loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mauzo ya mboga, maua nje ya nchi yaongezeka

THAMANI ya mauzo ya mazao ya bustani yakiwamo mboga na maua nje ya nchi yameongezeka na kufanya tasnia hiyo kuchangia asilimia 38 ya fedha za kigeni zinazotokana na sekta ya kilimo.

Zao la parachichi ni miongoni mwa mazao yanayochipukia na ambalo limeonesha mafanikio makubwa katika miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Aidha, katika kuhakikisha mazao ya kilimo yanapata soko ndani na nje ya nchi, wizara imeanzisha kitengo kinachosimamia utafutaji wa masoko, kufanya tafiti za masoko na bei za mazao pamoja na kufuatilia mifumo ya uuzaji wa mazao.

Taarifa ya Wizara ya Kilimo inaonesha uzalishaji wa mazao ya bustani ambayo ni matunda, mboga, maua, na viungo, umeongezeka kutoka tani 5,635,364 mwaka 2015/2016 hadi tani 6,575,640 mwaka 2018/2019.

Thamani ya mauzo imeongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 412 mwaka 2015 hadi Dola za Marekani milioni 779 mwaka 2018/2019. Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, uzalishaji wa parachichi umeongezeka kutoka tani 20,000 mwaka 2015 hadi kufikia tani 190,000 mwaka 2018.

Kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa zao hilo, mauzo ya parachichi nje ya nchi yameongezeka kutoka tani 3,279 mwaka 2015 hadi tani 9,000 mwaka 2018. Mauzo hayo yaliyofanyika katika soko la Ulaya hususani nchi za Ufaransa, Uholanzi na Uingereza, yana thamani ya Dola za Marekani milioni 8.5.

Wizara kwa kushirikiana na Chama cha Wakulima wa Mboga na Maua Tanzania (Taha), imewezesha upatikanaji wa usafiri wa moja kwa moja wa mazao ya bustani kutoka nchini kwa kutumia ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia.

Ndege inapitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro badala ya kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyata nchini Kenya. Kwa mujibu wa waziri Hasunga, ndege hiyo itakuwa inachukua mizigo wastani wa tani 55 kwa wiki hatua ambayo imesaidia kuwa na usafiri wa uhakika, kupunguza gharama za usafirishaji, kupunguza upotevu wa mazao kwa kupunguza muda wa usafirishaji na kuongeza fedha za kigeni.

Wakati huo huo katika kuhakikisha mazao ya kilimo yanapata soko ndani na nje ya nchi, wizara imeanzisha kitengo kinachosimamia utafutaji wa masoko, kufanya tafiti za masoko na bei za mazao pamoja na kufuatilia mifumo ya uuzaji wa mazao.

Kupitia kitengo hicho kwa kushirikiana na wizara za kisekta pamoja na sekta binafsi, serikali imeingia makubaliano ya kuuza muhogo mkavu nchini China na tani 2,242 zimenunuliwa.

Tanzania pia imenufaika na masoko ya nje yenye masharti nafuu ambayo hayana ukomo wa bidhaa wala ushuru wa forodha. Masoko hayo yapo katika nchi za, China, India, Japan, Uswisi, Norway, Uturuki, New Zealand, Iceland, Brazil, Morocco, Jamhuri ya Korea.

Masoko mengine yapo Marekani kupitia mpango wa AGOA; Umoja wa Ulaya (EU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Vile vile wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na sekta binafsi imeimarisha matumizi ya mifumo ya masoko ikiwemo soko la bidhaa, stakabadhi za ghala, minada na kilimo cha mkataba.

KAMPUNI ya uzalishaji wa vifaa mbalimbali vya umeme cha Kilimanjaro ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi