loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Serikali kufanya mabadiliko kadhaa ya kodi mbalimbali

SERIKALI imependekeza maeneo 16 ya kufanya mabadiliko kadhaa ya kodi mbalimbali, ikiwamo sheria ya mapato ili kuwapa nafuu ya kuondoa kodi katika mshahara wa mfanyakazi wa kima cha chini, msamaha katika Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye bima ya mazao na ulazima wa kusajili ardhi.

Mapendekezo hayo pia yameongeza Ushuru wa Forodha kwenye bidhaa mbalimbali zinazotoka nje ya nchi ikiwamo marumaru, kakao, chai, nyama, maji, mitumba, peremende na mafuta ya kula ili kulinda viwanda na huku bidhaa za ndani zikinufaika kutokana na punguzo ikiwamo vifungashio vya korosho, pamba na kahawa ili kulinda viwanda vya ndani.

Akisoma mapendekezo ya mapato na matumizi ya bajeti ya Serikali ya mwaka 2020/2021 jijini Dodoma jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliliomba Bunge liridhie jumla ya Sh trilioni 34.88. Kuhusu mapato ya jumla ya wafanyakazi, Dk Mpango alisema Serikali inapendekeza kupandisha kiwango cha mapato ya waajiriwa ili kuongeza kiwango cha mapato yasiyotozwa kodi kutoka Sh 170,000 kwa mwezi hadi Sh 270,000 (sawa na kutoka sh 2,040,000 kwa mwaka hadi sh 3,240,000.

Awali ilikuwa kiwango cha Sh 170,000 kwa mwezi kisichokatwa kodi. Mchanganuo wa mapato hayo na asilimia zake ni kwamba mapato ya jumla yasiozidi Sh 3,240,000 hayatatozwa kodi, asilimia tisa itatozwa kwa kiwango kinachozidi Sh 3,240,000, asilimia 20 ya kinachozidi Sh 6,240,000, asilimia 25 ya kinachozidi Sh 9,120,000 na asilimia 30 ya kiwango kianchozidi Sh 12,000,000.

“Lengo la mabadiliko hayo ni kutoa unafuu wa Kodi ya Mapato kwa wafanyakazi. Hatua hii pekee inatarajiwa kupunguza mapato kwa shilingi milioni 517.2,” alisema Dk Mpango.

Alisema Serikali inataka kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura 148 kama ifuatavyo ili kusamehe kodi hiyo kwenye bima ya kilimo cha mazao lengo la hatua hiyo likiwa ni kupunguza gharama na kutoa unafuu katika bima za kilimo ili kuwawezesha wakulima bima shughuli za kilimo na kuvutia wananchi kutumia huduma za bima kwa ajili ya kujikinga na majanga mbalimbali yanayoathiri shughuli zao za kilimo mfano ukame na mafuriko.

“Hatua zote za Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa ujumla wake zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 46,” alisema Dk Mpango.

Mapendekezo mengine ni kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye vifungashio vya kuhifadhia kahawa, korosho na pamba, vinavyotumiwa na viwanda vya kusaga kahawa nchini ili kuongeza thamani ya zao hilo na kuwapa unafuu viwanda vya ndani.

Alisema serikali inapendekeza pia kufuta msamaha wa Kodi ya Mapato kwa wazalishaji walio ndani ya maeneo maalum ya kiuchumi, wanaozalisha bidhaa na kuuza ndani ya nchi kwa asilimia 100 ili kuweka usawa katika utozaji wa kodi ya mapato baina ya wazalishaji wa bidhaa walio nje na walio ndani ya maeneo maalum ya kiuchumi. Kuruhusu michango ya wadau kwenye Mfuko wa Ukimwi, Serikali ilipendekeza isitozwe kodi ya Mapato .

“Aidha, napendekeza pia michango iliyotolewa na wananchi kwa Serikali na itakayoendelea kutolewa katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu ( Covid -19) isitozwe kodi hadi hapo serikali itakapotangaza kuisha kwa ugonjwa huu.

Imependekezwa maduhuli yatokanayo na sekta ya utalii na mazao ya misitu, yakusanywe na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na mapato yaingie katika mfuko Mkuu wa Hazina Ilipendekezwa pia kuwa kuendelea kusamehe ushuru wa forodha kwenye malighafi, vipuri na mashine vinavyotumika katika kutengeneza viatu vya ngozi na nguo.

Dk Mpango alisema Ushuru wa Forodha umeongezwa kwenye bidhaa mbalimbali zinazotoka nje ikiwamo marumaru, kakao, chai lengo likiwa ni kulinda viwanda na bidaha za ndani huku bidhaa za ndani zikinufaika kutokana na punguzo.

Bidhaa zilizopunguzwa ushuru ni pamoja na vifuniko vya chupa za mvinyo kutoka asilimia 10 hadi asilimia 0; vifungashio vya kuhifadhia kahawa asilimia 25 hadi asilimia 0. Nyingine ni vifungashio vya kuhifadhia korosho na vya pamba.

Punguzo limefanyika kwenye mashine za kielektroniki zinazotumika kukusanya mapato ya Serikali (EFDs) na Vifungashio vinavyotumiwa na wazalishaji wa maziwa kwa joto la juu kutoka asilimia 25 hadi tisa. Zilizoongezewa Ushuru wa Forodha ni marumaru kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35; Chai kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35; magunia kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35; kakao kutoka asilimia tisa hadi asilimia 10.

Ushuru utaendelea kutozwa kwa asilimia 0 kutoka kiwango cha awali cha asilimia 25 kwenye malighafi za kutengeneza taulo za watoto kuleta unafuu kwa gharama za uzalishaji, kuongeza ajira na mapato ya Serikali.

Mapendekezo mengine ni marekebisho ya Ushuru wa Bidhaa kwenye bia za unga kwa Sh 844 lengo likiwa ni kupanua wigo wa kodi kwa kuwa bidhaa hizo zinaagizwa kutoka nje. Imependekezwa pia kutoza ushuru wa bidhaa kwenye juisi za unga kwa Sh 232 kwa kilo inayoagizwa kutoka nje.

Mapendekezo mengine ni kwamba waziri mwenye dhamana ya masuala yanayohusu Serikali za Mitaa kukusanya tozo ya huduma ya asilimia 0.3 ya mapato ghafi kwenye sekta ya mawasiliano kwa niaba ya halmashauri na kuyagawa kwa halmashauri zote ndani ya siku 14 baada ya kukusanywa.

Hatua hiyo inatajwa kwamba itasaidia kuziondolea kero baadhi ya Halmashauri ya kukosa mapato kutoka kwenye chanzo hiki na kupunguza usumbufu wa ufuatiliaji wa kila Halmashauri kwenye Makao Makuu ya Makampuni yanayotoa huduma za mawasiliano nchini.

TRAFIKI Kanda Maalum Dar es Salaam imese- ma ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi