loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kampeni ya Ziro Malaria yaanza Dodoma

KAMPENI ya Ziro Malaria inayoenda na ugawaji wa vyandarua kwenye kaya bila malipo kwa mkoa wa Dodoma inaanza Julai, mwaka huu kwa kutoa mafunzo kwa wagawaji vijijini au mitaani.

Akizungumza wakati wa mafunzo kwa wadau wa afya mkoa wa Dodoma mwishoni mwa wiki, Mkuu wa Kitengo cha Uhamasishaji jamii katika Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria, Leah Ndekuka alisema kampeni hiyo inaanza Julai 6, mwaka huu.

Kampeni hiyo itaanza na utoaji wa mafunzo kwa watendaji kuanzia ngazi ya halmashauri hadi ngazi ya mitaa au vijijini ambavyo vyandarua vitagawiwa.

Ndekuka alisema kampeni ya utoaji mafunzo Dodoma itaanzia katika halmashauri za Chemba, Kondoa Mji na Kondoa Vijijini ambapo mafunzo hayo yatafanyika Kondoa Mjini kati ya Julai 6-7, mwaka huu.

“Mafunzo hayo pia yatafanyika Mjini Mpwapwa kati ya Julai 9-10 kwa kushirikisha watendaji katika Halmashauri ya Mpwapwa na Kongwa,” alisema.

Ndekuka alisema mafunzo hayo pia yatafanyika jijini Dodoma kati ya Julai 13-14 mwaka huu, ambayo yatashirikisha watendaji kutoka katika halmashauri ya Jiji, Chamwino na Bahi. Mratibu wa Malaria Mkoa wa Dodoma, Dk Francis Bujiku alisema hali ya maambukizi ya malaria mkoa wa Dodoma ni asilimia 0.6 kiwango ambacho ni wastani wa kitaifa wa asilimia 7.3.

“Katika mkoa huo, wilaya inayoongoza kwa wingi wa malaria ni Mpwapwa yenye asilimia 1.3, ikifuatiwa na Chamwino 0.7, Chemba 0.6, Kongwa 0.6, Kondoa Vijijini 0.4, Bahi 0.4, Jiji 0.3 na Kondoa Mjini ni 0.1,” alisema Bujiku.

Akielezea mafunzo yatakayotolewa kutokana na aina ya kundi, Ndekuka alisema, mafunzo kwa watendaji wa vijiji akiwemo mwenyekiti wa mtaa na vijiji yatalenga namna ya kushiriki kuchagua wanajamii wa kujitolea watakaohusika katika usajili na ugawaji wa vyandarua.

Pia yatalenga namna watakavyoshiriki katika ugawaji wa vyandarua katika kijiji/ mtaa wake na kutoa taarifa kwa wanakijiji /mtaa na vitongoji juu ugawaji vyandarua ili wajitokeze kupatiwa vyandarua.

“Viongozi hao pia watajifunza kuhakikisha ulinzi wa vyandarua vilivyopo katika eneo lake na usalama wakati wa ugawaji wa vyandarua,” alisema.

Pia mafunzo hayo kwa watendaji wa vijiji wa kujitolea yatalenga kuhakikisha vituo vya ugawaji vimepangwa vizuri ili kurahisisha utendaji.

“Watendaji hao watajifunza kutoa orodha ya idadi ya vyandarua vilivyogawiwa na vilivyobaki ofisini kwa ofisa mtendaji kijiji/mtaa kila siku,” alisema.

Katika mafunzo hayo, watendaji wa vijiji au mitaa watajifunza kuchagua wanajamii wa kujitolea kwa ajili ya uandikishaji na ugawaji wa vyandarua wenye sifa ya kutumia simu janja. Pia watajitunza kutuma taarifa za uandikishaji za kijiji/ mtaa kwenye mfumo wa kielektroniki.

Pia watahakikisha Tabiti (Tablet) imechajiwa kila siku baada ya kazi kwa ajili ya kazi ya siku inayofuata.

“Mafunzo kwa watendaji wa afya katika kusimamia usajili na ugawaji wa vyandarua katika vijiji ndani ya kata yake na kuhakikisha ushiriki wa viongozi wa kisiasa na kidini,” alisema. Pia watajifunza kusambaza taarifa za kampeni kabla, wakati na baada ya kampeni kwenye kata na kuhakikisha uwepo wa vifaa vya utekelezaji wa kampeni.

TRAFIKI Kanda Maalum Dar es Salaam imese- ma ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi