loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Tumebariki Usimamizi Shirikishi wa Misitu kwa kuona faida lukuki’

KATIKA makala mbili zilizopita tumeangalia manufaa ambayo wanavijiji wamepata kutokana na kuanzisha Usimamizi Shirikishi wa Misitu (USM) kwenye misitu ya vijiji vyao. Kulinganisha na misitu iliyo chini ya serikali au mamlaka nyingine, misitu ya vijiji ndiyo imekuwa ikikumbwa zaidi na uvunaji holela au kugeuzwa mashamba.

Kwa wanaofuatilia mfululizo huu wameona vijiji kadhaa katika wilaya za Kilwa mkoani Lindi na Kilosa, Morogoro na Mvomero mkoani Morogoro vilivyonufaika na misitu kupitia USM.

Je, macho ya viongozi mbalibali katika maeneo husika yanaona kama yanavyoona ya wananchi? Makala haya yanajibu: VIJIJI VINAPATA FEDHA Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Kilosa, Asajile Mwambambale anasema katika mahojiano na waandishi wa habari kwamba ni bahati kubwa kwa vijiji 20 katika halmashauri yake kufanya USM kupitia Mradi wa Kuleta Mabadiliko katika Sekta ya Mkaa (TTCS), maarufu kama ‘Mkaa Endelevu’.

“Katika vijiji hivyo kuna maeneo yanayotambulika kama hifadhi ya misitu ya vijiji na yanayoangaliwa na wanavijiji wenyewe ili yasije yakaathiriwa na matumizi ya binadamu. Uvunaji unafanyika katika maeneo hayo, lakini kwa njia ambayo inahakikisha misitu inaendelea kuwepo,” anasema.

Anasema kamati za maliasili katika vijiji husika zinalinda misitu kwa kuhakikisha hakuna anayevuna mazao ya misitu bila kupata kibali.

“Mtu akiomba kibali, hapewi hivi hivi, bali anajadiliwa na wanakamati, wanaangalia ni kiwango gani cha miti anakwenda kuvuna na kisha anasimamiwa ili kuona kama anavuna kwa kiwango kilichokubalika.

“Kwa hiyo vijiji vinapata pesa kwa wastani wa Sh milioni 30 hadi 40 kwa mwaka (kwa ajili ya shughuli za maendeleo ambayo ni asilimia 40 ya mapato). Kiwango hakijawa kikubwa sana kwa sababu sehemu ya mapato inafanya pia kazi ya uhifadhi wa misitu,” anasema.

Anasema vijiji vilivyoanza USM wilayani Kilosa vilikuwa 10, lakini baada ya kuona tija kubwa imepatikana mwaka 2015 vikaongezeka vijiji vingine 10 na kufikia 20.

“Sisi kama halmashauri kwenye miradi kama hii ya mkaa endelevu na inayowezesha usimamizi shirikishi wa misitu kwetu Kilosa ni muhimu sana. Kwanza inawezesha misitu kulindwa kwa maana ya kwamba maeneo ambayo hayana miradi kama hii watu wanavuna bila utaratibu na hivyo kutishia uhai wa misitu.

“Kwa hiyo faida ya kwanza ni uendelevu wa kuwepo kwa misitu na hivyo kuleta faida nyingi za misitu kama vile kutupatia hewa safi ya kuvuta, kulinda vyanzo vya maji, kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kadhalika.

“Faida nyingine ni kwamba misitu inapovunwa, vijiji vinapata fedha zinazoingia kwenye akaunti za vijiji. Fedha hizi zinapoingia kule, zinasaidia kwa kazi mbalimbali. Sisi kama halmashauri tunapata gawio la asilimia 10. Kama kijiji kimeingiza Sh milioni 20, halmashauri inapata Sh milioni mbili,” anasema.

MAHARAMIA WA MISITU WAMEBADILIKA

Mwenyekiti wa Halmashauri Wilaya ya Morogoro, Kibena Kingo, anasema usimamizi shirikishi wa misitu kupitia mkaa endelevu umeleta mabadiliko katika suala zima la hifadhi ya mazingira.

“Kwa mfano, katika Kijiji cha Mlilingwa kulikuwa na timu ambayo kazi yake ilikuwa ni kuvuna kwa njia haramu mazao ya misitu. Lakini kupitia USM, wote waliokuwa wanafanya hiyo shughuli wamelazimika kutafuta shughuli nyingine halali za kuwaingizia vipato.”

“Kwa mfano, wameanzisha mradi wa ufugaji wa kuku unaojulikana kama Boss Kuku na sisi kama halmashauri tuliwakopesha fedha kama kikundi kutoka kwenye fungu linalotengwa kwa ajili hiyo. Lakini pia, wameanzisha mradi wa kuvuna mbao kwa njia halali na kutengeneza samani mbalimbali.”

Kingo anasema na kuongeza: “Wameshapata tenda ya kupeleka milango katika Halmashauri ya Gairo kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya. Hata sisi katika halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, tumewapa tenda kama hiyo ya kutuuzia milango kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya.”

“Lakini pia mapato ya misitu wanafanyia miradi ya maendeleo mbalimbali bila kusahau ulinzi wa misitu. Kwa mfano, pale katika Kijiji cha Mlilingwa wameshapata kama Sh milioni 200. Hivyo, wanapanga bajeti zao, wamejenga madarasa, wanawalipia wananchi bima ya afya na shughuli nyingine za maendeleo. Siyo Mlilingwa pekee, bali na vijiji vingine kama Matuli, Diguzi na kwingineko.”

“Hatua hiyo imesaidia sana hata kuipunguzia serikali mzigo kwani ingelazimika kujenga madarasa, lakini sasa wanafanya wenyewe kupitia mapato yao,” anasema Mwenyekiti huyo wa Halmashauri ambaye pia ni Diwani wa Ngerengere anayemaliza muda wake.

SERIKALI IMEBARIKI HILI

Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilosa, Yohana Kasitila, anasema: “Mradi huu wa USM ulikuja kwa jina linalofahamika zaidi kwa wananchi kama Mradi wa Mkaa Endelevu, lengo lake kubwa lilikuwa kuwezesha wananchi kuvuna misitu kwa njia endelevu na kulinda mazingira.

“Kilosa ni wilaya iliyokuwa inasumbuliwa sana na migogoro ya ardhi na uvunaji holela wa misitu. Watu wanaingiza mifugo msituni... Siyo misitu ya vijiji pekee, bali hata iliyo katika milki ya serikali.”

“Mradi ulioletwa na TFCG (Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania) wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa (TTCS) kwa kushirikiana na MJUMITA (Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania) na kujulikana zaidi kama ‘mkaa endelevu’ tunaona una faida kubwa sana kwa wananchi hadi leo hii.”

“Kwanza wameweza kutunza misitu wenyewe na ule uvamizi wa misitu haupo. Lakini, kutokana na utumiaji mzuri wa misitu wamepata fedha zinazowezesha kijiji kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo.

“Kupitia mradi huu vijiji vimekuwa na uwezo wa kujenga ofisi za kisasa, wamejenga zahanati na madarasa kupitia fedha za mavuno ya mazao ya misitu kwa maana ya miti, mkaa na mbao na pia wanafundishwa namna ya kufuga nyuki.”

Anakwenda mbali na kufahamisha: “Sisi kama wilaya, tumelikubali jambo hili kwa sababu tunaona ni jambo ambalo linalenga kubadilisha hali ya maisha ya wananchi, badala ya kuendelea kuharibu misitu.”

“Ukiangalia, vijiji vyote vinavyoendesha mradi huu kwa kweli hali ya maisha pale imebadilika sana. Ikumbukwe kwamba, mradi unaenda sambamba na programu ya kuwafundisha wananchi ujasiriamali, kuanzisha vyama vya ushirika na vya kuweka na kukopa, kuendesha kilimo hifadhi na mambo mengi ya kitalaamu,” anasema.

“Ikumbukwe pia hata mkaa wanakata kitalaamu kwa kutenga eneo dogo tu la msitu kwa ajili hiyo huku wakiacha eneo lingine. Lile wanalovuna leo watalivuna baada ya miaka 15 hadi 20. Kwa hiyo, kuna mpangilio mzuri wa uvunaji unaowaletea faida kubwa.”

Je, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mohamed Utally naye anasema nini kuhusu USM? Madiwani je? Maofisa Misitu mkoani Morogoro na hata katika ngazi ya taifa wao wana lipi la kusema? Jumanne tutaendelea na mfululizo wa makala haya yanayoangalia faida na hasara kama zipo za Usimamizi Shirikishi wa Misitu (USM).

Yanatoa pia mtazamo wa wadau kuhusu Tangazo la Serikali Namba 417 (GN17) linaloonekana kupunguza kama si kuondoa kabisa uhuru wa vijiji kusimamia na kuamua juu ya masuala ya misitu yao kama Sheria ya Misitu ya Mwaka 2002 na ya kuyapeleka kwa mamlaka za kiserikali.

Nini faida ya tangazo hili na hasara zake? Kuna kitu pia kimeanzishwa kwenye uvunaji wa misitu kinachoitwa ‘Bei elekezi’ ambacho ni sehemu ya GN 417. Je, wadau wanasema nini kuhusu bei hiyo? Tukutane hapa Jumanne.

FERDINAND Kamuntu Ruhinda, Mwandishi wa Habari, Mshauri na Mwanastratejia wa ...

foto
Mwandishi: Hamisi Kibari

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi