loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Samaki ‘kaa mwizi’ awa kivutio Sabasaba

JAMII ya samaki kaa aitwaye Tuyuli au kaa mwizi kutokana na tabia yake ya kuiba nazi kwenye minazi, amekuwa kivutio kwa wananchi katika Maonesho ya 44 ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) maarufu Sabasaba, yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere.

Akimzungumzia kaa huyo katika banda la Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu(MPRU), Mhifadhi Utalii, Davis Mpotwa alisema jamii hiyo ya kaa aitwaye Tuyuli ni moja ya viumbe baharini vilivyo kwenye hatari ya kutoweka kutokana na wavuvi na watu kuwaua kupata kitoweo na wengine kuona ni viumbe waharibifu.

“Tuyuli tumemleta sabasaba kwa mara ya kwanza amekuwa kivutio kwa wananchi wanaotembelea maonesho haya, kwanza ni jamii ya kaa asiyejua kuogelea na anaishi kwenye mapango maeneo ya pwani chakula chake ni nazi, na vitu vingine lakini pia akikuta chakula au ugali anaiba anakula”,alisema Mpotwa.

Alisema Tuyuli ni jamii ya kaa ana uwezo wa kuwa mrefu hadi futi tatu na uzito wa kilogramu nne hadi tano na anaishi miaka 60 lakini pia anataga mayai zaidi ya 500 lakini yanayoanguliwa ni machache kutokana na tabia yake ya kutotulia hivyo kufanya samaki kuyala na mengine kuharibika.

Mpotwe alisema baada ya mayai yake kuanguliwa watoto wake huvaa magamba ya konokono kwa ajili ya kujilinda kwa sababu ngozi zao ni laini na wakianza kuwa wakubwa hujivua gamba na kuendelea na maisha yao kwani huwa na uwezo wa kujilinda wenyewe.

Alisema Tuyuli hajui kuogelea tofauti na kaa wengine na kwamba huishi zaidi maeneo ya Pwani kwenye mapango na hupenda zaidi kutembea na kula usiku kwa kupanda minazi kula nazi hivyo wananchi wa Pwani huwaua zaidi kwa kuwa wanasema ni waharibifu.

“Hawa Tuyuli ni viumbe waliohatariki kupotea, wanapatikana maeneo machache sana duniani ikiwemo Tanzania na hata hapa nchini wanaonekana zaidi kwenye Kisiwa cha Mbudya,Dar es Salaam ambacho bado kiko salama hakijaaribiwa,”alisema Mpotwa.

Alisema uwezo wa Tuyuli kukaa majini ni saa moja kisha anatoka na kwenda nchi kavu na kwenye mapango kutafuta malisho ikiwemo kupanda kwenye miti ya minazi kula nazi.

KAMPUNI ya uzalishaji wa vifaa mbalimbali vya umeme cha Kilimanjaro ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi