loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

EAC tumieni NIMRCAF kudhibiti corona

TANZANIA ni moja ya nchi zilizofanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kukabiliana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (Covid-19), kwa kumuomba Mungu, huku jitihada mbalimbali za kitaalamu zikifanywa.

Chini ya uongozi mahiri wa Rais John Magufuli, licha ya kusaidia kuondoa hofu kubwa iliyokuwa imetanda awali kwa wananchi juu ya ugonjwa huo kutokana na kuua watu wengi, lakini alisimama kidete kuhakikisha nchi inaukabili kwa kuchukua hatua mbalimbali madhubuti.

Mbali na elimu iliyotolewa kwa wananchi, juhudi mbalimbali za kupambana na ugonjwa huo ikiwemo kufunga shule, kuzuia mikusanyiko ya watu isiyo ya lazima, uvaaji barakoa, kusafisha mikono kwa sabuni na vikataka mikono na mengineyo, wananchi waliendelea kufanya kazi bila kuwapo kwa zuio la kutotoka nje (lockdown).

Kati ya kazi kubwa zilizofanywa tangu kuibuka kwa ugonjwa wa covid-19, ni taasisi za utafiti kuangalia namna ya kupata dawa za mimea lishe kusaidia kukabiliana na ugonjwa huo, ikiwamo Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Tanzania (NIMR).

Taasisi hiyo ilipata dawa iliyopewa jina la NIMRCAF, ambayo inatokana na mchanganyiko wa vyakula na katika majaribio imeonesha ina uwezo mkubwa wa kudhibiti virusi vya corona.

Licha ya kuwa hakuna serikali ya nchi za EAC zilizotoa maombi ya kutaka dawa hiyo kusaidia kukabiliana na ugonjwa huo na kuvifanya virusi kuwa mfu, dawa hizo zimeelezwa kusafirishwa na kuonekana katika nchi mbalimbali.

Ni dhahiri kuwa, janga hili katika nchi za Afrika Mashariki limeweza kukabiliwa zaidi nchini Tanzania na mpaka sasa huduma kadhaa zimeanza kurejea katika hali ya kawaida, ikiwamo wanafunzi kurejea vyuoni na shuleni na shughuli za michezo na burudani kuruhusiwa.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Tiba Asili cha NIMR, Dk Justine Omolo ameeleza kuwa kuwa kuna taarifa za kuwapo kwa dawa hiyo inayotengenezwa Tanzania kwenye mipaka mbalimbali ya nchi za EAC.

Amesema awali walianza uzalishaji kwa chupa 800 kwa siku, lakini sasa wana uwezo wa kuzalisha chupa 8,000 kwa siku na wakati maambukizi ya homa hiyo yako juu nchini walikuwa wakiuza kwa kiasi kikubwa tofauti na sasa.

Alisema kwa sasa chupa 2,000 zinachukuliwa kwa siku na watu wengi wamekuwa wakitumia kama kinga, ikiwamo kuwapatia wanafunzi waliopo shule za bweni na watu ambao waliopata maambukizi ya virusi vya corona walitumia na kupata nafuu kubwa.

Kutokana na hali hiyo, ni vema nchi za EAC ambazo zimekuwa na ushirikiano katika masuala mbalimbali ikiwamo kukabiliana na ugonjwa huo, kutumia dawa hiyo ili kuleta nafuu kwa wananchi wake kwa kuagiza rasmi kutoka NIMR na siyo kuacha wafanyabiashara kuingiza kinyemela katika nchi zao.

Kitendo cha kuuza dawa hizo bila nchi kuomba rasmi moja kwa moja au kupitia balozi zake nchini, kunaweza kusababisha wananchi wa nchi hizo kuuziwa kwa gharama kubwa tofauti na uhalisia wake na kutumia bila kuzingatia matumizi halisi ya dawa hiyo muhimu.

Ni vema taasisi za afya katika nchi za EAC kuwasiliana na NIMR na kuweka mikakati ya kupatikana kwa dawa hiyo na kujua matumizi yake kusaidia kuokoa maisha ya wana jumuya wenzetu.

Ni ajabu kuwa, nchi nyingine zinaendelea kupambana na ugonjwa huo usio na dawa, wakati Tanzania ambayo ni nchi washirika wakiwa na dawa hiyo inayosaidia kwa kiasi kikubwa kukabili ugonjwa huo, huku ikifahamika kuwa katika ukanda huu NIMRCARF imefanya utafiti na kuonesha mafanikio makubwa.

MWITO umetolewa kwa wakulima kwenye mikoa yanayozalisha chakula kwa wingi ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi