‘A’, Elizabeth Hyella, anasema kabla Jenista hajawa mbunge wao, Jimbo la Peramiho lilikuwa na kero kubwa na nyingi katika huduma za afya, hali iliyowakatisha tamaa kimaisha.

Anasema kero hizo ni pamoja na ukosefu wa huduma za upasuaji kwa wajawazito katika maeneo ya karibu, na wananchi kulazimika kutumia pesa nyingi kukodi pikipiki kwenda kutibiwa mjini lakini sasa huduma hizo zinapatikana katika maeneo yao kunakopatikana wataalamu na dawa.

“Kwa kuzifanya huduma za afya kuwa kipaumbele cha kwanza na tukaungana naye, tumezidi kumpenda mbunge wetu; Malkia wa Peramiho ameboresha sana huduma za afya jimboni Peramiho,” anasema Elizabeth.

Anaongeza: “Amejibu kiu yetu sasa kila kijiji kina zahanati na karibu kata zote kuna vituo vya afya na wanawake sasa tunajifungua kwenye vituo vya afya karibu yetu; kwa kweli amekuwa karibu kutusikiliza na kutatua kero zetu mbalimbali.”

ASEMAVYO MBUNGE JENISTA

Alipoulizwa anamudu vipi kuwatumikia wanajimbo wake licha ya majukumu mengine ya kitaifa, Jenista anasema: “Kila jambo linataka utashi na mipango sawia; hata uwe wapi, lazima utenge muda wa kutumikia watu wako jimboni, na uwe tayari kusikiliza kero zao na kushirikiana nao kuzitatua.” Jenista ambaye kwa sasa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu) anasema:

“Huu ndio msingi wangu katika kutumikia wanajimbo na hata Mwenyekiti wa CCM, Kitaifa, Rais John Magufuli, hilo ndilo analohimiza wanaCM tuwafanyie wananchi maana walituamini na kutupatia ridhaa ya kuongoza…”

Akizungumzia michango yake binafsi aliyotoa kuchangia sekta ya afya jimboni mwake anasema hadi sasa ametumia pesa nyingi (anakataa kutaja kiasi) kusapoti miradi ya afya katika kata zote ambapo hakuna kata ambayo hajaisaidia.

Anasema,wakati anaingia madarakani kulikuwa na zahanati 10 pekee, lakini sasa kila kijiji kina zahanati isipokuwa baadhi ya zahanati zinakamilisha ujenzi ikiwemo zahanati ya Mpitimbi A, Nyamechini, Mipeta, Matama na Mhepai. Mintarafu vituo vya afya anasema: “Nilikuta kituo kimoja, lakini sasa tumeongeza vituo vitano na tayari tumepata fedha za kukamilisha vituo hivyo.”

Anasema Kituo cha Afya Mhukuru, kimekamilika na kinatoa huduma za upasuaji na kwamba kituo cha Magagura,Matimila vipo kwenye hatua ya ujenzi na vituo cha Lugagala, Nakahegwa, Lipaya vimeanza kufanya kazi bila upasuaji wakati kituo cha Mpingi kinangoja vifaa kianze kutoa huduma.

“Nashukuru sana Serikali na wananachi wa Jimbo la Peramiho kwa ushirikiano wanaonipa na kwa kuunga mkono kwenye miradi ya maendeleo na ndiyo maana tumeweza kutatua changamoto zetu kwa pamoja; nitaendelea kusaidiana nao kutatua kero mbalimbali zinazowakabili ili kuleta maendeleo ya kweli katika jimbo letu,” anasema Jenista.

Anasema, kwa kushirikiana na wananchi na Serikali wamefanikiwa kujenga zahanati 4 na vituo vya afya vinne na sasa Hospitali ya Wilaya ya Songea kijijini Mpitimbi B inayogharimu Sh bilioni 1.5.

Anavitaja vituo vya afya vilivyojengwa kuwa ni Lilai (Sh milioni 500), Magagula (Sh milioni 400) na Matimila (Sh milioni 400); pamoja na Zahanati ya Lugagala ambayo imepandishwa hadhi kuwa kituo cha afya.

Anasema kipaumbele chake kikubwa ni kuhakikisha huduma za afya katika Jimbo la Peramiho zinaimarika kwa kushirikiana na viongozi wengine wa jimbo wakiwamo madiwani, viongozi wa kata na vijiji na wananchi kwa jumla.

“Jambo kubwa linaloniumiza ni pale unapoona mtu anateseka au hata kufa kutokana na ukosefu wa huduma za afya; inauma sana na ndiyo maana hata Rais Dk Magufuli amehakikisha huduma za afya nchini zinaimarishwa kwa kiasi kikubwa,” anasema.

SIGARA ina kemikali zaidi ya 4,000 ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi