loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wananchi tembeleeni maonesho ya Sabasaba

Maonesho ya 44 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba, yalifunguliwa rasmi juzi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na yanaendelea kwenye Viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam.

Tunawahimiza wakazi wa jiji la Dar es Salaam na mikoa ya jirani, kwenda kwa wingi katika maonesho hayo, kutokana na faida zake nyingi na mojawapo ni teknolojia ya hali ya juu, inayooneshwa na baadhi ya washiriki.

Kwa mfano, wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), wamebuni mashine ya kupumulia (ventilator) inayosaidia wagonjwa hasa wa maeneo ya vijijini. Wanaonesha mashine hiyo kwenye banda lao.

Mashine hiyo ya DIT inatumia mfumo wa umeme wa kawaida au wa jua, na inaweza kuhifadhi umeme kwa muda hata kama umeme umekatika, hivyo kuifanya kuwa nzuri zaidi kwenye maeneo yenye changamoto ya umeme hususan vijijini.

Mashine hiyo inaweza kufungwa hospitalini na kutumiwa kama mashine nyingine zinazonunuliwa kutoka nje ya nchi.

Mashine za aina hiyo kutoka nje ya nchi, zinauzwa kati ya Sh milioni tano hadi 25. Faida nyingine ya maonesho hayo ya Sabasaba ni wananchi kupewa bure huduma za afya au kwa bei nafuu.

Kwa mfano, katika banda la Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwenye maonesho hayo, watu wanafanyiwa uchunguzi wa macho bila malipo. Wale wanaobainika kuwa na mahitaji ya kutumia miwani, wanauziwa kwa bei punguzo ya Sh 10,000 tu.

Pia, wanawake wamejitokeza kwa wingi katika banda hilo la Muhimbili, kufanyiwa uchunguzi wa saratani ya matiti bila malipo. Pia, ushauri kuhusu magonjwa mbalimbali unatolewa katika banda hilo.

Wagonjwa ambao wanakutwa na changamoto kubwa zaidi za kiafya, hasa kwenye macho na saratani ya matiti, wanapewa rufaa kwenda Muhimbili hospitalini Upanga au Mloganzila, kwa matibabu zaidi.

Aidha, katika banda la Maliasili, watu wanaelezwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama Pori (TAWA) juu ya utaratibu mpya wa mabucha ya kuuza nyama za wanyama pori. Mamlaka hiyo inawataka Watanzania wenye kutaka kufanya biashara hiyo, kufuata kanuni za kuendesha biashara hiyo nchini.

Kwa mujibu wa Naibu Kamishna wa TAWA, Imaan Nkuwi hatua ya kuanzisha mabucha hayo, inatokana na agizo la Rais John Magufuli kwa Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi zake kuangalia utaratibu wa kufanya biashara hiyo nchini. Nkuwi anasema kuwa wizara imekamilisha kuandaa Kanuni za mwaka 2020 zitakazotumika kuendesha mabucha hayo nchini.

FUKUTO la Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani linazidi ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi