loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Vitabu vya fasihi vilivyochangia kukuza Kiswahili baada ya Uhuru-2

WIKI iliyopita tulianza makala haya yanayoangalia namna uandishi wa vitabu vya fasihi unavyosaidia kukuza Kiswahili baada ya uhuru. Tuliona kwamba moja ya dhima za fasihi ni kuelimisha jamii, kukuza lugha, utamaduni, kuburudisha, kuonya jamii, kukuza uwezo wa kufikiri na kadhalika.

Pia tuliona kwamba mwandishi ni mtu yeyote anayeweza kuwasilisha mawazo yake kwa maandiko akikusudia kuelimisha na kuburudisha jamii.

Tukaangalia pia baadhi ya vyama vilivyoanzishwa na waandishi wa vitabu vikilenga kuboresha kuboresha kazi hiyo ya uandishi kama vile “Tanzania Writers Association” na badaye Umoja wa Waandishi wa Vitabu nchini ambao ulijulikana kama (UWAVITA).

Tukaona kwamba kwa sasa umoja ambao upo na unafanya kazi za kuandika na kuhamasisha uandishi wa vitabu ni UWARIDI.

Baadhi ya waandishi na wapenzi wa lugha ya Kiswahili wameanzisha umoja huu ili uwasaidie katika kujadili na kushughulikia matatizo ya waandishi mbalimbali wa kazi za fasihi na hadithi za kusisimua.

Umoja huu unaojulikana kwa kirefu (Umoja wa Waandishi wa Riwaya wenye Dira, Tanzania) umekuwa ukiwatumia waandishi wakongwe kama vile Shafi Adamu Shafi na Amri Bawji ili waweze kuhamasisha uandishi wa vitabu. Uamuzi wa kuanzisha umoja huu umeanzishwa baada ya kuona kuwa vyombo vingine vilivyokuwa vinasimamia waandishi vimelegalega katika kutekeleza majukumu yao.

Uandishi wa vitabu ulivyokuza Kiswahili Baada ya nchi ya Tanzania kupata uhuru mwaka 1961 na baada ya kutangazwa Azimio la Arusha mwaka 1967, kuliibuka waandishi wa vitabu ambao waliandika vitabu kwa mtazamo tofauti na ilivyokuwa siku nyuma.

Vitabu vilivyoandikwa wakati huu vilikuwa vinasawiri hali ya nchi kwa wakati huo ambayo ilikuwa ni kufurahia uhuru na kuwa na matumaini mapya ya maisha bora kwa sababu watu walianza kusherehekea Uhuru.

Baadhi ya vitabu hivyo ni pamoja na kile kilichoandikwa na Faraji Hussein Hassan Katambula mwaka 1965, kilichojulikana kama Simu ya Kifo kilichochapishwa na Nairobi: Kenya Literature Bureau maudhui yake yakiwa ni upelelezi.

Hii ilikuwa riwaya maarufu ambayo mhusika aliyetamba sana aliitwa Inspekta Wingo, bila shaka waliokisoma kitabu hicho wanakumbuka. Miaka ya sabini kukaibuka waandishi wengi wa riwaya na tamthiliya zilizoandikwa kuhusu hali ya wakati huo ambayo ilikuwa ni kushadidia matumaini ya maisha mapya ya kufaidi matunda ya uhuru. Waandishi wengi waliandika kuhusiana na maudhui yaliyohusu uchumi wa nchi, kwa mfano kwenye kitabu cha Uchumi wa Utajiri, Athari ya Tamaa Uchoyo na Ulafi, mwandishi wa kitabu hiki alikuwa ni Banzi Alex mwaka 1970. Vitabu vingine vilivyoandikwa wakati huo ni Pamoja na Hadithi zenye Mafunzo, mwandishi akiwa ni Amiri Alli Jamadari, mwaka 1973 kikiwa kina maudhui yanayohusiana na elimu na maadili, Hekaya za Mjini, kilichoandikwa na Backman, P.J mchapishaji akiwa ni Ndanda Mission mwaka 1974 kikiwa na maudhui yanayohusiana na Kiroho na Upendo. Aidha, uandishi wa vitabu vya riwaya vyenye maudhui ya Kimagharibi ambavyo vingi vilikuwa ni vya upelelezi vilivutia pia wasomaji. Baadhi ya waandishi maarufu wa riwaya hizi ambazo baadaye zilipata jina maarufu la riwaya pendwa ni kama vile Aristablus Elvis Musiba ambaye alikuwa mtunzi mashuhuri wa hadithi za kusisimua katika miaka ya 1980.

Musiba alivuma sana kwa tungo zake kama vile Kufa na Kupona, Kikomo, Kikosi cha Kisasi, Njama na Hujuma. Riwaya hizi zilipendwa na watu wa marika yote kwa kuwa zilitungwa zikihusisha matukio ya kusisimua.

Musiba ni mmoja kati ya waandishi wa mwanzo nchini Tanzania kutunga hadithi za kijasusi, kipelelezi na za matukio ya kutisha, hadithi ambazo baadaye zilipigwa marufuku.

Aidha, mwandishi mwingine wa riwaya pendwa ambaye amekuwa akiandika riwaya na kutengeneza filamu ni Amri Bawji ambaye amekuwa akiandika hadithi za kusisimua zikiwamo zile za riwaya yake ya Majaaliwa na Kubali Tuyamalize.

Katika kuhakikisha kuwa tasnia hii ya uandishi inaendelea kufanya vizuri, baadhi ya taasisi zimejitolea kutoa zawadi kwa waandishi bora ambao wameandika vitabu ambavyo vinavutia.

Taasisi inayojulikana kwa jina la Mabati-Cornell, ambayo inadhaminiwa na Kampuni ya Mabati Rolling Mills na Chuo Kikuu cha Cornell cha Marekani hutoa tunzo kila mwaka. Waandishi ambao wameandika vitabu bora katika riwaya na ushairi hushindanishwa na hatimaye mshindi anatunukiwa tuzo.

Malengo ya tuzo hii ni kuthamini uandishi wa lugha ya Kiswahili na ule wa lugha za Kiafrika na vilevile kutafsiri lugha nyingine kwa lugha za Kiafrika. Hata mwaka huu taasisi hiyo ilikuwa inaandaa kutoa tunzo lakini ikasitisha hatua hiyo kutokana na kuibuka kwa janga la corona.

Aidha, taasisi nyingine ambazo zimewahi kutoa tuzo ya Shaaban Robert ni Kampuni ya Maendeleo ya Kiswahili inayojulikana kama KIDE na ile ya Tanzania Growth Trust ambayo imewahi kutoa tuzo ya Ibrahim Hussein. Bilas haka taasisi nyingi zaidi zinapaswa kujitokeza kuzawadia waandishi wa vitabu ili kukuza fasihi nchini.

Changamoto za uandishi wa vitabu Kutokana na utandawazi na mabadiliko ya maisha, hamasa ya uandishi wa vitabu imepungua sana, hii ilichochewa zaidi na kukosekana kwa wasomaji wengi wa vitabu. Watu wengi wamekuwa wakipata taarifa za mambo mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii zaidi kuliko kwenye maandishi.

Mbali na talanta ya uandishi wa vitabu waandishi wengi wa vitabu hasa vya riwaya na tamthiliya walichochewa kuandika kutokana na kipato, hivyo baada ya kupungua kwa wasomaji wa vitabu waandishi wengi wamekata tamaa ya kuandika.

Aidha, ukosefu wa soko ni tatizo jingine linalowakabili waandishi wa vitabu vya Kiswahili.

Iwapo mwandishi atachapisha kazi yake na kazi hiyo ikakosa nafasi ya kuingia katika mfumo wa elimu hasa shule za msingi na sekondari, kuna uwezekano mkubwa akakosa mauzo mengi ambayo yatamchochea kuandika kazi nyingine. Hii ni kwa sababu mfumo wa elimu nchini Tanzania una utaratibu wa kuchagua vitabu vinavyoingia katika mtaala.

Aidha, uandishi ni taaluma inayohitaji muda mwingi ili mtu aweze kuandika kitabu ambacho kitakuwa na maudhui yenye mafunzo ambayo yanawavutia wasomaji.

Waandishi wengi wa vitabu vya Kiswahili ni walimu wanaofundisha katika ngazi mbalimbali katika shule za sekondari na vyuo vya kati na vya juu. Mara nyingi, walimu huwa na kazi nyingi kama vile kufundisha, kusahihisha, kusimamia kazi za wanafunzi na majukumu mengine ya kazi zao. Baadhi ya wahadhiri huwa na kazi za ziada kama kufanya utafiti hivyo inakuwa vigumu kupata muda wa kutosha.

Kwa ujumla kukosekana kwa muda wa kutosha imekuwa ni tatizo kwa waandishi kwa kuwa hakuna mwandishi anayetegemea kazi ya kuandika tu, wengi wa waandishi wana kazi nyingine. Aidha, ukosefu wa vifaa vya kisasa vya uandishi kama vile kompyuta zenye programu maalumu ya uandishi ni tatizo kwa kuwa hadi sasa wapo waandishi ambao huanza kuandika kitabu kwa kutumia kalamu na karatasi.

Vifaa vya kusaidia uandishi ni ghali mno hasa kwa waandishi wachanga ambao wanaanza kuandika. Vilevile, baadhi ya wachapishaji hawakubali kuchapisha miswada ya waandishi wachanga.

Waandishi wengi hasa wa vitabu vya sanaa huandika maudhui ambayo hayakubaliki matokeo hivyo vitabu vyao vinapigwa marufuku.

Tatizo jingine ni kwa wale wanaotaka kuandika kila utanzu wa fasihi yaani thamthilia, riwaya, ushairi, hadithi fupi, vitabu vya watoto na vinginevyo jambo ambao haliwezekani kwa waandishi chipukizi.

Mwisho, pamoja na kwamba kwa sasa kuna vyanzo vingi vya kupata taarifa lakini maandishi ni chanzo ambacho kinadumu kuliko vyanzo vingine vya taarifa. Vitabu vinaweza vikadumu kwa miongo kadhaa bila kuharibika kama vitatunzwa.

Mwandishi ni Mchunguzi Lugha Mwandamizi katika Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita).

Anapatikana kwa 0712747199/0757900894.

KATIKA makala mbili zilizopita tumeangalia manufaa ambayo wanavijiji wamepata kutokana ...

foto
Mwandishi: Mussa R. Kaoneka

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi