loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Takukuru yawatia mbaroni walimu 3 kwa udanganyifu

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Kagera, inawashikilia walimu watatu wa Shule ya Sekondari Kalenge wilayani Biharamulo kwa tuhuma za kufanya udanganyifu wakati wa mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana.

Aidha, taasisi hiyo katika Mkoa wa Mwanza, imemkamata raia wa China, Sheng Binglin (40) kwa tuhuma za kushawishi na kutoa rushwa ya Sh 100,000 kwa Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Calfonia-Nyegezi aweze kumrejeshea mashine yake ya kuchezeshea mchezo wa bahati nasibu.

Taarifa kuhusu matukio hayo zilitolewa jana kwa nyakati tofauti na wakuu wa Takukuru wa mikoa hiyo. Mkuu wa Takukuru wa Mkoa wa Kagera, John Joseph, aliwataja walimu wanaoshikiliwa ni mkuu wa shule, Boniphace Eliab, makamu mkuu wa shule, Edwin Valentine na mwalimu wa taaluma wa shule hiyo ya Kalenge, Grevas Richard.

Alisema watu hao wanashikiliwa kutokana na kupokelewa kwa taarifa Juni 19 mwaka huu iliyokuwa ikiwatuhumu kufanya udanganyifu wakati wa mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana.

“Uchunguzi wa Takukuru ulibaini kwamba walimfukuza shule mwanafunzi mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa kwa kisingizo cha kuwa alikuwa mgonjwa na kisha wakati wa kufanya mitihani ulipofika, kwa njia za rushwa walitumia namba ya mwanafunzi huyo aliyefukuzwa ya mtihani na kumpatia mwanafunzi mwingine ambaye aliufanya,” alisema Eliab.

Aliema uchunguzi wa taasisi umebaini kwamba baada ya matokeo ya kidato cha nne kutoka, jina la mwanafunzi aliyekuwa amefukuzwa lilionekana kuwa amefaulu kwa kupata daraja la pili huku ikiwa inafahamika kuwa mwanafunzi halisi mwenye jina hilo alishafukuzwa na hakufanya mitihani.

Hali hiyo ilimfanya mzazi wa mwanafunzi aliyekuwa amefukuzwa shule kutoa taarifa Takukuru. Uchunguzi ulibaini pia kuwa katika shule hiyo iliyopo Kata ya Kalenge, Agosti mwaka jana kuna mwanafunzi aliyekuwa akiumwa na wakati anaendelea na matibabu, viongozi wa shule walimtaarifu kuwa amefukuzwa kwa utoro, hivyo hakuweza kuendelea na shule.

Mwanafunzi anayedaiwa kuingizwa kwa njia za rushwa kufanya mtihani (jina limehifadhiwa) kwa kutumia namba ya aliyefukuzwa, matokeo ya kidato cha nne yalipotoka alipata daraja la pili.

Kuhusu raia wa China aliyekamatwa, Naibu Mkuu wa Takukuru mkoa wa Mwanza, Daudi Ndyamukama alisema alishawishi na kutoa Sh 100,000 kwa Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Calfonia-Nyegezi aweze kumrejeshea mashine yake ya kuchezeshea mchezo wa bahati nasibu.

Kwa mujibu wa Naibu Mkuu wa Takukuru mkoa wa Mwanza, Daudi Ndyamukama, Sheng ambaye ni msimamizi wa kampuni wa JX Betting, alishawishi na kutoa rushwa baada ya mashine yake kukamatwa kwa kutokuwa na kibali, kuchezesha nje ya muda uliopangwa na serikali pamoja na kuhusisha watoto chini ya umri wa miaka 18 katika mchezo huo.

“Hata hivyo, Mchina huyo alipokuwa akitakiwa kufika kituoni kutoa maelezo kuhusiana na kosa hilo hakuweza kutii amri hiyo badala yake alipiga simu na kumshawishi ofisa mtendaji ampe rushwa ili amrejeshee mashine yake,” ilisema sehemu ya taarifa na kuongeza kwamba mtuhumiwa alifikishwa mahakamani jana.

MWITO umetolewa kwa wakulima kwenye mikoa yanayozalisha chakula kwa wingi ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi