loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Gesi asilia itakavyotoa ajira Lindi

LINDI, licha ya ukongwe wake, ni miongoni mwa mikoa ambayo imekuwa haina vitega uchumi vingi kulinganisha na mikoa mingine nchini lakini sasa mambo mazuri yanakuja mkoani humo.

Wakazi wa mkoa huo wametakiwa kukaa mkao wa kula kwa kuwa neema ya ajira inakuja kutokana na ujio wa miradi ya ama kuchakata gesi asilia, utafutaji wa mafuta na gesi au usambazaji wa rasilimali hiyo ambayo imegunduliwa kwa wingi katika mikoa ya kusini ya Lindi na Mtwara.

Mbali na ajira za moja kwa moja, wakazi wa Lindi wameambiwa kwamba watanufaika pia na miradi hiyo kwa kusambaza mahitaji kwa makampuni yanayoshughulika na miradi hiyo kama vile mboga, matunda, kuku, nyama, maziwa na kadhalika. Lingine ambalo limetajwa kwamba wana-Lindi wanatarajia kunufaika nalo ni kuandaa huduma za hoteli za kitalii na nyumba za wageni.

Mradi wa karibuni kabisa kuanza ‘kuwatoa’ wana- Lindi umetajwa kwamba ni wa kuchakata gasi asilia unaoshirikisha makampuni makubwa mawili ya Shell Tanzania Ltd na Equinor Tanzania Ltd kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC).

Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dk Jeams Mataragio amesema mradi huo utaanza karibuni kufuatia wakazi waliokuwa wakiishi au kuwa na vitega uchumi kwenye eno la mradi kuanza kulipwa fidia inayofikia Sh bilioni 5.2 ili kupisha mradi huo. Wanaonufaika na malipo hayo ni wakazi wa maeneo ya Likon’go, Mtomkavu na Masasi ya Leo katika Halmashauri Manispaa ya Lindi.

Anasema kutokana na fedha hizo zilizotolewa na serikali kutolipwa kwa wakati tangu kufanywa kwa tathmini, jumla ya Sh milioni 800 imeongezwa kwa watanzania hao wanaopisha mradi kwa mujibu wa gharama za sasa.

Mkurugenzi huyo anawahakikishia Watanzania kwamba kutokana na hatua hiyo, sasa mradi uko katika hatua za mwisho kuanza na hivyo kuwataka Watanzania kuufahamu na kuupokea mradi huo sambamba na kuchangamkia fursa zinazoletwa na mradi.

Kwa mujibu wa Dk Mataragio, wananchi wa Lindi kama ilivyo kwa Watanzania wengine wakiwemo wakazi wa Dar es Salaam, mradi huo unaleta fursa nyingine ya ajira kutokana na kuwapo kwa mradi wa kusambaza gesi asilia majumbani na kwenye vituo vya mafuta kwa ajili ya magari.

Kuhusu watakaonufaika na gesi asilia majumbani mwao katika hatua za mwanzo, Mataragio anasema ni pamoja wakazi wa kata za Mingoyo, Mnazi Mmoja katika Halmashauri manispaa ya Lindi na Kiwalala katika Halmashauri ya Mtama.

Anasema katika awamu ya kwanza takribani nyumba 200 zitawekewa miundombinu ya gesi asilia kwa ajili ya kupikia majumbani na hatua ya pili itahusisha nyumba 300. Anasema gesi hiyo pia inawalenga wateja wenye matumizi makubwa ya kupika kama mahospitali, mashule, vyuo, magereza na kadhalika na kwamba gesi hiyo asilia inatokana na bomba kuu la gesi kutoka mkoani Mtwara.

Dk Mataragio anafafanua kwamba gesi nyingi imegundulika katika kina kirefu cha maji na kwamba gesi hiyo ndio itakayochakatwa katika mitaa ya Likong’o, Mto Mkavu na Masasi ya Leo, katika manispaa ya Lindi.

Anasema mbali na sehemu ya gesi hiyo kutatumika nchini, sehemu nyingine inatarajiwa kusambazwa kwa ajili ya kuuzwa nje ya nchi katika soko la kimataifa.

Kuhusu matumizi ya gesi asilia kwenye magari, Mataragio anasema tayari TPDC kwa kushirikiana na wabia wake walishaanza kutoa huduma hiyo katika magari kadhaa, hususani katika jiji la Dar es Salaam kwa kuyawekea mifumo ya kutumia gesi asilia badala ya petroli.

Akizungumza kwenye mkutano wa kuzindua mradi wa kusambaza gesi asili majumbani katika mji wa Lindi, Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani anaitaka TPDC kuhakikisha awamu ya kwanza ya mradi huo inayohusisha uwekaji wa miundombinu kwenye nyumba 200 iwe imekamilika ndani ya miezi sita.

Anasisitiza uwekaji huo usifanyike kwa kunyanyapaa baadhi ya nyumba alimradi wahusika wawe wanahitaji huduma hiyo. “Serikali inataka kuona watanzania wote wanatumia fursa za gesi asilia na kunufaika nazo,” anasisitiza.

Anasema matumizi yagesi asilia ni nafuu sana kwani kwa siku ni Sh 1,000 wakati gharama za mkaa kwa familia ya wastani kwa siku ni Sh 5,000.

Kwa upande wake, mbunge wa Jimbo la Mtama wilayani Lindi aliyemaliza muda wake, Nape Nnauye, anawataka vijana wakamate fursa hizo za ajira kwani nyingi zinawezekana kufanywa na wana-Lindi huku zile za kitaalamu zikifanywa na watu kutoka nje. Nape anaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuliwezesha jimbo la Mtama kung’aa tofauti na miaka ya nyuma ambapo lilikuwa ni giza.

Akizungumza katika mkutano huo wa uzinduzi wa mradi wa kusambaza gesi asilia katika mitaa ya Miongoyo, Mnazi Mmoja na Kiwalala, Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Mohammed Luhumbo anasema ilikuwa kama ndoto kuamini kwamba kuna siku kutakuwa na mradi muhimu kama huo katika manispaa hiyo.

Anasema ni hatua muhimu sana kuona mwananchi sasa atakuwa anafungua nyumbani kwake gesi asilia kama anavyofungua maji ya bomba mara mradi utakapokamilika na kupika vyakula vyake.

Naye mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Wilaya ya Lindi, Abdallah Madebe anasema miradi hiyo ya kuchakata gesi asilia na usambazaji wa gesi hiyo majumbani ni mkombozi wa aina yake kwa wananchi wa Lindi, mintarafu sula zima la ajira.

Anawataka vijana wa Lindi kuchangamkia fursa zinazoletwa na miradi hiyo, kwa kuchapa kazi kwa uaminifu mkubwa ili kuwavutia wawekezai zaidi.

Anasema anaamini kupitia miradi hiyo, uchumi wa wilaya ya Lindi na wa mtu mmoja mmoja utapanda kwa asilimia kubwa.

KATIKA makala mbili zilizopita tumeangalia manufaa ambayo wanavijiji wamepata kutokana ...

foto
Mwandishi: Kennedy Kisula

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi