loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Miaka mitano ya nguvu sekta ya madini Tanzania

AKIHUTUBIA Bunge la 11 mjini Dodoma, Novemba 20, 2015 kwa mara ya kwanza, Rais John Magufuli alizungumzia kero kadhaa alizokutana nazo wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo.

Alisema kuna maeneo yaliyolalamikiwa zaidi na wananchi na kuyataja baadhi, likiwamo tatizo rushwa alilosema limelalamikiwa sana karibu maeneo yote yanayogusa wananchi.

Kwa Tamisemi, alisema upotevu wa mapato, kushindwa kukusanya kodi, ubadhirifu, matumizi mabaya ya fedha na utekelezaji wa baadhi ya miradi chini ya viwango, wizi, uzembe, n.k; ni miongoni mwa malalamiko wakati katika ardhi, ilikuwa ni migogoro ya wakulima na wafugaji, viwanja, kuhodhi maeneo bila kuyaendeleza, mipango miji, kujenga maeneo ya wazi, n.k, wakati bandari ni rushwa, wizi, ubadhirifu na urasimu.

Katika madini, Rais Magufuli alisema kero ni wenyeji kutofaidika, vilio vya wachimbaji wadogo wadogo kutengewa maeneo ya uchimbaji na kupatiwa mikopo, kutolipa kodi stahiki, usumbufu kulipa fidia, n.k.

“Kero hizi tutazishughulikia kwa nguvu zetu zote. Wizara, ofisi na taasisi husika zijipange ipasavyo kutatua kero hizi. Nimetaja baadhi ya kero hizi ili wabunge mzitambue na mshirikiane na serikali na wadau wengine tuzitatue haraka,” akasema Rais Magufuli.

Takriban miaka mitano sasa tangu atoe kauli hiyo, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli imefanya mapinduzi makubwa katika sekta ya madini ambako sasa Taifa linafaidika na rasilimali hiyo.

Kwa mfano, hivi karibuni ilibainika kuwa serikali imevunja rekodi katika mapato kwenye sekta ya madini kutokana na mageuzi makubwa yaliyofanywa katika sekta hiyo. Msemaji Mkuu wa serikali, Dk Hassan Abbasi, anasema katika mwaka huu wa fedha, serikali ilipanga kukusanya mapato katika sekta ya madini yanayofikia Sh bilioni 470, lakini hadi Mei 31, 2020, mwezi mmoja kabla ya mwaka wa fedha kuisha, ilivuka lengo kwa kukusanya Sh bilioni 479.45.

“Moja ya maeneo ya mageuzi ya Dk Magufuli ni kwenye sekta ya madini. Alipoahidi mabadiliko ya kweli kwenye kampeni, alizungumzia mageuzi kuhakikisha si tu tunakuwa na madini na kubaki na mashimo, bali yanakuwa na manufaa kwa Watanzania,” alisema Dk Abbasi.

Dk Abbasi ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, anasema hata hivyo baadaye baadhi ya watu walianza kutoa vitisho ikiwemo kudai kuwa hatua zilizochukuliwa kuhakikisha kunakuwa na mabadiliko hayo, zinaweza kuipeleka nchi pabaya jambo ambalo halikutokea.

“Baadaye tukaanza kutishana, leo kwa maana ya kufanya dhukuru (Tafakuri) tunapozungumzia sekta ya madini hakuna kupelekwa miga wala mwiba, mageuzi yamefanyika, mikataba karibia kampuni zote kubwa imeanza kufanyiwa kazi, imeanza kupitiwa ili kuhakikisha nchi inafaidika,” anasisitiza.

Anasema katika eneo ambalo serikali imepata mafanikio makubwa ni kukubaliana na Kampuni ya Barrick na kwa pamoja wakaunda kampuni ya pamoja ya Twiga Minerals Corporation Limited.

“Kwa mara ya kwanza tunamiliki kampuni, sisi na mwenye mtaji na sisi ndio wenye madini,” anasema Abbasi.

Anasema kampuni hiyo imeanza kufanya kazi ambapo pia, serikali imelipwa Sh bilioni 250 kama sehemu ya mabilioni mengine yanayokuja.

“Tutapata kodi nyingi, tutalipwa hisa zetu kwa jumla si tu kumiliki hisa zile 16 kama hisa za Twiga Minerals, lakini manufaa ya kiuchumi yatakwenda kwenye 50 kwa 50 na kuna wakati tutakuwa tunazidi kidogo,” anafafanua.

Anasema sekta ya madini ilivyokuwa na sasa, imekuwa na mageuzi makubwa ikiwemo Rais Magufuli kuzuia makaboni, kuanzisha masoko ya madini na sasa kila mkoa makusanyo na mapato yameongezeka.

Mafanikio haya, ni miongoni mwa mambo yaliyokuwa yamebainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa Mwaka 2015-2020. Moja ya taasisi zilizochangia mafanikio hayo ni Tume ya Madini iliyoundwa kwa mujibu wa Sheria ya Madini Sura ya 123 ikiwa na majukumu mbalimbali ikiwemo kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli ya serikali yatokanayo na rasilimali madini; kuimarisha ukaguzi wa masuala ya usalama, afya na mazingira.

Majukumu mengi ni uzalishaji na biashara ya madini katika migodi midogo, ya kati na mikubwa; kudhibiti utoroshaji wa madini; na kuendelea kuboresha mazingira ya kuwawezesha wananchi kufaidika na rasilimali madini.

Tangu kuundwa kwake, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini imefanya jitihada mbalimbali katika kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa madini ikiwamo wizara kutenga maeneo sita kwa ajili ya wachimbaji madini wadogo yenye jumla ya ukubwa wa hekta 38,951.88. Maeneo 13 yenye ukubwa wa hekta 22,970.00 yamependekezwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo.

Maeneo hayo yapo Msasa na Matabe mkoani Geita, Biharamulo na Kyerwa mkoani Kagera, Itigi mkoani Singida, D-Reef, Ibindi na Kapanda mkoani Katavi, Ngapa mkoani Songea, Nzega mkoani Tabora na Kitowelo mkoani Lindi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Tume ya Madini, ukaguzi wa migodi katika masuala ya usalama, afya na utunzaji wa mazingira umeimarishwa kwa kufanya ukaguzi katika migodi mikubwa, ya kati na midogo.

“Serikali kupitia Tume ya Madini imeweka wakaguzi wa madini katika migodi yote mikubwa na ya kati nchini ili kuhakiki kiasi na thamani ya madini yanayozalishwa na kusafirishwa nje ya nchi,” inasema taarifa ya Tume ya Madini.

“Kifungu cha 25(2) na 100 cha Sheria ya Madini Sura Namba 123 kinaweka sharti la kisheria kuwa kila mgodi mkubwa au wa kati lazima uwe na ofisa mgodi mkazi ili kusimamia na kukagua shughuli za migodi. Uwekaji wa mfumo huu umesaidia serikali kupata takwimu sahihi za madini yanayozalishwa na kuuzwa na migodi husika na hivyo kukusanya mapato yake kwa usahihi zaidi,” anasema.

Inaeleza kuwa, migodi mikubwa ya dhahabu inayosimamiwa kwa karibu na inayofanyiwa ukaguzi wa mara kwa mara ni Bulyanhulu Gold Mine Limited (Kahama), Geita Gold Mining Limited (Geita), North Mara Gold Mine Limited (Tarime), Shanta Mining Company Limited (Songwe), Stamigold Company Limited (Biharamulo), na Pangea Minerals Limited (Kahama).

Aidha, wizara imeweka utaratibu wa kutoa vibali vya kusafirisha madini nje ya nchi vinavyotolewa na maofisa maalumu walioteuliwa walioko chini ya Tume ya Madini. Mintarafu madini ya vito, serikali imeweka utaratibu wa kuhakikisha maofisa wa serikali wanakuwa katika maeneo husika wakati wa kuchambua madini yote ya almasi (kwa Mgodi wa Williamson Diamond Limited (WDL) na El Hilal) na tanzanite kwa machimbo ya Mirerani na kuchukua takwimu zake.

Aidha, serikali hufanya uthamanishaji wa madini husika kuwezesha tozo na malipo mengine stahiki kufanyika. Wizara kupitia Tume ya Madini inayoongozwa na Katibu Mtendaji, Profesa Shukrani Manya, imekuwa ikifanya ukaguzi wa kimkakati wa madini katika maeneo ya wachimbaji wa kati na wadogo ili kupata takwimu sahihi za uzalishaji katika migodi husika na kutumia taarifa hizo kulinganisha na takwimu za uzalishaji madini zinazowasilishwa serikalini na wahusika.

Kutokana na ukaguzi huo, serikali ilifanikiwa kukusanya mrabaha stahiki wa Sh 10,098,979,246.56 na ada ya ukaguzi Sh 3,316,360,392.38 zilizotokana na uzalishaji na mauzo ya tani 23,596,994.70 za madini ujenzi na tani 1,022,958.57 za madini ya viwandani ya Sh 336,632,641,554.24.

Takwimu za Tume ya Madini zinaonesha kuwa, hadi kufikia Machi 2020, migodi 123 ilikuwa imekaguliwa. Kati ya hiyo, migodi mikubwa ilikuwa ni Geita Gold Mining Limited (Geita), North Mara Gold Mine Limited (Tarime), Bulyanhulu Gold Mine Limited (Kahama), na Pangea Minerals Limited (Kahama).

Migodi minne ya kati ni Buswola Mining- Geita, Nyarugusu Mining-Geita, ZEM Minerals Development Ltd-Shinyanga, ZEM Minerals Development Ltd- Musoma; na migodi midogo 115.

Aidha, ukaguzi maalumu wa mitambo ya uchenjuaji madini (Vat-leaching na CIP) na SSM kwa madhumuni ya kukusanya taarifa husika na shughuli za uchenjuaji madini zinazojumuisha uratibu na uendeshaji wake; uwezo wa uzalishaji. Ukaguzi huu ulifanyika katika Mkoa wa Geita.

Jumla ya Vat-leaching 90, CIP 3 na SSM 15 zilikaguliwa. Kuhusu utunzaji wa mazingira, serikali imewaelekeza wamiliki wa migodi mikubwa na ya kati kuandaa mpango wa ufungaji migodi utakaokuwa na gharama za kurejesha mazingira katika hali inayoweza kutumika kwa matumizi mengine.

Migodi inahitajika kuweka hati fungani inayoendana na gharama halisi za ufungaji wa mgodi. Hadi Machi mwaka huu, migodi 11 imewasilisha mipango ya ufungaji migodi. Migodi iliyowasilisha ni Dangote Cement Limited, NMGM – North Mara, BGM – Bulyahulu, BZGM – Buzwagi, GGM-Geita, WDL – Mwadui, Twiga Cement Limited, Tanga Cement Limited, TANCOAL, Joshua Kazi – Chunya, na NLGM –New Luika.

Tume ya Madini inaeleza kuwa katika kuhakikisha uwasilishaji wa mipango ya ufungaji migodi inayozingatia uchimbaji wa madini endelevu, serikali imeandaa Rasimu ya Mwongozo wa Ufungaji Migodi.

“Hadi kufikia Machi, 2020 migodi mitatu ya Geita Gold Mine, Williamson Diamonds na New Luika imewasilisha mipango yao ya ufungaji migodi iliyorekebishwa kufuatia maelekezo waliopatiwa na Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji Migodi,” inasema Tume ya Madini.

Katika kuhakikisha sekta ya madini inaendelea kusimamiwa ipasavyo, serikali imeendelea kutoa mafunzo kwa wakaguzi wa migodi kuhusu ufungaji wa migodi. Kwa kushirikiana na Serikali ya Sweden, Serikali imetoa mafunzo kwa watumishi tisa kuhusu ufungaji salama wa migodi.

Vilevile, kwa kushirikiana na Serikali ya Canada, serikali iliendesha mafunzo ya kujenga uwezo wa kupitia na kuthibitisha mipango ya ufungaji migodi kwa wakaguzi wa migodi. Tume ya Madini imesema imeendelea na Ukaguzi wa Mabwawa ya kuhifadhia takasumu zinazotoka katika mitambo ya uchenjuaji madini.

Migodi iliyokaguliwa kwa ajili ya kuomba kibali cha ujenzi/kutumia mabwawa ya kuhifadhia takasumu ni Bulyanhulu Gold Mine Limited, Buzwagi Gold Mine, North Mara, Geita Gold Mine, ZEM Development (T) Co Ltd, Katavi Mining Co. Ltd, Lindi Jumbo Graphite, Busolwa Mining na Nyarugusu Mine.

Aidha, katika kuhakikisha uwepo wa usalama wa wakaguzi na kupata ufanisi unaotarajiwa, serikali imekuwa ikitoa vitendea kazi pamoja na vifaa vya kujilinda kwa wakaguzi wote.

Kwa kutumia taarifa za kaguzi zilizofanyika, serikali imeendelea kuimarisha ukaguzi katika migodi pamoja na kutambua vyanzo vya ajali na kuweka mikakati ya namna ya kuzuia na kukabiliana nazo na kufanya ukaguzi na kutoa elimu ya matumizi bora na salama ya baruti kwa wachimbaji wadogo na wadau wengine wa baruti.

Kwa mujibu wa taarifa, hadi kufikia Machi 2020, elimu juu ya matumizi bora na salama ya baruti imetolewa kwa watumiaji takriban 100 katika maeneo mbalimbali nchini.

“Tume ya Madini kwa kushirikiana na NEMC, LGA na Wizara ya Maji ilifanya mkutano uliolenga kuoanisha mfumo wa usimamizi mpango wa uhifadhi mazingira (EPP) na shughuli za uchimbaji mdogo.

“Tume ya Madini ilishiriki katika kamati maalumu ya watalaamu inayosimamiwa na Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) inayoshughulikia suala la uchafuzi mazingira unaotokana na shughuli za Mgodi wa North Mara,” ilieleza Tume ya Madini.

Aidha, ukaguzi maalumu ulifanywa ili kudhibiti uwezekano wa uchafuzi wa mazingira unaotokana na shughuli za uchimbaji na uchenjuaji madini kando na Bonde la Mto Ruaha Mkuu. Ukaguzi ulifanyika katika maeneo yaliyo kando ya vyanzo vya maji vya bonde hilo katika Mikoa ya Morogoro, Mbeya, Iringa na Dodoma.

Pia ukaguzi maalumu wa maeneo ya uchimbaji pembezoni mwa Ziwa Manyara katika Mikoa wa Manyara na Arusha kaguzi zililenga kuona shughuli za uchimbaji zinavyoathiri vyanzo vya maji katika Ziwa Manyara.

TAMKO la Kimataifa Kuhusu Haki za Binadamu (UDHR 1948), Mkataba ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi