loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kila la heri vikao vikuu CCM

KUANZIA leo hadi Jumapili wiki hii jijini Dodoma, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitakuwa na vikao vikuu vya chama hicho tawala, kinachoongoza serikali ambavyo vina umuhimu mkubwa kwa nchi.

Leo Kamati Kuu ya CCM chini ya Mwenyekiti wake wa Taifa, Rais John Magufuli, itakutana ambako pamoja na mambo mengine, itapendekeza majina matatu ya wanachama wake kati ya watano kuwania urais wa Zanzibar baadaye mwaka huu baada ya mchujo uliofanywa visiwani humo na vikao vingine.

Aidha, kesho Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM itapiga kura katika majina hayo matatu, kupata jina la mtu mmoja atakayepewa dhamana ya kupeperusha bendera ya chama hicho kuwania kumrithi Rais Dk Ali Mohamed Shein katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Kama hiyo haitoshi, Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM utafanyika kwa siku mbili Jumamosi na Jumapili wiki hii, ambao umuhimu wake mmojawapo ni kumchagua mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye amejitokeza mmoja tu, Rais Magufuli.

Kwa kuangalia kazi zitakazofanywa na chama hicho kwa siku hizo nne, ni dhahiri vikao hivyo ni muhimu, siyo kwa tu kwa Chama Cha Mapinduzi na wanachama na mashabiki wake, bali kwa mustakabali wa Tanzania kwa ujumla.

Ni chama ambacho kwa sasa kinaongoza serikali zote mbili, ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, hivyo umuhimu wa vikao hivyo kwa Watanzania ni mkubwa, kwani vinaamua mambo muhimu kwa maisha na ustawi wa wananchi wa pande zote mbili za Muungano.

Uteuzi wa mgombea wa urais wa Zanzibar ni suala linalogusa maisha ya watu wa visiwa hivyo na pia Watanzania, kwani huyu ni kiongozi wa juu katika serikali zote mbili, hivyo nani atapewa nafasi ya kuteuliwa kupeperusha bendera ya CCM Oktoba visiwani humo ni jambo linalosubiriwa na wengi.

Wanasubiri kumuona mtu ambaye kama atashinda Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, atakuwa na jukumu la kuendeleza mengi mazuri yaliyofanywa na Rais Shein katika miaka yake 10 ya Awamu ya Saba.

Lakini pia wananchi wanasubiri kuona CCM itampitisha Rais Magufuli, kuendelea na muhula mwingine wa pili, hasa ikizingatiwa makubwa aliyoyafanya kwa Watanzania katika miaka mitano inayomalizika sasa.

Wanataka kuona CCM inamrejesha ili kuendeleza mambo makubwa aliyoyafanya, ambayo yameifanya serikali yake ya awamu ya tano kuwa serikali ya kutolewa mfano katika kila kona ya dunia.

Ndio maana sisi tunasema hivi ni vikao muhimu sana kwa Watanzania, na kwa msingi huo tunaamini kuwa wajumbe wa vikao hivyo watatumia nafasi zao kujadili yote yaliyoelekezwa kwao, wakizingatia umuhimu huo kwa chama chao na kwa Taifa kwa ujumla.

FUKUTO la Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani linazidi ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi