loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JPM amuagiza Lukuvi amalize migogoro ardhi

RAIS John Magufuli amemtaka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ahakikishe anamaliza migogoro ya ardhi wilayani Kilosa mkoani Morogoro.

Ametoa maagizo hayo wilayani Kilosa jana wakati akiweka jiwe la msingi wa ujenzi wa handaki katika reli ya kisasa na jiwe la msingi wa barabara ya Rudewa-Kilosa yenye urefu kilometa 24.

Magufuli alisema katika Mkoa wa Morogoro, kuna migogoro ya ardhi na mashamba kati ya wananchi na wawekezaji na kati ya wakulima na wafugaji.

Alisema ameshayafuta mashamba 49 mkoani humo na bado anamsubiri Waziri Lukuvi ampelekee taarifa ya mashamba mengine 11 ifikapo Jumamosi ili nayo ayafute na kupewa wananchi.

“Siwezi kuongoza nchi yenye watu milioni 60 ambao hawana ardhi, siwezi kuongoza nchi ya watu wenye machozi, walilia wakati nafanya kampeni, na leo niko Rais waendelee tena kulia?”alihoji Magufuli.

Kutokana na unyeti wa suala hilo, aliwataka Waziri Lukuvi, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loatha Sanare na Mwenyekiti wa Kijiji cha Kimamba kuwa kwenye kamati ya Lukuvi ya kupata ufumbuzi wa migogoro hiyo.

Rais Magufuli aliagiza ardhi hiyo yote wapewe wananchi bure ili waendeshe shughuli za uzalishaji wa kilimo na ufugaji. Magufuli pia alimuonya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo na Mkuu wa Wilaya kwa kujihusisha na migogoro ya ardhi.

Alimtaka ajirekebishe kwa sababu anazo taarifa zake kuwa alifanya kikao cha siku moja na mwekezaji na kusaini mkataba na aliingiza benki Sh milioni 225 wakati alilipwa Sh milioni 400.

Pia alimuonya Mkuu wa Wilaya ya Kilosa na kumtaka ajirekebishe kwa kitendo chake cha kwenda na Polisi eneo la Kimamba kuwatisha wananchi kwa lengo la kumsaidia mwekezazaji badala ya kuwasaidia wananchi.

Awali, Waziri Lukuvi alimweleza Rais kuwa Wilaya ya Kilosa ndiyo inayoongoza kwa migogoro ya ardhi mkoani Morogoro.

Alisema mashamba 49 yameshafutwa na mashamba mengine makubwa 11 atayatolea taarifa kwa Rais ndani ya siku saba kuanzia jana ili nayo yaweze kufutwa.

Lukuvi alisema wananchi wa vijiji vyote kwenye mashamba hayo 49 hawataondolewa.

Aidha, Rais Magufuli alitembea kwa miguu kwenye handaki hilo lenye urefu kilometa 1.1 kabla ya kuwahutubia wananchi.

TRAFIKI Kanda Maalum Dar es Salaam imese- ma ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera, Morogoro

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi