loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Misingi 10 kuingia uchumi wa kati

MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi ametaja misingi 10 ya mambo yaliyochangia Tanzania kuingia kundi la nchi 50 duniani zenye uchumi wa kati, ikiwamo utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayochechemsha uchumi.

Dk Abbasi aliyasema hayo jana jijini hapa katika mkutano wake na waandishi wa habari, alipozungumza kwa kina sababu zilizochangia Tanzania kuingia kwenye uchumi wa kipato cha kati.

Alisema msingi wa kwanza ni amani na utulivu wa nchi na ambao awamu zote za uongozi, zimefanya juhudi ya kuimarisha.

“Tunawashukuru viongozi wote wa awamu zote, kwasababu hatukufika kipato cha kati kwa bahati, bali waliweka misingi ya uchumi ya kipekee,” alisema Dk Abbasi.

“Tunamshukuru Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere kwa misingi ya uchumi aliyoiweka. Rais mstaafu Ali Hassan mwinyi kwa mchango wake, Rais mstaafu Benjamin Mkapa ambaye kipindi chake Dira ya Taifa ilitengenezwa, Rais mstaafu Jakaya Kikwete alitekeleza aliyoyaweza na ikaja awamu hii ya tano.

“Kuna nchi zingependa kuwa na amani hazina amani, zingependa kuwa na utulivu hazina utulivu, na hii haikuja kwa bahati mbaya, ni kudra za Mungu na pia viongozi wetu ambao kila ambapo palikuwa na dalili cha chokochoko za ndani na nje ya nchi, palipokuwa na uzandiki, udhalimu ambao ungeweza kuleta kukosekana kwa utulivu walifanya kazi ya ziada kwa kutumia sheria za nchi kushughulikia huo uzandiki, ubazazi,” alifafanua.

Alisema Dira ya Maendeleo ilitoa mwongozo wa kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda. Alisema Tanzania ina viwanda zaidi ya 60,000 tangu nchi kupata Uhuru na ndani ya kipindi cha uongozi wa Rais John Magufuli, zaidi ya viwanda 8,000 vimeanzishwa, vimejengwa, vinafanya kazi na vingine vinamaliziwa.

“Hapa ninapozungumza Tanzania tunazalisha kila aina ya bidhaa, tunaunganisha matrekta, tunaunganisha mabasi, tunazalisha nondo, mabati, tunachenjua katika sekta ya madini, bidhaa nguo, vyakula mbali mbali leo hii vinazalishwa na vinatengenezwa Tanzania,” alieleza.

Dk Abbasi alisema msingi wa pili, ni mipango thabiti ya maendeleo, ambayo imefanywa na uongozi wa awamu zote.

“Tangu awamu ya kwanza, serikali imekuwa na mipango thabiti ya maendeleo, ilikuwa ni mipango yenye malengo makubwa, hivyo serikali itaendela kuenzi uwekezaji wa mipango yenye malengo makubwa ili kusaidia,” alisema.

Aliongeza kuwa msingi wa tatu ni utekelezaji usioyumba wa mipango ya maendeleo.

“Kwenye masuala ya maendeleo na mageuzi unaweza kuweka mipango lakini tusiweze kutekeleza, sisi tunatekeleza na awamu zote za uongozi zimetekeleza licha ya changamoto mbali mbali.

“Kuna nyakati tumekutana na majanga, uhaba wa rasilimali za kufanya kile tulichotamani kukifanya, na hata baadhi ya wenzetu kukengeuka, kuna wakati fulani tuliyumba, tunaanguka, tunajikung’uta na kuendelea kupiga kazi,” alisema Dk Abbasi, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Alisema msingi wa nne ni maamuzi magumu, ambayo yamefanywa na viongozi wa nchi, hususani Rais Magufuli ya kupambana na rushwa na wahujumu uchumi.

“Katika kipindi chote cha miaka 59 na husuani katika kipindi hiki cha miaka mitano, tumekuwa tukitekeleza kanuni muhimu sana kwenye dhana ya maendeleo ya maamuzi magumu “Hatuwezi kufika uchumi wa kipato cha kati kwa nadharia rahisi, kuna nyakati yamefanyika maamuzi magumu sana ya kupambana na wala rushwa, wahujumu uchumi, wanafiki, uzandiki na wakati mwingine ikatuletea shida, tukaitwa majina mnaenda kwenye dikteta, na wakati fulani tumekataa sera au maelekezo ya baadhi ya nchi ya kutaka tuenende wanavyotaka wao,” alibainisha.

Dk Abbasi alitaja msingi wa tano kuwa ni kutekeleza azma ya kujitegemea wakati msingi wa sita ni nidhamu katika matumizi ya fedha za umma, unaokwenda sambamba na msingi wa saba ambao ni miiko ya uongozi, ambayo iliwekwa tangu utawala wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere. Alisema msingi wa nane ni uwekezaji kwenye miradi mikubwa ya kimkakati iliyochechemsha uchumi.

“Kuna baadhi walikuwa wanabeza uwekezaji wa miradi ya kimkakati wakidai imewekeza kwenye vitu, lakini ukweli ni kuwa mradi wa kuzalisha umeme mpaka leo umezalisha ajira zaid ya 3,500 ambao hawakuwa na ajira na kwa sasa wanapata kipato,” alieleza.

“Kwenye Mradi wa Reli ya Kisasa, ukiangalia ni kitu ambacho kimechangia takribani ajira 8,000 huku viwanda vikichangia ajira zaidi ya 200,000, sasa tungewasikiliza wanaosema tunawekeza kwenye vitu watu hawa wasingepata ajira na ujira na nchi kuingia kipato cha kati,” alieleza.

Dk Abbasi alisema msingi wa tisa ni hatua ya serikali kuwekeza kwenye maendeleo ya watu, mambo ambayo yamegusa maisha ya watu kwa kupata kipato na huduma.

“Serikali imeimarisha sana sekta ya elimu ambayo pia imechangia upatikanaji wa ajira zaidi ya 6,000 na pia kuimarisha sekta ya afya, maji, umeme ambapo hadi ifikapo Juni mwakani vijiji vyote vitakuwa vimefikishiwa umeme,” alifafanua.

Alisema msingi wa 10 ni uamuzi wa serikali wa kuwezesha sekta binafsi, yenye tija kwa maendeleo ya taifa.

“Na ili kuendelea kuimarisha sekta hii, serikali imeanzisha mpango wa Blue Print ambayo imelenga kutatua changamoto za uwekezaji kwa sekta binafsi. Hii inapaswa kuendelea kutiliwa mkazo ili kuifanya Tanzania kufikia kiwango cha kipato cha kati cha juu na hatimaye kuwa nchi ya kiwango cha juu cha uchumi,” alieleza.

KATIBU Tawala wa Wilaya ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi