loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kilimo kilivyochangia safari kufikia uchumi wa kati

SERIKALI ya Awamu ya Tano ingawa ilijipanga kuwa nchi ya uchumi wa kati ifi kapo mwaka 2025, lakini imefi kia hatua hiyo kabla ya wakati uliolengwa kutokana na mchango mkubwa wa sekta ya kilimo inayoandaa malighafi .

Katika makala haya, mwandishi BEDA MSIMBE anabainisha mafanikio ya mikakati ya Wizara ya Kilimo katika kufi kia malengo hayo. Katika mazungumzo na waandishi wa habari mkoani Morogoro hivi karibuni, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya anasema, kuingia Tanzania katika uchumi wa kati ni matokeo ya mapinduzi makubwa katika sekta ya kilimo ambapo kila mdau katika mnyororo wa thamani wa kilimo, anapaswa kufurahia.

Kwamba, sekta ya kilimo imeendelea kuchangia katika ufanisi katika viwanda kwa kuzalisha malighafi zinazotumiwa kutengeneza bidhaa mbalimbali za viwandani. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka huu zilizotolewa, kilimo kinachangia asilimia 65 ya malighafi kwa ajili ya viwanda.

Kusaya anasema, ongezeko hilo la mchango wa kisekta limetokana pia na utanuzi wa kilimo cha umwagiliaji na ndio siri ya mafanikio hasa kipindi hiki cha mabadiliko ya hali ya hewa.

“Ili kufanikisha hili, Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 461,326 mwaka 2015/2016 hadi hekta 694,715 mwaka 2019/2020 sawa na ongezeko la asilimia 33.6,” anasema.

Aidha anasema, tija ya uzalishaji katika skimu za umwagiliaji zilizoendelezwa imeongezeka kutoka wastani wa tani 1.8 – 2.0 kwa hekta mwaka 2015/2016 hadi wastani wa tani 4.0 – 5.0 kwa hekta mwaka 2018/2019 kwa zao la mpunga.

“Kwa upande wa mahindi, kumekuwa na ongezeko kutoka tani 1.5 kwa hekta mwaka 2015/2016 hadi tani 3.7 - 5.0 kwa hekta mwaka 2018/2019 na tani 13 kwa hekta mwaka 2015/2016 hadi 26 kwa hekta mwaka 2018/2019 kwa hekta kwa vitunguu; na tani 5 kwa hekta mwaka 2015/2016 hadi tani 18 kwa hekta mwaka 2018/2019 kwa zao la nyanya,” anasema.

SABABU YA MAFANIKIO

Mafanikio hayo yamechangiwa na kukamilika kwa miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa uboreshaji miundombinu ya Skimu ya Umwagiliaji ya Dakawa yenye ukubwa hekta 2,000 iliyogharimu Sh 21,156,050,278 na skimu 8 kati ya 16 zenye ukubwa wa hekta 2,547 za Mradi wa Kuendeleza Skimu za Umwagiliaji za Wakulima Wadogo (SSIDP).

Mingine ni pamoja na mradi wa ukarabati wa miradi 4 ya skimu za umwagiliaji zenye jumla ya ukubwa wa hekta 2,000 iliyogharimu Sh 1,166,220,000; na kukamilika kwa ujenzi wa mabwawa mawili ya Itagata iliyopo Itigi (Singida) na Dongobesh (Mbulu).

Mafanikio hayo pia yamechangiwa na skimu zilizojengwa kabla ya Awamu ya Tano ikiwemo skimu ya umwagiliaji ya Mbarali mkoani Mbeya. Katika uzalishaji wa mazao ya bustani katika kipindi hicho, uzalishaji wa mazao ya bustani (matunda, mboga, maua, na viungo) umeongezeka kutoka tani 5,635,364 mwaka 2015/2016 hadi tani 6,575,640 mwaka 2018/2019.

Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Kilimo anasema, thamani ya mauzo ya mazao ya bustani yakiwemo mbogamboga na maua nje ya nchi imeongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 412 mwaka 2015 hadi Dola za Marekani milioni 779 mwaka 2018/2019 na kuifanya tasnia ya mazao ya bustani kuchangia asilimia 38 ya fedha za kigeni zinazotokana na sekta ya kilimo.

Katika juhudi za kuhifadhi mazao kwa ubora unaostahili, serikali imekamilisha ujenzi wa ghala mbili katika Halmashauri ya Wilaya za Songea na Mbozi zenye uwezo wa kuhifadhi tani 10,000 na ukarabati wa ghala 105 zenye uwezo wa kuhifadhi tani 31,500.

Anasema: “NFRA (Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula), inatekeleza mradi wa ujenzi wa ghala na vihenge vya kisasa vyenye uwezo wa kuhifadhi tani 250,000 katika Halmashauri za Wilaya za Babati (tani 40,000), Mpanda (tani 25,000), Sumbawanga (tani 40,000), Mbozi (tani 20,000), Songea (tani 50,000), Shinyanga (tani 35,000), Dodoma (tani 20,000) na Makambako (tani 30,000).

Utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 60. Kuhusu utafiti na mafunzo ya kilimo, serikali imeimarisha shughuli za utafiti na ugunduzi wa kilimo kwa kuifanyia mabadiliko Sheria Na. 10 ya Mwaka 2016 ya kuanzisha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) iitwayo kwa Kiingereza TARI’s Act No. 10 of 2016. Mkurugenzi wa TARI Naliendele, Dk Fortunatus Kapinga anasema TARI imefanikisha tafiti za mimea na matumizi ya bidhaa mbalimbali za kilimo. Katika kipindi cha miaka minne, TARI imegundua aina 125 za mbegu bora huku kampuni binafsi zikigundua aina 35 za mbegu bora za mazao ya kilimo.

MCHANGO WA KILIMO

Pamoja na kilimo cha umwagiliaji, katika kipindi cha mwaka 2015/16 hadi 2019/20, Serikali imefuta ushuru, tozo na ada 105 na kupunguza nne kati ya 146 zilizokuwa zinatozwa katika mazao ya kilimo, pembejeo za kilimo na ushirika.

Kuondolewa kwa tozo hizi kumemwondolea mkulima kero, kupunguza gharama za uzalishaji na kuchochea uzalishaji na uwekezaji katika kilimo. Hatua hiyo imevutia sekta binafsi kuwekeza takribani Sh trilioni 3.7 katika mnyororo wa thamani wa kuendeleza mazao ya chai, kahawa, mkonge, ngano, shayiri na mpunga.

Uwekezaji huo umezalisha ajira 41,798. Aidha, Wizara ya Kilimo imehamasisha ujenzi wa viwanda ili kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na kutengeneza ajira kwa Watanzania.

“Katika kipindi cha miaka minne, viwanda vikubwa na vya kati vya kubangua korosho vimeongezeka kutoka 22 mwaka 2015/2016 hadi kufikia 31 mwaka 2019/2020.”

Anasema Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Kilimo. Viwanda tisa vilivyoongezeka vina uwezo wa kubangua korosho tani 25,000 kwa mwaka na vimeanzishwa katika mikoa ya Mtwara, Dar es Salaam na Pwani.

Aidha, vikundi vya kubangua korosho vimeongezeka kutoka 92 mwaka 2016 hadi 206 mwaka 2020. katika kipindi hicho, viwanda vitatu vya chai vimeanzishwa kikiwemo Kabambe Tea Factory (Unilever) chenye uwezo wa kusindika majani mabichi ya chai tani 50 kwa siku. Kiwanda hicho cha Unilever kimewekeza mtaji wa Sh bilioni 17.8 na kinaajiri watu 250 hadi 300 kwa siku.

Inaelezwa kuwa, viwanda vingine viwili ni Tropical Treasres Limited kilichopo Kilimanjaro chenye uwezo wa kusindika kilo 1,000 za majani mabichi kwa siku na Chai Collection Tanzania Limited kinachochanganya na kufunga chai kwenye vikasha kwa ajili ya hoteli kubwa na kinajiri watu 15 hadi 20 kwa siku kutegemeana na uzalishaji.

“Kwa zao la mkonge, viwanda vikubwa 11 vyenye uwezo wa kuchakata mkonge tani 7,193 kwa mwaka na viwanda vidogo 70 vyenye uwezo wa kuchakata mkonge tani 7,343.2 kwa mwaka vimeanzishwa na kuzalisha ajira 37,907,” kinasema chanzo.

Aidha, Sh bilioni 160.8 zimewekezwa katika uzalishaji na uendelezaji wa viwanda vya kahawa. Kiwanda cha Murzah Wilmar Rice Millers chenye uwezo wa kukoboa tani 600 za mpunga kwa siku, kimeanzishwa katika eneo la viwanda Kihonda Morogoro.

Kutokana na mazingira ya sasa, imeonekana dhahiri mipango iliyopo imewavutia vijana kujishughulisha na kilimo kupitia Mkakati wa Taifa wa Vijana kushiriki katika Kilimo wa Miaka Mitano (5) (National Strategy for Youth Involvement in Agriculture – NSYIA) uliozinduliwa Oktoba, 27, 2016 jijini Dar es Salaam ukilenga kuwavutia vijana kushiriki katika shughuli za kiuchumi kupitia sekta ya kilimo nchini.

Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu imewezesha mradi wa teknolojia ya kitalu nyumba (green house) katika halmashauri 81 katika mikoa 12 kwa kujenga vitalu nyumba 84 na kufikia vijana 8,700 ambapo Sh 3,138,000,000 zimetumika.

Aidha, Wizara imefanya makongamano ya kikanda na kuwafikia vijana wapatao 2,000. MASOKO Kusaya anasema ili kuhakikisha mazao ya kilimo yanapata soko ndani na nje ya nchi, Wizara imeanzisha kitengo kinachosimamia utafutaji wa masoko, kufanya tafiti za masoko na bei za mazao pamoja na kufuatilia mifumo ya uuzaji wa mazao.

Anasema: “Kupitia kitengo hicho kwa kushirikiana na Wizara za kisekta pamoja na sekta binafsi, serikali imeingia makubaliano ya kuuza muhogo mkavu nchini China.”

“Tani 2,242 za muhogo zimenunuliwa na kupelekwa na tani 850 zitasafirishwa tena baada ya mlipuko wa homa ya mapafu (Covid–19) kupungua au kumalizika. Aidha, Tanzania imenufaika na masoko ya nje yenye masharti nafuu ambayo hayana ukomo wa bidhaa wala ushuru wa forodha.”

Anafahamisha kuwa, masoko hayo yapo katika nchi za, China, India, Japan, Uswisi, Norway, Uturuki, New Zealand, Iceland, Brazil, Morocco, Jamhuri ya Korea; Soko la Marekani kupitia mpango wa AGOA (African Growth Opportunity Act); Umoja wa Ulaya, EAC, na SADC. Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na sekta binafsi imeimarisha matumizi ya mifumo ya masoko ikiwemo soko la bidhaa, stakabadhi za ghala, minada na kilimo cha mkataba.

Matokeo ya mifumo hiyo ni pamoja na kuviunganisha vyama vya ushirika 63 vinavyozalisha ufuta na kakao ili kuuza mazao yao kwa Mfumo wa Soko la Bidhaa.

Aidha,Kusaya anasema: “Wizara imewezesha na kusimamia vyama 16 vya ushirika vya wabanguaji wadogo wa korosho kutumia mfumo wa stakabadhi za ghala na kuuza tani 291,329.51 katika nchi za India, China na Vietnam.”

Matumizi ya mifumo hiyo yamesaidia kuimarika kwa bei ya mazao ya kilimo. Kwa mfano, bei ya zao la ufuta imeongezeka kutoka Sh 1,500 kwa kilo mwaka 2015/2016 hadi kufikia Sh 3,500 kwa kilo mwaka 2019/2020 huku bei ya kakao ikipanda kutoka Sh 3,200 kwa kilo mwaka 2015/2016 hadi Sh 5,000 kwa kilo mwaka 2019/2020.

Aidha, bei ya zao la korosho imeimarika kutoka wastani wa Sh 1,820 mwaka 2015/16 kwa kilo hadi kufikia wastani wa Sh 3,000 kwa kilo mwaka 2019/20 huku bei ya singa za mkonge nayo ikiongezeka kutoka Sh 2,083 kwa kilo mwaka 2015/16 hadi Sh 2,745 kwa kilo mwaka 2018/19 kwa mauzo ya ndani ya nchi.

Aidha, bei ya kahawa aina ya Arabika katika soko la ndani imeimarika zaidi kwa kuuzwa kwa Dola za Marekani 112 ikilinganishwa na bei ya Dola za Marekani 107.04 katika soko la dunia kwa gunia la kilo 50 na bei ya kahawa aina ya robusta ikaimarika kwa kuuzwa kwa Dola za Marekani 87.13 katika soko la ndani ikilinganishwa na Dola za Marekani 73.90 katika soko la dunia kwa gunia la kilo 50.

TAMKO la Kimataifa Kuhusu Haki za Binadamu (UDHR 1948), Mkataba ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi