loader
Mil 50/- kutumika mradi wa maji Nyasa

Mil 50/- kutumika mradi wa maji Nyasa

SERIKALI imetoa Sh milioni 50 za mradi wa maji Kitongoji cha Mingohi kijiji cha Chimate Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, Ruvuma.

Akisoma taarifa ya mradi huo kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme juzi hapa alipokagua mradi huo, Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) Wilaya ya Nyasa, Evaristo Ngole alisema utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 90 ambapo zimetumika zaidi ya Sh milioni 43.

Ngole alisema mradi ulianza kutekelezwa Februari mosi mwaka huu na kulikuwa na mikataba mitatu ya utekelezaji wa mradi huo ikiwemo ujenzi wa tangi lenye mita za ujazo 25,000 chanzo cha maji milima ya Livingstone.

“Mradi unatekelezwa kwa fedha za wadau wa maendeleo kutoka Uingereza ambao hutoa fedha kupitia Wizara ya Maji chini ya Mpango wa Lipa kutokana na matokeo’’, alisema Ngole.

Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Isabela Chilumba alisema serikali imetoa zaidi ya Sh milioni 390 za kujenga mradi wa maji katika vitongoji vitatu vilivyobaki vya kijiji cha Chimate ambavyo ni Mtakanini, Chimate kati na Chiwanda.

Baada ya kukagua mradi, Mndeme alisema ameridhika na utekelezaji wa mradi wa maji kitongoji cha Mingohi ambao umewaondolea kero wananchi ya kutumia muda mrefu kwa kutembea umbali mrefu kutafuta maji.

“Mradi wa Sh milioni 50 wanaenda kufaidika wananchi zaidi ya 1,200 kwa kujengewa vituo 12 vya kuchota maji kitongoji cha Mingohi ambacho tangu nchi ipate uhuru hawajawahi kupata maji ya bomba,” alisisitiza Mndeme.

foto
Mwandishi: Muhidin Amri, Nyasa

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi