loader
TPDC yapewa eneo kujenga maghala 15 ya mafuta

TPDC yapewa eneo kujenga maghala 15 ya mafuta

OFISI ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam imetoa sehemu ya eneo la Kigamboni kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kwa ajili ya ujenzi ya maghala 15 ya kuhifadhia mafuta kipindi hiki ambacho shirika hilo limeanza biashara ya kuuza mafuta nchini.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alipokuwa akitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Kate Kamba.

Alisema hayo kwenye ziara ya chama hicho, kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali iliyopo Dar es Salaam. Makonda alisema baada ya vikao vyake na uongozi wa TPDC, kwa pamoja walikubaliana mambo mbalimbali ikiwemo ujenzi wa maghala hayo, ambapo TPDC katika kulitekeleza hilo waliomba kupatia eneo kwa ajili ya ujenzi huo, suala alilosema kuwa tayari limeshafanyika na kwamba kilichobaki ni kwenda kuoneshwa eneo la ujenzi.

“Katika kulitekeleza hilo, tayari eneo lilishapatikana kinachosubiriwa ni kwenda kuoneshwa eneo lao, jukumu hili lipo mikononi mwa Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sara Msafiri, nendeni mkaoneshwe ili kazi ya ujenzi ianze haraka nina imani kuwa fedha mnazo,” alisema Makonda.

Mbali na eneo hilo, Makonda aliitaka TPDC kujenga miundombinu ya gesi katika eneo la Pembamnazi, mahali ambapo panatarajiwa kujengwa viwanda mbalimbali takribani 40. Alisisitiza kuwa tayari mikakati ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami imeanza.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dk James Mataragio alisema TPDC imejipanga kikamilifu kuhakikisha inaingia katika biashara ya mafuta na kuleta ushindani kwa kampuni binafsi zilizopo, hatua itakayoondoa kupandishwa kwa bei ya mafuta holela na kusababisha uhaba wa nishati hiyo kwa nyakati tofauti. Alisema mbali na kutumika kusambaza mafuta ya biashara, maghala hayo pia yatatumika kuhifadhia mafuta kwa ajili ya akiba ya serikali.

Alisisitiza kuwa hata usambazaji wa nishati utakaofanyika, utajikita katika kutoa huduma zaidi na siyo biashara. Dk Mataragio alisema katika kipindi cha miaka mitano ijayo, wanatarajia watakuwa wamejenga vituo zaidi ya 100 nchi nzima kwa ajili ya kusambaza nishati hiyo na hivyo kumaliza changamoto za mara kwa mara zinazojitokeza katika maeneo mengi nchini.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/3cd34ebb5b55bd5e754bc5ca96e8462c.jpg

WAFANYAKAZI wa Kituo cha Redio ...

foto
Mwandishi: Oscar Job

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi