loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Usimamizi shirikishi wa misitu unavyonyanyua uchumi, ulinzi

IJUMAA iliyopita, tulianza kuangalia manufaa ambayo nchi inaweza kuyapata kupitia Ulinzi Shirikishi wa Misitu (USM), hususani katika misitu ya vijiji ambayo ndio imekuwa ikikumbwa sana na uharibifu.

Uharibifu ambao umekuwa ukitokea kusiko na USM ni pamoja na ukataji wa misitu hovyo sambamba na tatizo kubwa ambalo limekuwa haliangaliwi kwa umuhimu wake la misitu kugeuzwa kuwa mashamba na hususani kupitia kilimo cha kuhamahama.

Utafiti uliofanywa hivi karibuni nchini ulionesha kwamba asilimia 89 ya upotevu wa misitu nchini inatokana na shughuli za kilimo, uchomaji mkaa huchangia asilimia saba, ufugaji na moto kwa asilimia tatu huku ufyekaji misitu kwa ajili ya uanzishwaji wa mashamba mapya ya miti ukichangia kwa asilimia moja.

Katika makala iliyopita, tuliangalia vijiji ambavyo vinanufaika na misitu kupitia USM kuwa ni pamoja na kijiji cha Nanjrinji A, kilichoko wilayani Kilwa, Lindi kikiwakilisha vijiji vingine katika wilaya hiyo vya Likawage, Ngea na vinginevyo.

Tuliona kwamba Nanjirinji katika kipindi cha kuanzia mwaka 2012 walipoamua kufanya USM kwa msaada wa shirika lisilo la kiserikali la kuhifadhi misitu (Mpingo Conservation & Development Initiative-MCDI) hadi mwaka jana wamefanikiwa kuingiza zaidi ya shilingi milioni 800.

Tuliona mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai na Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Renatus Mchau wakieleza namna USM ulivyopunguza kama si kuondoa kabisa utegemezi kwa serikali kutokana na kuvuna maliasili za misitu kwa njia endelevu na kuzilinda ipasavyo. Kwamba sasa wakazi wa Kilwa walioko mbali na bahari huwatambia wenzao wa pwani kwamba “kama nyie mnajivunia rasilimali za majini sisi tuna misitu.”

Pia tuligusia dhana kwamba kama USM ikisimamiwa nchi nzima kama ilivyofanyika kwenye madini kwa kufungua masoko, basi misitu inaweza kuingiza fedha nyingi sawa au hata zaidi ya madini.

Wakati madini yanaisha ardhini, misitu ikivunwa kwa njia endelevu inakuwepo milele na kuendelea kutoa manufaa mengine kama kuvuta mvua, kuhifadhi bayoanuai, kuzuia mabadiliko ya tabiachi, kulinda vyanzo vya maji na faida nyingine lukuki.

Kwa upande wa mkoa wa Morogoro, waandishi wa habari walitembelea vijiji mbalimbali vinavyonufaika pia na USM. Wakati Kilwa kinachovunwa zaidi ni mbao, Morogoro misitu huvunwa zaidi kwa ajili ya mkaa ambao sehemu kubwa unatumika katika jiji la Dar es Salaam.

Takwimu Msingi za Hewa Ukaa (Forest Reference Emission Level- FREL) za mwaka 2016 zilionesha kwamba asilimia 96 ya kaya nchini bado zinategemea nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia na kwamba asilimia 91 ya kaya katika jiji la Dar es Salaam zinategemea pia mkaa huku zaidi ya asilimia 50 ya mkaa wote unaovunwa nchini ukitumika Dar es Salaam.

Kinachofahamika ni kwamba bado kuna uchomaji mkaa mwingi holela nchini lakini kuna vijiji vinavyotekeleza USM mkoani Morogoro na hivyo kuvuna mkaa kwa njia endelevu na baadhi ya vijiji hivyo ndivyo vilivyotembelewa na waandishi wa habari.

Mwenyekiti wa kijiji cha Ulaya Mbuyuni, Kilosa, mkoani Morogoro, Selemani Hashimu, anasema Usimamizi Shirikishi wa Misitu kupitia Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS) unaojulikana zaidi kama mkaa endelevu umekuwa wa manufaa makubwa kijiji hapo.

“Kabla hatujaanza USM, kijiji kilikuwa kikiingiza mapato takribani sifuri na tulikuwa tegemezi kwa serikali au kuwachangisha wanakijiji tunapokuwa na mradi wa maendeleo. Lakini kupitia misitu sasa tunatembea kifua mbele,” anasema.

Anafafanua kwamba walianza kwa kupima msitu wao kisheria na hivyo kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi.

“Kabla ya mradi kulikuwa na wavamizi wengi katika msitu wa kijiji lakini kupitia elimu wameondoka. Hata hivyo, wamebaki wavamizi wachache ambao bado wameng’ang’ania kwenye msitu, hivyo kupitia kwenu waandishi wa habari tunaomba sana vyombo husika vitusaidie kuwaondoa,” anasema.

Anasema kupitia ushuru wanaopata kutokana na uvunaji wa msitu wamekuwa wakiingiza wastani wa shilingi milioni 100 kwa mwaka tangu walipoanza USM kwa msaada wa mashirika yasiyo ya kiserikali ya Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) na Shirika la Kuendeleza Nishati Asilia (TaTEDO).

“Baadhi ya mafanikio ambayo tumepata ni ujenzi wa madarasa mawili pamoja na ofisi ya mwalimu katika shule ya kijiji kwa thamani ya shilingi milioni 37, ujenzi wa kisima kirefu cha maji (milioni zaidi 20) na sasa tuna mradi wa ujenzi zahanati,” anasema.

Hata hivyo, anasema mapato yao yamesuasua hivi karibuni kufuatia hatua ya serikali kuanzisha kitu kinachoitwa bei elekezi ambayo wanapaswa kutoza kama ushuru.

“Hii bei elekezi imekuwa changamoto kwetu. Imefukuza wateja na kusababisha malengo yetu kuharibika. Sisi tulikuwa tunatoza ushuru wa Sh 6,500 lakini serikali inatutaka tutoze Sh 12,000,” anasema.

(Mjadala kuhusu bei hiyo utakuja katika makala zijazo). Kwa upande wake Pyaron Lyatuu, Ofisa Mtendaji wa kijiji cha Ulaya Mbuyuni anasema kwamba wamepata mafanikio makubwa kwa sababu wana miradi mingi ya maendeleo ambayo inawanufaisha wananchi na yote ni kutokana na USM.

“Kwanza USM imesababisha kutenga maeneo mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya ardhi ukiwemo misitu. Kwa upande wa misitu tuna sheria ndogo ya matumizi ya ardhi. Hatua hii ilisaidia pia kumaliza migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji au kijiji na kijiji.

Sasa hivi tuna eneo la makazi, la mashamba na hata wafugaji. Anasema mbali na mradi wa ujenzi wa zahanati lakini wamelipia kaya zaidi ya 200 huduma ya afya ya jamii (CHF), na pia wameboresha viwaja vya michezo kijijini Katibu wa Kamati ya Maliasili katika kijiji cha hicho cha Ulaya Mbuyuni Victoria Ndekelo anasema USM imekuwa sehemu ya maisha ya wakazi wa kijiji hicho kwani kutokana na elimu waliopata kupitia mashirika yaliyoleta mradi wa mkaa endelevu uliowafanya waanzishe USM imeleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi.

“Mbali na kuvuna misitu kwa njia ya endelevu lakini tumepata elimu ya vicoba, kilimo hifadhi, ufugaji nyuki, uvunaji mbao na faida nyingine lukuki kama vile wananchi kutochangishwa mara kwa mara kwa ajili ya miradi ya maendeleo,” anasema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kijiji cha Mlilingwa, kata ya Tununguo, Tarafa ya Ngerengere wilaya ya Morogoro, Salum Ally maarufu Kapombe anasema kuanzia mwaka 2017 hadi sasa walipoanza rasmi Usimamizi Shirikishi wa Misitu kupitia mradi wa Kutelata Magezi ya Mkaa nchini maarufu Mkaa Endelevu wamepata mafanikio makubwa.

“Tumepata mafanikio mengi, kubwa likiwa ni ulinzi wa misitu yetu kwa kuwa tunayo kamati ya maliasili ya misitu. Lakini kwa upande wa miradi tumejenga choo ya ofisi ya kijiji, tumejenga vyoo vya shule, tumejenga darasa na ofisi ya mwalimu na pia tumejenga madarasa matatu katika shule ya mkondo,” anasema.

Anaendelea: “Pia tumekarabati zahanati ya kijiji, tumelipia kaya zaidi ya 300 huduma ya afya kupitia Mfuko wa Afya ya Jamii na pia tumenunua baiskeli 12 kwa ajili ya wajumbe wa maliasili wanaofanya doria kwenye msitu wa kijiji.

“Kabla ya kuanza USM iliyokuja na mradi wa mkaa endelevu, msitu wa kijiji ulikuwa unatumika vibaya. Watu walikuwa wanakata misitu ovyo, wanalima ovyo lakini sasa hilo hakuna. Lakini tulipata pia elimu ya kilimo hifadhi kiasi kwamba sasa tunalima eneo dogo kwa manufaa makubwa,” anasema.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mlilingwa, Vicent Clement anasema.

“Kwa kifupi USM imekuwa na manufaa makubwa sana katika kijiji hiki. Na tunayashukuru sana mashirika ya TFCG, MJUMITA na TaTEDO ambayo yametupa elimu kuhusu matumizi bora ya ardhi na namna ya kuvuna misitu kwa njia endelevu na kuisimamia.

“Lakini pia faida kubwa ambayo tunapata ni kupunguza uhalifu wa misitu kwa sababu sasa tunavuna kwa njia endelevu na tuna kamati ya maliasili ya misitu ambayo kwa kujua manufaa tunayopata kutokana na misitu inafanya doria kila mara,” anasema.

“Faida nyingine ni kuondoa utegemezi. Hatusibiri tena serikali kuleta huduma kwenye kijiji au kuchangisha wananchi. Ile hali ya kusubiri nguvu za wananchi hapa Mlilingwa haipo… Ushuru wa kijiji kinaopata kupitia uvunaji endelevu wa misitu unafanya pia kazi ya kulinda misitu,” anasema.

Fatuma Mohamed, Mkazi wa Mlilingwa, Tarafa ya Ngerengere wilaya ya Morogoro, anayejitambulisha kama mchoma mkaa anasema mradi wa mkaa endelevu ambao ulikuja na elimu ya kuchoma mkaa kwa njia bora zaidi kupitia matanuri kichuguu yaliyoboreshwa umewafanya wavune kidogo na kupata mkaa mwingi.

“Mwanzoni tulikuwa tunachoma mkaa sisi wenyewe tunavyojua na hivyo tulipata mkaa kidogo sana. Na pia uchomaji ulikuwa kama wa wizi na tunakata miti holela lakini kwa sasa tunakata kwenye vitalu maalumu tulivyotengewa,” anasema.

Anasema mradi wa mkaa umemwongezea kipato na sasa amejiunga na benki za vijijini (vicoba) na kwamba kupitia mkaa anamudu kusomesha watoto wake na kwamba pesa anazopata kwenye mkaa anawekeza pia kwenye miradi mingine ikiwemo kilimo.

“Kwa sasa nimeachika lakini sijaathirika kitu kwani ninapata mahitaji yangu kupitia mkaa,” anasema.

Je, viongozi wa mkoa wa Morogoro walioona kwa macho yao manufaa ya USM wanasemaje? Na wanavijiji, viongozi na wadau wengine wanatoa maoni gani kuhusu kanuni mpya za mwaka jana kupitia tangazo la Serikali namba 417 (GN417) zinavyohamasisha wajibu wa kuandaa mipango ya uvunaji katika ardhi za vijiji kutoka kwa wanavijiji wenyewe kwenda kwa Mkurugenzi wa Misitu.

FERDINAND Kamuntu Ruhinda, Mwandishi wa Habari, Mshauri na Mwanastratejia wa ...

foto
Mwandishi: Hamisi Kibari

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi