loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Miaka mitano ya JPM na mafanikio lukuki katika Muungano

WAKATI Serikali ya Awamu ya Tano ikielekea kutimiza miaka mitano Novemba mwaka huu, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao umetimiza miaka 56 umeendelea kuwa imara.

Chini ya uongozi thabiti wa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ofisi yake imekuwa ikitekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wananchi wanatambua umuhimu wa Muungano na kuulinda.

Tumeshuhudia kuimarika kwa miundombinu ya barabara, usafiri wa anga, usafiri wa majini na huduma za jamii ikiwemo elimu na afya sambamba na kuendelea kutumia maliasili zetu vizuri zaidi kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili za Muungano.

Utatuzi changamoto za Muungano Taarifa kutoka ofisi ya Makamu wa Rais kwa gazeti hili inaonesha kwamba utaratibu wa vikao vya Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ya kushughulikia masuala ya Muungano uliopitishwa na kamati hiyo Februari 9 mwaka jana na kusambazwa kwa wizara zote za SMT na SMZ kwa ajili ya utekelezaji umeleta manufaa makubwa.

Utaratibu huo pia umeainisha uwepo wa kamati mbili; Kamati ya Fedha, Uchumi na Biashara na Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala zilizopewa jukumu la kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazohitaji utatuzi wa haraka, inasomeka taarifa. Hivyo utaratibu huu ni chachu katika kuimarisha na kuongeza ufanisi wa vikao vya kamati ya pamoja ikiwa ni pamoja na kufuatilia maagizo na maelekezo yanayotolewa na kamati hiyo.

Mifumo imara iliyowekwa ya kujadili na kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali za Muungano wetu, imewezesha pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano kupiga hatua kubwa kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni na hivyo kupata sifa kubwa kimataifa.

Changamoto zilizopatiwa ufumbuzi Kwa mujibu wa taarufa hiyo, katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2020 vimefanyika vikao viwili vya Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ vilivyotanguliwa na vikao vya mawaziri, makatibu wakuu na wataalamu wa kisekta kutoka serikali zote mbili. Katika vikao hivyo jumla ya changamoto 18 zilijadiliwa na kushuhudia 11 zilipatiwa ufumbuzi.

Changamoto zilizopatiwa ufumbuzi ni pamoja na kutungwa kwa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015 ya SMT ambayo ilifuta sheria ya zamani ya utafutaji na uzalishaji wa mafuta, Sura ya 328 na Sheria ya Mafuta na Gesi Asilia ya mwaka 2016 ya Zanzibar na kuondoa VAT kwenye umeme unaouzwa na TANESCO kwa ZECO sambamba na kufuta malimbikizo ya deni la kodi ya VAT lililokuwa limefikia shilingi bilioni 22.9 kwa ZECO.

Lingine, taarifa inasema, lilikuwa ni kupitishwa kwa mwongozo wa ushirikishwaji wa SMZ kwenye masuala ya kimataifa na kikanda ambao umezingatia maeneo ya ziara za viongozi wa kitaifa; mikutano ya kimataifa; nafasi za masomo ya elimu ya juu nje ya nchi na utafutaji wa fedha za misaada au mikopo ya kutekeleza miradi mbalimbali kutoka nje ya nchi.

Taarifa inaonesha kwamba changamoto nyingine iliyopatiwa ufumbuzi ni kuondoa kodi katika unga wa maziwa kutoka Zanzibar kuja Tanzania Bara. Ufumbuzi mwingine ulipatikana katika kuondoa changamoto za kibiashara baina ya Tanzania Bara na Zanzibar ni pamoja na kubainisha gharama za kushusha mizigo (landing fees); ruhusa ya sukari inayozalishwa katika kiwanda cha Mahonda Zanzibar kuingia katika soko la Tanzania Bara na kutungwa kwa sheria mpya ya Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA) ya mwaka 2020.

Vikao vya pamoja pia viliwezesha pia kusainiwa kwa mkataba wa mradi wa ukarabati wa Hospitali ya Mnazi Mmoja mwezi Aprili, 2020; kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wa barabara ya Chake Chake hadi Wete – Pemba mwezi Aprili, 2020 na kuanza kufanya kazi kwa Mfumo wa e- RCS mwezi Januari, 2020 hivyo kuondoa tatizo la usimamizi wa ukokotoaji na ukusanyaji wa kodi kwenye huduma za simu pande mbili za Muungano.

Mafanikio yaliyopatikana katika utatuzi wa changamoto ni matokeo ya jitihada zilizochukuliwa na serikali zetu mbili tangu kuundwa kwa Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ mwaka 2006. Taarifa inaonesha kwamba changamoto zilizobakia ambazo ni pamoja na masuala ya fedha, uchukuzi, biashara na usajili wa vyombo vya moto, zipo katika hatua mbalimbali za kupatiwa ufumbuzi.

Ongezeko miradi ya maendeleo Katika kipindi hiki cha miaka mitano, kwa mujibu wa taarifa, serikali hizi mbili zimeendelea kushirikiana katika kuibua miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo hufadhiliwa na SMT kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

Taarifa inasema miradi hii imewasaidia wananchi wa pande zote mbili za Muungano kushiriki na kuinua hali zao za kiuchumi pamoja na kuongeza ajira. Miradi na programu hizo ni pamoja na zifuatazo.

Mosi, ni Mfuko wa Maendeleo ya Jamii awamu ya tatu (TASAF III) iliyozinduliwa Agosti, 2012 na kuanza utekelezaji wake mwaka 2013 katika halmashauri 159 za Tanzania Bara na wilaya zote za Zanzibar.

Mpango huu umejikita katika maeneo manne ambayo ni pamoja na kunusuru na kutoa kinga kwa kaya maskini kwa njia ya kuhawilisha; kuboresha maisha na kuongeza kipato kwa kaya maskini kupitia uwekaji wa akiba na shughuli za kiuchumi; na kujenga na kukarabati miundombinu katika sekta za elimu, afya na maji kwenye maeneo yaliyolengwa.

TASAF III imekuwa na mafanikio kwa wananchi wa pande zote mbili za Muungano kwa kuwa ruzuku zinazotolewa kwa walengwa zimewasaidia kupata mahitaji ya msingi yakiwemo ya chakula, mahitaji ya shule kwa watoto na miradi midogomidogo ya kujiongezea kipato. Pili, ni programu ya miundombinu ya msoko na uongezaji thamani na huduma za fedha vijijini (MIVARAF).

Programu hii ya miaka saba utekelezaji wake ulianza mwaka 2011. Ni mpango unaogharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Taasisi ya Mapinduzi ya Kijani Afrika (Alliance for a Green Agricultural Revolution in Africa - AGRA).

Gharama za programu hii ni jumla ya dola za Marekani milioni 169.5. Lengo la programu ni kupunguza umaskini na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi endelevu kwa kuziwezesha kaya za vijijini kuongeza kipato na usalama wa chakula.

Programu hii inatekelezwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar. Ni programu inayohusisha uendelezaji wa miundombinu na mifumo ya masoko pamoja na uendelezaji wa huduma za kifedha vijijini.

Programu imesaidia kuongeza thamani ya mazao; kuwajengea uwezo na kuwaunganisha wananchi na masoko na imewezesha upatikanaji wa huduma za fedha vijijini. Kwa maeneo yanayopitiwa na barabara zilizojengwa na programu hii, shughuli za kiuchumi zimeongezeka na hivyo kuongeza kipato kwa jamii inayozunguka eneo husika. Tatu ni mradi wa Kuongeza Tija na Uzalishaji wa Zao la Mpunga (ERPP).

Taarifa inaonesha kwamba Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Maliasili Zanzibar zinatekeleza mradi wa kuongeza tija na uzalishaji wa zao la mpunga (Expanded Rice Production Project-ERPP) kwa ufadhili wa Mpango wa Kuendeleza Kilimo na Kuongeza Upatikanaji wa Chakula Duniani (Global Agriculture and Food Security Program-GAFSP).

Kupitia kamati yake ya uendeshaji, GAFSP ilikubali kuipatia Tanzania Dola milioni 22.9 kwa ajili ya kutekeleza mradi huu kwa muda wa miaka mitano (2015-2020). Lengo la mradi ni kuongeza uzalishaji wa mpunga kukidhi mahitaji ya ndani, na kupanua mauzo nchi jirani.

Lengo hili litatimia kupitia vipengele vinne, ambavyo ni mifumo endelevu ya mbegu; kuboresha uzalishaji wa mazao kupitia kilimo cha umwagiliaji bora na usimamizi wa mazao; mikakati ya ubunifu wa masoko na usimamizi na uratibu wa mradi.

Kwa upande wa Tanzania Bara, mradi unatekelezwa Morogoro katika halmashauri za Kilombero, Kilosa, Mvomero, Morogoro, Malinyi na Ulanga. Kwa Zanzibar, mradi unatekelezwa katika skimu za umwagiliaji za Kibonde Mzungu, Mtwango, Koani, Mchangani, Bandamaji (Unguja), Machigini, Kwalempona, Ole, Dobi – 1 na Dobi – 2 (Pemba).

Mradi huu umesaidia katika kuongezeka kwa tija katika zao la mpunga kutoka kuzalisha tani 1.8 kwa hekta mwaka 2013 mpaka tani 4.6 kwa hekta mwaka 2016/2017. Halikadhalika wakulima 7,100 wamepatamafunzo ya kilimo cha shadidi. Itaendelea

KATIKA makala mbili zilizopita tumeangalia manufaa ambayo wanavijiji wamepata kutokana ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi