loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Flaviana ajengea walimu nyumba Chalinze

MWANAMITINDO wa Kimataifa anayefanya shughuli zake nchini Marekani, Flaviana Matata kupitia Taasisi yake ya Flaviana Matata, amekabidhi nyumba mbili alizozijenga kwa ajili ya walimu katika Shule ya Msingi Msinune iliyopo kata ya Kiwangwa, wilaya ya Chalinze mkoani Pwani.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi wa ujenzi wa nyumba za walimu shuleni hapo iliyotokana na kukamilika kwa mradi wa kuboresha mazingira ya shule hiyo.

Uboreshaji huo wa awali wa mazingira ya shule ulijumuisha ujenzi na ukarabati wa madarasa, ujenzi wa ofisi za walimu na vyoo vya walimu na wanafunzi Pamoja na kujenga mfumo wa maji pamoja na hifadhi ya maji shuleni hapo.

Akizungumzia harakati zake hizo za kuimarisha mazingira ya kujisomea kwa wanafunzi hao, Flaviana alibainisha kuwa Taasisi yake inatambua nafasi ya walimu katika kufanikisha elimu bora kwa wanafunzi na ndio maana katika mradi mzima ameamua kujenga nyumba za walimu nane.

Alisema, nyumba hizo mbili za walimu ambazo ameshazijenga hadi sasa zina sebule, vyumba viwili vya kulala, jiko, choo pamoja na bafu huku zikiwa kwenye eneo zuri la kuishi walimu hao.

Alisema,“Taasisi yetu hii imekuwa ikishirikiana na shule ya Msinune kwa zaidi ya miaka mitano tulianza na kutoa bidhaa za masomo, tukaja visima, madarasa na kwa sasa tunaendelea na nyumba, taasisi inaamini kuwa kama walimu wakihakikishwa mazingira bora zaidi ya kuishi watafanya kazi zao vema zaidi”.

Flaviana akiwa shuleni hapo huku akishuhudiwa na viongozi mbalimbali wa Kijiji alimkabidhi mwalimu Anna Daudi ambaye ni mlezi wa wanafunzi wasichana shuleni hapo funguo wa nyumba huku akisisitiza kuwa anatambua kwa kumwezesha mwalimu huyo mahala pazuri pa kukaa anatengeneza pia mazingira rafiki kwa wanafunzi wasichana kujadiliana na mwalimu mambo kadhaa yahusianayo na makuzi kama wasichana.

Alienda mbali zaidi kwa kukabidhi vifaa vya watoto wa kike kujistiri pindi wanapokuwa kwenye siku zao za kila mwezi hivyo kuwasaidia kutokosa pindi wakiwa kwenye siku zao hizo, awali walikuwa wakikosa masomo hadi kwa siku nne wawapo mwezini.

Kwa upande wake Afisa Elimu Kata ya Kiwangwa, Kaduli Mbazi alisema nyumba hizo za walimu ni mchango mkubwa kwa kuwa umemgusa mwalimu moja kwa moja na kumfariji kwa kumhakikishia mahala sahihi na salama pa kuishi.

“Flaviana kupitia Taasis yake hii amekuwa Rafiki mkubwa kwetu, hakika amesaidia hata ufaulu nao kuongezeka kwa kiasi kikubwa na serikali inatambua hilo hakika kadiri ambavyo walimu watakuwa wakiajiriwa kipaumbele kitaletwa hapa shule ya Msinune ili jitihada za Taasisi ya Flaviana Matata zisikwame njiani wala zisififishwe kwa namna yoyote”.

Awamu ya pili ya mradi huo inatarajia kuanza kutekelezwa kuanzia Oktoba 2020 ambapo Taasisi hiyo inawakaribisha wadau kujitokeza kwa wingi zaidi kushirikiana nayo katika kuboresha elimu shuleni hapo.

KAMPUNI ya uzalishaji wa vifaa mbalimbali vya umeme cha Kilimanjaro ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi