loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

DC Moro ataka Nanenane isaidie wakulima

MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Bakari Msulwa amezitaka halmashauri za wilaya hiyo kuhakikisha Nane Nane Kanda ya Mashariki inawasaidia wakulima, wafugaji na wavuvi kubadili shughuli zao za uzalishaji ili ziwe na tija itakayowaletea manufaa yao na Taifa.

Alitoa agizo hilo kwa viongozi wa halmashauri hizo mbili alipokuwa katika ziara ya kukagua vipando vya mashamba darasa ya mazao banda la Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.

Kanda ya Mashariki inaundwa na mikoa ya Tanga, Pwani, Dar es Salaam na Morogoro na halmashauri kadhaa zipo katika maandalizi ya wiki ya maadhimisho hayo kuanzia Agosti mosi hadi 8 mwaka huu kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere mkoani Morogoro.

Msulwa alisema maonesho ya wakulima na wafugaji ya Nanenane yapo miaka mingi katika kanda mbalimbali na kuna vitu vya kuvutia vinavyozalishwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa na mbinu bora za kilimo na mifugo ambazo zina uwezo wa kuleta tija kubwa.

“Teknolojia na ubunifu unaopatikana kwenye maonesho haya unahitaji kuwafikia wakulima wa chini, tusiwe tunaandaa maonehso haya kwa ajili ya tabaka la watu wenye nacho tukawasahau wale wa hali ya chini ambao ndiyo wanaojihusisha na kilimo,” alisema Msulwa.

Alizitaka halmashauri hizo kuhakikisha mashamba darasa yanakuwa vituo vya kudumu na wataalamu wa kilimo na mifugo kutakiwa kuwepo eneo hilo kipindi chote cha mwaka ili kusimamia shughuli hizo.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba aliwataka wasimamizi wa mashamba darasa kukamilisha maandalizi ili halmashauri ifanye vizuri ngazi ya Kanda ya Mashariki.

“Maofisa mifugo na kilimo ngazi zote ongezeni nguvu katika maeneo haya, muda si rafiki, tuna wiki tatu za maandalizi, tuhakikishe kila kinachotakiwa kimefanyika,” alisema Lukuba.

Ofisa Kilimo wa Manispaa wa hiyo, Michael Waluse, alisema maandalizi yanaendelea vizuri na washiriki ni wakulima, wakala wa kampuni za pembejeo na wasindikaji wa mazao nchini.

KAMPUNI ya uzalishaji wa vifaa mbalimbali vya umeme cha Kilimanjaro ...

foto
Mwandishi: John Nditi, Morogoro

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi