loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Fursa nyingi, wanaoziona wachache

KUANZIA Julai Mosi, mwaka huu, Benki ya Dunia (WB) imeiorodhesha Tanzania katika orodha ya nchi za uchumi wa kati. Hatua hii inajiri miaka mitano kabla ya muda ambao Tanzania ilijiwekea kufi kia lengo hilo, mwaka 2025.

Hii ni ishara kwamba siasa za Tanzania zinaenda sambamba na ukuaji wa chumi wa taifa hili na kwamba, sifa hiyo itatusaidia kuvutia uwekezaji zaidi wa kigeni na kulifanya taifa kuimarika zaidi kiuchumi.

Japo Tanzania imeingia uchumi wa kati, Watanzania wanapaswa kufanya bidii zaidi kuboresha uchumi ili watoke katika orodha ya mataifa yenye kipato cha kati yaliyo na uchumi mdogo na kuwa taifa lenye kipato cha kati lenye uchumi unaoimarika.

Hili linawezekana endapo Watanzania wataamua, kwa dhati, kufanya tathmini upya na kuiongeza sekta nzima ya hakimiliki (sanaa na ubunifu) katika takwimu, kama lilivyofanya taifa la Nigeria, kwani sekta ya hakimiliki ni chanzo muhimu cha kichumi.

Mwaka 2014 Nigeria ilitangazwa kuwa ndilo taifa lenye uchumi mkubwa barani Afrika na kuipita Afrika Kusini, ikiwa na Pato Ghafi la Ndani (GDP) la Dola bilioni 509, baada ya wanauchumi wa nchi hiyo kuziongeza sekta za Mawasiliano na Filamu (Nollywood) kwenye takwimu.

Kwa hali hiyo, masoko ya Nigeria yamevutia mitaji ya uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi na kupunguza nakisi kubwa ya bajeti, jambo linaloongeza tija, uchumi kupaa na ushawishi wa nchi hiyo katika diplomasia na siasa za kimataifa.

Hii ni ishara ya jinsi gani sekta ya hakimiliki inavyoweza kukuza na kubadili uchumi wa nchi yoyote, kwa njia ya utoaji wa ajira kama itachukuliwa kwa umakini mkubwa. Matokeo ya kukubalika kwa kazi za sanaa na ubunifu pia huwafanya wasanii kuwa na heshima kwenye jamii na hata kisiasa.

Tanzania inahitaji kuichukulia sekta ya hakimiliki kama sekta mpya yenye mchango mkubwa kiuchumi na wasanii wenyewe wajue kuwa suala si kupata umaarufu tu ili uweze kuwasaidia kwenye mambo yasiyo ya kisanii, ikiwemo kukimbilia kwenye siasa.

Wapo wasomi wengi mitaani wamefungwa na vyeti vyao wakati wana vipaji lukuki na wana uwezo wa kuanzisha miradi katika sekta za ubunifu kama filamu, muziki n.k. lakini wamebaki kukosoa tu na wengine kulala fofofo.

Nimekutana na vijana wa kawaida sana hawajaenda hata shule, hawajui hata kuandika lakini wameweza kujiajiri kupitia sanaa na wanaingiza fedha kimchezo mchezo kuliko hata mameneja, na wengi wao wanamiliki kampuni, tena nyingi tu.

Hebu fikiria, kama kungekuwa na utaratibu wenye kueleweka nchi hii ingeingiza pato kiasi gani kupitia sekta hii muhimu? Watanzania wengi na Afrika kwa jumla wanapenda burudani, wanapenda kuburudishwa na hii ni fursa muhimu kwa wasanii.

Fursa katika sekta ya sanaa na ubunifu ni zaidi ya kawaida. Hili linaweza kuthibitishwa na wanaojiita wazee wa fursa, ambao wanaendesha matamasha ya muziki nchi nzima, utashangaa fedha wanazoingiza.

Milango iliyofunguliwa na fursa hii ni mingi, cha ajabu watu ni wagumu kuingia; fursa hii imefungua milango mingine zaidi ya fursa nyingine. Ni watu wachache wanaoliona hili, na hadi sasa kwa kiasi kikubwa mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nasib Abdul (Diamond Platnumz), ndiye anayeonekana kuiona milango ya fursa hizi, na sasa ameingia kufanya matamasha yake.

Watanzania wasishangae katika miaka michache ijayo, wakamshuhudia msanii huyu wa muziki akiajiri maprofesa na madaktari kusimamia miradi yake. Sekta ya sanaa na burudani ni biashara inayokua kwa kasi barani Afrika zaidi ya kawaida. Sekta hii imejaa fursa nyingi kupita kawaida. Yeyote atakayeamua kuichunguza sekta hii kwa makini atashangaa ilivyojaa fursa.

Kila siku mamilioni ya watu duniani wanahangaika kutafuta sehemu za kuburudika, vitu vya kujiburudisha, michezo na matamasha ya kufurahisha. Kwa mujibu wa tafiti zilizopo, sekta ya sanaa na burudani inatengeneza zaidi ya Dola za Marekani billioni 50 kila mwaka na inaongoza katika kutengeneza ajira kuliko sekta zote barani Afrika.

Tanzania yenye vivutio vingi vya utalii, kwa mujibu wa Ripoti ya Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) ya Mwaka 2019, ipo katika nafasi ya 12 duniani kwa ubora wa vivutio vingi vya utalii na ya kwanza barani Afrika.

Hivyo, Watanzania waangalie namna ya kuhusisha utalii na sekta ya hakimiliki. Vipaji vya sanaa na burudani nchini bado ‘vibichi.’ Dunia nzima sasa inahamia Afrika kwa sababu Afrika inaendelea kukua na kukua katika sekta ya burudani.

Hii fursa bado mbichi sana Tanzania. Japo watu wanafanya sanaa, lakini sekta hii bado haijaguswa vya kutosha. Wasanii katika sekta ya burudani ni zaidi ya watu wa kawaida. Wapo juu ya kilele.

Msanii katika burudani anaweza kuingiza fedha nyingi ndani ya nusu saa, fedha ambayo mtu mwingine anaweza kuipata kama akikusanya fedha hizo tokea anapojitambua mpaka uzeeni. Wao wanaweza kutengeneza ndani ya nusu saa na serikali inaweza kujipatia kodi kubwa, kama ikiiangalia kwa jicho la kiuchumi na kuijumuisha kwenye takwimu.

Kwa maoni yangu, sekta hii imejaa fedha nje nje kuliko kawaida, ingawa ukikutana na wasanii wengi maarufu utasikitika kuona kuwa maisha yao kwa asilimia kubwa hayana uhalisia, hii maana yake ni kuwa bado hawajagusa sekta hii ipasavyo. Kuna uzembe fulani wa kufikiri hapa na wanajua hivyo. Hakuna malengo hapa. Kuna ubabaishaji uliopindukia.

Hii ndiyo sababu wasanii wengi wanawasikika kuwa wanatumika kwenye mambo yasiyo na tija. Msanii ni mtu mkubwa duniani, siyo mtu wa mchezo mchezo lakini wasanii wetu Mungu awasaidie maana hawajaamka, ingawa kwenye muziki kuna unafuu kidogo tofauti na upande wa sanaa nyingine kama filamu, ambako soko la filamu ni kama limeparaganyika.

Wako wapi wafanyabiashara wajanja Afrika waweze kuichangamkia fursa ya filamu Tanzania? Watanzania wanatamani kuona filamu zenye ubora, lakini hazipo sokoni. Hakuna filamu nzuri sasa. Wasanii waseme wenyewe, mauzo ya filamu zetu yakoje kwa sasa? Yameshuka kuliko kawaida. Hii haimaanishi kuwa, Watanzania hawapendi filamu, bali filamu ‘za maana’ ni chache kuliko mahitaji ya soko.

Hii ndiyo sababu filamu na ‘series’ za nje, hasa za Kikorea, China na India zilizotafsiriwa Kiswahili zinatawala soko… hebu fikiria kama badala ya umaarufu wa series hizo, tufanye ingekuwa ni filamu mpya ya JB (Jacob Stephen) ni kiasi gani cha kodi serikali ingekusanya?

Lakini pia hao wanaotafsiri hizo filamu wanalipa kodi? Tunajua wanaharibu kwa kiasi gani sekta ya filamu ya Tanzania? Pia tujiulize, kwa nini hivi sasa filamu hizo zinatamba na kupata umaarufu? Ni kwa sababu wasanii katika tasnia ya filamu nchini walibweteka. Kwa maoni yangu, walibweteka na kusahau kuwa sanaa ndiyo inayoweza kutengeneza fedha nyingi sana kuliko hata kazi za kuvaa tai posta.

0685 666964 au bjhiluka@yahoo.com

FERDINAND Kamuntu Ruhinda, Mwandishi wa Habari, Mshauri na Mwanastratejia wa ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi