loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wapinzani wajifunze zaidi CCM kuliko kushindana

Katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020, vyama mbalimbali vimeendelea na maandalizi kuhakikisha vinafanya vema huku kila chama kikijipanga kwa namna yake.

Mwangwi wa maandalizi kwa baadhi ya vyama, hausikiki kabisa ukilinganisha na vyama vingine hasa katika maandalizi ya makada na viongozi wao. Ikumbukwe kuwa, ili kushinda uchaguzi hasa katika siasa za ushindani kama zilivvyo sasa, maandalizi ya ushindi huambatana na mambo mbalimbali kuanzia maandalizi ya ilani za uchaguzi za vyama, nyaraka za kusimamiana katika michakato ya kuwapata wagombea, uendeshaji wa mafunzo kwa makada na viongozi watendaji wasimamizi wa michakato ya uchaguzi.

Katika siku za hivi karibuni, tumeshuhudia na kuona katika vyombo vya habari mbalimbali vyama vikianza kufungua michakato ya uchaguzi ndani ya vyama vyao na sasa fomu za kugombea urais zikianza kutolewa Tanzania Bara na Visiwani.

Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), takriban vyama 19 vinatarajiwa kuingia katika kinyang’anyiro hicho kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge na urais ambapo wananchi wataamua ni chama gani wakipe ridhaa ya kuongoza kutokana na sera, muundo, nidhamu ya chama, itikadi na imani inayojenga misingi ya vyama hivyo.

Katika jicho la uchambuzi, licha ya vyama kuwa na sera nzuri, muundo na itikadi, ushawishi wa chama chochote hutokana na maandalizi ya muda mrefu wa viongozi waandamizi wa chama husika kupitia mafunzo na semina mbalimbali zinazotolewa kwa njia za mitandao na njia ya madarasa kwa muda uliopangwa kuanzia siku moja, mbili, tatu, mwezi hata mwaka mzima kulingana na uzito wa mafunzo hayo.

Katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, kwa upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), maandalizi yake yamekuwa dhahiri ukilinganisha na vyama vingine ambavyo licha ya kazi kubwa iliyofanywa na serikali zake mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais John Magufuli na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, chini ya Rais wake, Dkt Ali Mohammed Shein, mafunzo yanayoendelea katika maeneo mbalimbali yanaipa CCM nafasi ya kuwa mbele zaidi kwa maandalizi ikilinganishwa na vyama vya upinzani.

Mafunzo ndani ya chama tawala hiki (CCM), yamekuwa dhahiri kukipa chama hicho uhakika wa kufanya vizuri kwa umma kwa sababu katika siasa, kuna hoja iitwayo, “win power preparation” inayoangalia maandalizi kuelekea siku ya uchaguzi na hii huchangia asilimia 30 ya ushindi wa chama chochote cha siasa. Sera za chama huchangia asilimia 40, nidhamu na itikadi ya chama huchangia asilimia 20, na hoja za papo kwa papo pamoja na mambo mengine huchangiaasilimia 10.

Katika sayansi ya siasa, hadi sasa vyama vya upinzani vinakwenda katika uchaguzi mkuu huu vikitegemea zaidi hoja za papo kwa papo ambazo kwa mikakati ya ushindi, hoja hizo huwa hazina uhakika kwa sababu hutegemea zaidi hali ya wakati huo na udhaifu wa chama shindani katika uwasilishaji wa sera na siyo maandalizi ya sera, kwa sababu inawezekana sera za chama fulani zikawa nzuri, lakini uwasilishwaji ukapunguza ushawishi na mara nyingi hupunguza asilimia siyo zaidi ya 10.

Wiki iliyopita CCM kupitia kwa Makamu Mwenyekiti (Bara), Philip Mangula alifungua mafunzo ya siku tatu kwa watendaji wa CCM wa mikoa yote nchini jambo lililotafsirika kama ni hatua kubwa kuelekea ushindi wa chama hicho kikongwe Afrika.

Katika ufunguzi huo, Mangula alifafanua majukumu ya makatibu wa mikoa na namna wanavyopaswa kujipanga katika mikoa yao kuhakikisha chama hicho kinapata ushindi mkubwa kulinganisha na ule wa mwaka 2015.

Akifafanua katiba ya chama chake anasema:

“Katiba ya CCM, katika Ibara ya 96, Kifungu cha 3, inawataja makatibu wa mikoa kuwa ndio wakurugenzi wa uchaguzi ndani ya chama hicho”, hivyo semina hiyo ilikuwa na kazi ya kufafanua kwa undani majukumu yao kuhakikisha ushindi wa CCM unapatikana kwa mikoa yote.

Katika semina hiyo ya aina yake kimkakati hasa kwa medani ya kisiasa na sayansi ya siasa, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally anayeonekana kukimudi vema Chama Cha Mapinduzi katika nafasi hiyo, mbali na mafunzo yaliyotolewa na waandamizi wa chama chake, aliitumia semina hiyo kutoa na kufafanua masuala mbalimbali tatanishi kwa sasa likiwemo suala la ukomo wa wabunge, wawakilishi na madiwani wa CCM.

“Hoja ya wabunge, wawakilishi na madiwani kuendelea ama kutoendelea na kazi ni kuwa, wote hao bado wapo kazini, ukitaka mbunge asiwe kazini maana yake waziri mkuu, spika wote wasiwe kazini kwa sababu woteni wabunge; hatuwezi tukaacha ombwe la uongozi, nchi itaendeshwaje? Chama hiki siyo cha uchaguzi ni chama cha uongozi.”

Akasisitiza: “Nasikia mnafukuzana huko kama digidigi na wabunge na madiwani eti kwa sababu ya kanuni, kanuni hazijawafuta kazi, wale ni wajumbe wa vikao vyote vya kazi na ni wawakilishi wetu wanatakiwa kufanya kazi ya chama na kazi ya umma mpaka Julai 14, 2020 wanapochukua fomu.” Dk Bashiru akaongeza:

“Mbunge ama mwakilishi anayehangaika siku mbili ama wiki mbili kabla ya uchaguzi, mnahangaika naye wa nini; kama amedondoka atakusingizia wewe katibu, alinizuia nisikutane na wananchi kumalizia ahadi zangu, kumbe alishajifia miaka minne iliyopita, unahangaika naye wa nini?”

Katika nchi yenye mfumo wa vyama vingi kama Tanzania, udhaifu wa baadhi ya vyama huonekana kwa urahisi pale ambapo chama kimoja ndicho kinakuwa kikihangaika na nidhamu ya viongozi wake kwa uwazi ukilinganisha navyama vingine.

Mathalani, ni nadra sana kumsikia Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika akisisitiza kuhusu nidhamu ndani ya chama chake ukilinganisha na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally ambaye mara nyingi amesikika akisimamia nidhamu ndani ya chama chake kwa nguvu kubwa jambo linaloipa CCM uhalali wa kusimamia nidhamu nje ya chama.

Aidha, hata pale vyama vya upinzani vinapojaribu kujifunza kwa CCM katika suala hilo la nidhamu, wameonekana huchukua hatua bila kufuata utaratibu, na hii imeonekana wazi katika Bunge la 11 ambapo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwataka wabunge wake kutohudhuria bungeni kutokana na kuwepo na ugonjwa wa Covid-19 nchini.

Kutokana na baadhi ya wabunge wa chama hicho kuona hakuna mantiki kutohudhuria vikao vya Bunge, walipinga hadharani kwa sababu maamuzi hayo hayakuwa shirikishi wala yenye tija kwa umma, na hata walipowachukulia hatua ya kuwafukuza uanachama, uongozi wa Chadema haukufuata utaratibu wa Katiba yao wenyewe.

Jambo hili limeacha maswali na masikitiko mengi kwa wachambauzi, wadau wa siasa na wananachi wapenda siasa za vyama vingi kwa kuwa vyama hivi bado havioneshi kukua kiuongozi na hivyo, vinahitaji muda wa kujifunza kwa chama kikongwe; chama tawala (CCM), badala ya kushindana, vijifunze ili vikomae. Katika ujenzi na uimarishaji wa chama kukiwezesha kushinda, kuna nadharia inayofahamika kama

“Politiking of Bottom Index Figuration” inayotumiwa sana na CCM na hata kuifanya kuwa mbele zaidi ya vyama vya upinzani ambapo pia mara nyingi hutumiwa na vyama vya kijamaa kikiwemo CPC cha China, kinachoweka mbele zaidi maarifa ya ushindi darasani kuliko mbinu nyingine yoyote.

Hivyo katika ushauri wa sayansi ya siasa, ni vema vyamavya upinzania vikakitumia Chama Cha Mapinduzi kujifunza zaidi, kuliko kushindan aili kwa miaka ya mbeleni wawe na uwezo wa kushindana tofauti na ilivyo sasa. Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya siasa na maendeleo.

Anapatikana kwa 0742102913.

KATIKA makala mbili zilizopita tumeangalia manufaa ambayo wanavijiji wamepata kutokana ...

foto
Mwandishi: Said Nguya

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi