loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Watendaji simamieni, itunzeni New Mv Victoria

UKARABATI wa meli ya New Mv Victoria umekamilika na leo inaanza safari ya majaribio, ambapo itatia nanga katika Bandari ya Kemondo iliyopo Bukoba mkoani Kagera ikitokea Mwanza.

Tunaipongeza serikali kwa kufanikisha ukarabati wa meli hiyo kubwa, ambayo itapunguza changamoto kubwa ya usafiri, iliyopo katika Ziwa Victoria kwa takribani miaka 24 sasa, tangu ilipozama meli ya Mv Bukoba mwaka 1996.

Ni wazi kuwa meli hii inaanzisha mapinduzi makubwa ya usafiri na usafirishaji wa mizigo na abiria katika Ziwa Victoria.

Mapinduzi haya yamewezeshwa na utekelezaji wa ahadi ya Rais John Magufuli ya kurejesha usafiri salama ndani ya Ziwa Victoria, aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Habari kutoka Mwanza zinasema New Mv Victoria itaingia Bandari ya Kemondo ikiwa na tani 100 ya mizigo, iliyosafirishwa bure kutokana na agizo la Rais Magufuli, la kutaka wakati wa majaribio ya kwenda Bukoba na kurudi Mwanza, mizigo ya wananchi isafirishwe bure.

Kwa ujumla, meli hii italeta faida nyingi za kiuchumi na kijamii.

Kwa mfano, mama lishe wataweza kuuza chakula kwa abiria na wabeba mizigo wa meli, hivyo kupata kipato kizuri. Kwa miaka yote hii wakati usafiri wa meli ukiwa umesimama, mama lishe walikuwa na wateja kiduchu.

Aidha, meli hiyo itatoa ajira kwa vijana wengi na inaelezwa kwa kuanzia vijana 200 watafanya kazi kama vibarua na makarani katika meli.

Usafiri wa meli hiyo utapunguza gharama za usafirishaji wa mizigo ukilinganisha na usafiri wa malori.

Kwa mfano, gharama ya kusafirisha tani mmoja ya ndizi kwa meli ni chini ya Sh 24,000 lakini kusafirisha tani hiyo moja kwa lori ni kati ya Sh 80,000 - 100,000.

Tunaomba watendaji wa serikali, kuhakikisha meli hiyo ya New Mv Victoria, inafanya kazi kwa weledi na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.

Tunataka wahakikishe kuwa haipakii abiria na mizigo kupita uwezo wake, kama ilivyofanyika kwa Mv Bukoba, iliyozama mwaka 1996 ikiwa na umri wa miaka 17 tu tangu inunuliwe na serikali.

Meli hiyo ilipozama ilisababisha vifo vya watu wengi na upotevu wa mali nyingi. Ikumbukwe kuwa meli ya Mv Bukoba, ingeweza kutumika kwa muda mrefu zaidi na kuliingizia taifa faida kubwa, kama baadhi ya watendaji wasingefanya uzembe na kutanguliza mbele maslahi yao binafsi badala ya maslahi ya taifa. Uzembe wao ulisababisha meli hiyo kuzidisha mizigo na abiria kupita uwezo na kisha ikapinduka.

Ni wazi kuwa binadamu hufanya makosa. Lakini, watendaji wa serikali hawapaswi kurudia makosa kama yale yaliyofanyika kwa meli Mv Bukoba.

Tunawahimiza wawe macho usiku na mchana na meli hii ya New Mv Victoria, meli zingine zilizopo na zijazo pamoja na vivuko. Tunawaomba waisimamie vizuri na kuitunza meli hiyo.

Tukumbuke kuwa serikali inatumia fedha nyingi, kuwekeza kwenye miundombinu ya usafirishaji mfano meli na vivuko ; na inafanya hivyo ili wananchi wapate usafiri mzuri na kufanya biashara; na serikali yenyewe kupata mapato yanayotumika kuboresha huduma zingine kama afya, elimu, maji na umeme.

KUANZIA leo hadi Jumapili wiki hii jijini Dodoma, Chama Cha ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi