loader
JPM ampongeza Majaliwa kwa uhodari

JPM ampongeza Majaliwa kwa uhodari

RAIS John Magufuli amemuagiza mkandarasi wa Kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation kutoka China, aliyesaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya kutoka Ruangwa hadi Nanganga, yenye urefu wa kilomita 53.2 kwa gharama ya Sh 59,286,553,159, aanze kazi mara moja.

Pamoja na agizo hilo, Rais Magufuli amempongeza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye pia ni mbunge wa Ruangwa, kwa uhodari wake katika kazi. Rais alisema hayo alipozungumza na wananchi wa wilaya ya Ruangwa kwa njia ya simu, alipompigia Waziri Mkuu wakati wa tukio la utiaji saini mkataba huo.

“Nashukuru ahadi niliyoitoa, leo (jana) imeanza kuzaa matunda na ilimradi mkandarasi amekubali kusaini, aanze mara moja kupeleka mitambo kwenye eneo la mradi na nitakuja kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi huo,” alisema Rais Magufuli.

Aidha, Rais alimpongeza Waziri Mkuu kwa uhodari wake katika kufanya kazi.

“Endeleeni kumuamini Mheshimiwa Majaliwa, amekuwa akinisaidia. Aendelee kuchapa kazi kwa ajili ya Ruangwa na Tanzania,” alisema Rais Magufuli.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu amemshukuru Rais Magufuli kwa kuthamini na kujali maendeleo ya Watanzania, wakiwemo na wananchi wa wilaya ya Ruangwa, kwa sababu ujenzi wa barabara ya Ruangwa hadi Nanganga kwa kiwango cha lami, ni utekelezaji wa ahadi yake.

“Leo hii ni siku ya kihistoria kwa sababu kile ambacho tulikuwa tunatamani, kikaahidiwa hapa na kiongozi wa nchi Rais wetu Dk John Pombe Magufuli alipofanya ziara Ruangwa, aliweza kuvunja kiu yetu Wana- Ruangwa toka alivyokuwa anaingia Nanganga, wananchi walimuomba asimame na yeye alisimama akijua kuwa hawa wana hamu ya maendeleo.”

Waziri Mkuu aliongeza kuwa baada ya Rais Magufuli, kusimama aliwaambia kuwa “Najua hamu yenu ni ya maendeleo, lakini mimi ninaanza kuwaondolea kiu ya muda mrefu ya barabara yenu kutoka hapa Nanganga mpaka Ruangwa kwa kuijenga kwa kiwango cha lami. Sifa moja ya Rais Magufuli ni kusema na kutenda na ametekeleza.”

Vilevile, Waziri Mkuu aliwataka Watanzania wote waendelee kushirikiana bila ya kujali itikadi zao za kisiasa, kwa sababu maendeleo hayana chama na miradi ya maendeleo, anayoitekeleza katika maeneo mbalimbali nchini imekuwa ikiwanufaisha wananchi wote.

Akizungumzia kuhusu Kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation kutoka China, iliyosaini mkataba huo wa ujenzi wa barabara ya kutoka Ruangwa hadi Nanganaga kwa kiwango cha lami, Waziri Mkuu alisema ni miongoni mwa kampuni kubwa zinazojenga kwa viwango vya kimataifa.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Ujenzi, Elias Kwandikwa alisema barabara hiyo itakuwa na madaraja makubwa matatu na makaravati 31. Kwamba itajengwa kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya ubora vinavyohitajika.

Mapema, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Patrick Mfugale alisema barabara ya Nachingwea - Ruangwa - Nanganga ni muhimu kwa uchumi wa mkoa wa Lindi, kwani inaunganisha mkoa wa Lindi na mikoa jirani kwa barabara kuu ya Mtwara – Dar es Salaam na Mtwara – Masasi – Songea.

“Ili kurahisisha utekelezaji mradi huu umegawanywa katika sehemu mbili:Sehemu ya Nachingwea hadi Ruangwa yenye urefu wa kilometa 52.8 na sehemu ya pili ni kutoka Ruangwa hadi Nanganga yenye urefu wa kilometa 53.2. Serikali imeamua kuanza ujenzi wa sehemu ya Ruangwa hadi Nanganga yenye urefu wa kilometa 53. 2 na upana wa meta 10.0, kwa kutumia fedha za ndani na itajengwa kwa muda wa miezi 27” alisema.

Mfugale aliongeza kuwa ujenzi wa barabara hiyo utakapokamilika, utasaidia kukuza kilimo na utalii katika wilaya ya Ruangwa na mkoa wa Lindi kwa ujumla.

Aidha, mradi utakapokamilika utachochea ukuaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii kwa wananchi waishio maeneo ya Ruangwa, Nanganga na Nachingwea.

Wakizungumzia ujenzi wa barabara hiyo, wananchi wa wilaya ya Ruangwa walimshukuru Rais Magufuli pamoja na Waziri Mkuu ambaye pia ni mbunge wa Ruangwa kwa uamuzi wao wa kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami, kwani itasaidia katika ukuaji wa uchumi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/2b707bce34405c113aab4b275d994e5b.jpg

RAIS Samia Suluhu Hassan amehutubia taifa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Ruangwa

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi