loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Hoja dhaifu zisitumike ubunge Rorya

JIMBO la Rorya ambalo Lameck Airo amekuwa mbunge wake kwa vipindi viwili, lipo mkoani Mara. Kwa nyakati tofauti, Airo amesema hakusudii kugombea tena nafasi hiyo. Wakati ninaandika makala haya jana na juzi, nimejaribu kumtafuta, lakini simu yangu haikupokewa.

Ikumbukwe katika uchaguzi uliopita 2015, Airo pia alidai hatogombea, lakini baada ya kusoma upepo akaamua kugombea. Jimbo hili lina makabila makuu mawili ya Wasuba na Wajaluo. Lahaja za makabila haya ni pamoja na Wajaluo, Wasimbiti, Wahacha, Wasweta, Wakine na Wasulwa.

Mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mwalimu Chacha Matete wa Idara ya Elimu ya Ufundi katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia, Mbeya (MUST), ameandika katika mtandao wa kijamii wa WhatsApp anadai: “Kama ilivyo kawaida kwa wanasiasa kubuni mikakati na kuunda makundi ya kufanikisha ushindi, Jimbo la Rorya halikunusurika na hatua hiyo katika chaguzi zilizopita na hadi sasa hali hiyo ipo japo kunaweza kuwepo mabadiliko kidogo kimuundo, kimkakati na hata kimakundi.”

Matete anazidi kudai kwamba liliundwa kundi la watu sita waliokusudia kumiliki siasa za Rorya kwa maslahi yao na jamii zao, wakaliita G6 (Group of Six) na ili kufanikisha malengo yao katika chaguzi mbalimbali, wakaandaa mikakati mikuu mitatu.

Anadai kwamba kundi hilo liliandaa mikakati ambayo ni kuhakikisha kuwa, kwa gharama yoyote viti vya ubunge na uenyekiti wa Halmashauri ya Rorya mara zote wanavichukua wao yaani, watu wa maeneo ya Girango na Shirati. Hili ni jambo hatari kwa ustawi na maendeleo ya watu wa jimbo hili kwani inatakiwa kiongozi apatikane kwa sifa za utendaji na uadilifu siyo ukoo, ukabila au umaeneo.

“Ukimwacha Prof. Sarungi,” anadai Matete katika andiko lake mtandaoni: “Hakuna, kwa gharama yoyote iwayo, kuruhusu msomi yeyote wa Rorya kupewa nafasi ya ubunge wala kuwa mwenyekiti wa Halmashauri ya Rorya na mkakati wa tatu ni kuwadhibiti na kuwamiliki watu kwa gharama yoyote ili watumike kufanikisha malengo yao (G6) binafsi.”

Mwandishi mashuhuri Percy Bysshe, aliwahi kuandika katika andiko lake, ‘The Necessity of Atheism’ akisema jamii isiyo na wasomi ni jamii iliyo nyuma kimaendeleo, ni jamii inayochekwa na jamii jirani kwa kubaki nyuma kielimu.’

Serikali ya awamu ya tano imehakikisha inaboresha mazingira na miundombinu ya utoaji wa elimu katika ngazi mbalimbali likiwamo suala la elimu bila malipo kwa elimu ya msingi hadi kidato cha nne, na kutumia mabilioni ya pesa kuhakikisha wanafunzi wa elimu ya juu wanapata mikopo kwa wakati na kwa kiasi kinachotosha ili kuzalisha wasomi wa kutosha katika nyanja mbalimbali kuipeleka nchi kwa kasi katika uchumi wa viwanda.

Hongera Serikali ya Rais John Magufuli kwa kuchochea taifa kupata wasomi ili walitumikie vyema. Katika muktadha huo, mkazi mmoja wa Jimbo la Rorya ambaye hakutaka jina lake litajwe anasema kuna kipande cha video (clip) mtandaoni kinachomwonesha kiongozi mmoja wa CCM katika Mkoa wa Mara akisema, hataki wasomi wenye shahada kujipitisha katika kipindi hiki kutoa misaada.

Katika video hiyo kigogo huyo anasikika akisema: “Hao wenye madigrii (shahada) yao na ma-PhD (shahada za uzamivu), walikuwa wapi?” Bila kufafanua kama kigogo huyo yumo kwenye kundi la G6 au la, Mwalimu Matete naye anasema katika andiko lake kwenye WhatsApp: “Bwana huyu hajui na hataki kujua kuwa sasa hivi tunalo kundi kubwa sana la hao aliowaita wasomi wenye shahada za kwanza, uzamili na uzamivu (PhD) ambao hawana ajira rasmi na hivyo ubunge, udiwani ndio ajira wanayoilenga ili walitumikie taifa.”

Anasema: “Nimesoma na dada mmoja amemaliza shahada ya umahiri na amedunduliza sana mkopo aliokuwa anapewa na Bodi ya Mikopo akajisomesha shahada ya ubobevu 2019 sasa huyu mdogo wangu amenieleza anatia nia ubunge viti maalumu katika Mkoa wa Mara.

Kwa (kigogo) huyu anakosa sifa ya kuwa mbunge kwa sababu hakutoa hela ya kuchangia maendeleo, ajira hana mpaka sasa hivi na pesa ya kula hana, lakini huyu kigogo anataka hela ya mchango wa maendeleo!” Hii ni hoja ya ajabu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.

“Tatu, kigogo huyu hajui kutofautisha kati ya kuwa na elimu kubwa na kuwa na fedha; anadhani kuwa ukishakuwa profesa au daktari, basi una pesa nyingi sana. Wapo hao aliowaita wasomi tena wengi tu, lakini wapo hoi sana kiuchumi tena wanazidiwa kwa mbali sana kiuchumi na wasio na elimu kubwa ya darasani wanaofanya biashara zao hata katika vijiji vya Sota, Kibuyi, Ruhu, Utegi, Obwere, au hata pale mwalo wa Kanga, Kwa Kiberiti au Nyangabo.”

“Huyu bwana hajui kuwa wapo wasomi wana mawazo pevu kutoka vitabuni, lakini hawawezi kuyafanyia kazi, hawawezi kuwaelezea wengine na ni waoga sana kujaribu, hivyo wamebaki wakimya tu.”

Katika kipengele kingine Mwalimu Matete anaandika: “Mheshimiwa huyu hajui na hataki kujua kuwa kwa upande mwingine, kuchangia shughuli za maendeleo ya jimbo au kata ni kujitengenezea uadui, chuki na fitina dhidi ya mbunge na au diwani aliyeko madarakani katika eneo husika.”

Anafafanua kwamba siasa zimechafuliwa na wanasiasa waoga wanaopiga ‘kufuli’ watu waogope kuchangia ili wasionekane wanajipitisha jimboni au katani ili wachaguliwe. CCM haijawazuia wasomi wasigombee ubunge wala udiwani kwa madai kuwa hawakuchangia kile anachokiita michango ya maendeleo. Hoja hii siyo imara maana Tanzania kama taifa, nayo inawahitaji wasomi ndio maana inawasomesha vijana wake kila mwaka.

Kimsingi, suala la ukabila na ugonjwa wa kuwapanga watu katika mafungu ya wasomi na wasio wasomi, huenda ni woga wa G6 (wakubwa sita wasio wasomi) dhidi ya wasomi kwa kisingizio cha kutoleta maendeleo.

Ugonjwa huu ukiachwa sambamba na ukabila unaojikita katika koo, maendeleo katika Jimbo la Rorya yatazidi ‘kubemendwa’ na kudumaa kadiri siku zinavyokwenda maana katika ulimwengu wa sasa, kiongozi bora hapimwi kwa kuwa hakusoma sana au amesoma sana, bali kutokana na uadilifu wake, na uwezo wa kiutendaji, kukiongoza na uwezo wa kuwakilisha watu katika vyombo vya maamuzi.

Kama wanajimbo wa Rorya watakuballi kudanganywa na kubaguana kwa mafungu ya usomi na ukabila kwa misingi ya koo, wajue kadiri miaka inavyokwenda ndivyo watakavyozidi kurudi nyuma kimaendeleo huku ‘majimbo ndugu’ ya Tarime na Tarime Vijijini ‘yakikimbia’ kimaendeleo. Hoja ya wasomi ambao hawakuchangia maendeleo kujaribu kutumiwa kama kigingi kwao ni ugonjwa unaopaswa kukataliwa kwa 

nguvu. Kinachojitokeza ni kama vile G6 wanataka jimbo libaki kuwa la ‘mbunge mfadhili,’ badala ya dhana ya ‘mbunge mwakilishi.’

Dhana ya mbunge mfadhili ni ugonjwa unaowafanya wabunge wengi wakiwamo baadhi katika Mkoa wa Mara (wanajijua na wanajulikana) kutohudhuria vikao vya bunge na badala yake, wanajikita katika biashara na miradi yao ili wapate ‘tone la mvua katika bahari’ walitumie kudanganyia wananchi kama msaada wa maendeleo.

Rorya ikumbuke kuwa, jimbo lao haliwezi kuendelea kwa kutegemea ufadhili wa mbunge, bali ushirikishwaji wa watu wa kada na tabaka mbalimbali kuleta maendeleo yao. Hao, ndio wanatafutwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Hapana shaka ugonjwa huu ndio umelifanya Jimbo la Rorya kuwa na shule chache kulinganisha na maeneo mengine ya nchi kwa kuwa, hao wanaotaka ‘kuliatamia’ kwa kujificha katika ‘vichaka’ mbalimbali’ likiwamo suala la usomi, kimsingi wanalinda biashara zao na wepesi wa kupata tenda serikalini hasa katika halmashauri zao na siyo kuangalia maslahi ya umma.

Ndiyo maana ninasema, Jimbo la Rorya liwe makini, lisidanganywe kwa hoja dhaifu zinazobebwa na wachache ambao hawakusoma sana. Rorya ni jimbo la Watanzania wote kwa jumla.

Kimsigi inashangaza maana wakati baadhi ya makabila nchini yakiwamo ya Wahaya, Wanyakyusa na Wachaga yanapongezwa na kusifika kutokana na kupiga hatua kimaendeleo hasa kiuchumi, siri yao kubwa ikiwa ni kuthamini na kuweka mbele elimu kama ajenda ya kwanza na hivyo, Rorya wasidanganywe kuhusu umuhimu wa elimu.

Kauli kama hizi ni hatari maana zinaua ari ya watu kuondoa ujinga kupitia elimu hasa ya darasani. Rorya na hata jamii kwa jumla isikubali kudanganywa na yeyote kuona elimu kama jambo lisilo na maana au kana kwamba kusoma ni kashfa.

Huu ni mwelekeo wa kujaribu kuficha kushindwa kwa viongozi kulisimamia upungufu unaoifanya Rorya kudaiwa kuwa na sekondari mbili pekee za serikali za Nyanduga na Buturi. Hii ni tofauti na mkoani Kilimanjaro ambako takribani kila kijiji kina shule ya sekondari na ‘high school’ kila kata. Ndiyo maana ninasema katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, hoja dhaifu kama ukabila, udini, umajimbo, ukoo, usomi na jinsia zisipewe nafasi.

KATIKA makala mbili zilizopita tumeangalia manufaa ambayo wanavijiji wamepata kutokana ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi