loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Magufuli: Tumeandika historia

RAIS John Magufuli amesema Tanzania imeandika historia ya pekee kwa kujenga reli ya kisasa yenye mahandaki makubwa na ya kisasa ambayo yatavutia watalii wa ndani na nje.

Alisema hayo wilayani Kilosa mkoani Morogoro jana wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa handaki lenye urefu wa kilometa 1.1 na mahandaki mengine matatu ambayo kwa jumla yana urefu wa kilometa 2.7.

Mahandaki hayo ni sehemu ya ujenzi wa Reli ya Kisasa ya Umeme (SGR), awamu ya pili kutoka Morogoro hadi Makutupora mkoani Dodoma yenye urefu wa kilometa 422.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa alisema ujenzi wa reli ya hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro yenye urefu wa kilometa 300 umefikia asilimia 82, na Morogoro-Makutupora kilometa 422, umefikia asilimia 34.

Kadogosa alisema ujenzi wa stesheni katika kipande cha Dar es Salaam-Morogoro umefikia asilimia 90, na ujenzi wa stesheni kipande cha Morogoro-Makutupora umefikia asilimia 15.8.

Ameyataja mambo mengine kuwa ujenzi wa daraja la juu la SGR Dar es Salaam lenye urefu wa kilometa 2.56 umefikia asilimia 86, ujenzi wa madaraja 187 umefikia asilimia 80 katika kipande cha kwanza, na asilimia 32 kipande cha pili.

Kutokana na mafanikio ya ujenzi wa reli hiyo yakiwemo mahandaki, RaisMagufuli alisema kwa mara ya kwanza alishuhudia handaki kama hilo nchini Uingereza mwaka 1992 alipokwenda kimasomo.

Alisema amefurahishwa kuona Watanzania nao wameweza kujenga mahandaki hayo kwa fedha zao wenyewe na kuifanya Tanzania kuandika historia ya kipekee kwani mradi huo utavutia utalii.

“Watu watatoka nchi mbalimbali na ndani ya Tanzania kuja kuangalia handaki hili ambalo litaunganishwa na daraja la juu lenye urefu wa mita 500, leo nimekuwa shahidi kwa kujionea jambo hili kwa macho yangu, Kilosa tumefungua fursa ya utalii, tumieni nafasi hii kuleta maendeleo mengine,” alisema Magufuli.

Alisema wakati anatoa ahadi ya kujenga reli hiyo mwaka 2015, hakuwa na hakika kama watu wengi walimwamini wakiwemo mawaziri na watendaji wengine.

Rais Magufuli alisema aliwahi kufika Kilosa wakati akiwa Waziri wa Ujenzi na kushuhudia mchezo mchafu kati ya mkandarasi na baadhi ya watendaji wa wizara hiyo wa kujilipa kati ya Sh bilioni 5 hadi 7 kila mwaka kwa ajili ya kukarabati reli ya zamani iliyokuwa inaharibiwa na Mto Mkondoa.

Hivyo, mwaka 2015 wakati anaahidi ujenzi wa reli ya kisasa, alionekana kama anaota ndoto za mchana, lakini kwa kuwa alimwamini Mungu, jambo hilo limefanikiwa.

“Watanzania wengi leo tuna raha, ukiwa na raha unapata nguvu, hivyo nawapongeza Watanzania wote kwa juhudi kubwa zilizofanikisha mradi huu unaogharimu zaidi ya Sh trilioni 6.05,” alieleza Magufuli.

Sambamba na hilo, Rais Magufuli pia jana aliweka jiwe la msingi wa ujenzi wa Barabara ya Rudewa- Kilosa yenye urefu wa kilometa 24.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Patrick Mfugale, alimweleza Rais Magufuli kuwa mradi huo unajengwa na kampuni ya wazawa ya Umoja Kilosa JV kwa gharama ya Sh bilioni 32 na ujenzi huo ulianza mwezi Februari mwaka jana na utakamilika Januari mwakani.

Mfugale alisema mpaka sasa, mkandarasi ameshalipwa Sh bilioni 6.19 na mkandarasi mshauri ameshalipwa Sh milioni 646. Hata hivyo, baada ya maelezo hayo ya Mfugale, ndipo Rais Magufuli alisema amechukizwa na kasi ndogo ya wakandarasi hao.

Alisema hajafurahishwa na kazi ya wakandarasi hao na endapo kama angekuwa Waziri wa Ujenzi, angewafukuza kazi jana. Kutokana na uzembe wa wakandarasi hao, aliwataka wabadilike na kuwapa mwezi mmoja wahakikishe wanafanya kazi usiku na mchana.

Rais Magufuli aliwaambia kuwa kuna siku atapita tena kuangalia mradi huo na kama hawatabadilika atawafukuza kazi pamoja na Waziri na Mtendaji Mkuu wa Tanroads waliowapa kazi hiyo.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alisema mahandaki manne aliyoyazindua jana yana jumla ya urefu wa kilometa 2.7, hivyo hakutakuwa na tatizo la Mto Mkondoa kuharibu reli hiyo kama ilivyo kwa reli ya zamani.

Viongozi mbalimbali walishiriki uzinduzi huo akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge, Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Maduka Kessy, Wabunge wote wa Mkoa wa Morogoro, viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali.

TRAFIKI Kanda Maalum Dar es Salaam imese- ma ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera, Morogoro

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi