loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Flaviana Matata ajenga nyumba za walimu

MWANAMITINDO wa kimataifa wa Tanzania anayefanya shughuli zake Marekani, Flaviana Matata, kupitia taasisi yake, amekabidhi nyumba mbili alizozijenga kwa ajili ya walimu wa Shule ya Msingi Msinune, kata ya Kiwangwa, wilaya ya Chalinze, mkoani Pwani.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi wa ujenzi wa nyumba za walimu shuleni hapo iliyotokana na kukamilika kwa mradi wa kuboresha mazingira ya shule hiyo.

Uboreshaji huo wa awali wa mazingira ya shule ulijumuisha ujenzi na ukarabati wa madarasa, ujenzi wa ofisi za walimu na vyoo vya walimu na wanafunzi na kujenga mfumo wa maji pamoja na hifadhi ya maji shuleni hapo.

Akizungumzia harakati zake za kuimarisha mazingira ya kujisomea kwa wanafunzi hao, Flaviana alisema taasisi yake inatambua nafasi ya walimu katika kufanikisha elimu bora kwa wanafunzi na ndio maana katika mradi mzima ameamua kujenga nyumba za walimu nane. Alisema nyumba hizo mbili za walimu ambazo ameshazijenga hadi zina sebule, vyumba viwili vya kulala, jiko, choo na bafu, huku zikiwa kwenye eneo zuri la kuishi walimu.

“Taasisi yetu hii imekuwa ikishirikiana na shule ya Msinune kwa zaidi ya miaka mitano sasa, tulianza na kutoa bidhaa za masomo, tukaja visima, madarasa na kwa sasa tunaendelea na nyumba, taasisi ina amini kuwa kama walimu wakihakikishwa mazingira bora zaidi ya kuishi watafanya kazi zao vema zaidi,” alisema.

Flaviana akiwa shuleni hapo huku akishuhudiwa na viongozi mbalimbali wa Kijiji, alimkabidhi Mwalimu Anna Ambare, mlezi wa wanafunzi wasichana shuleni hapo funguo ya nyumba hizo, huku akisisitiza kuwa anatambua kumwezesha mwalimu mahali pazuri pa kukaa anatengeneza pia mazingira rafiki kwa wanafunzi wasichana kujadiliana na mwalimu mambo kadhaa yahusianayo na makuzi kama wasichana.

Aidha, Flaviana alikabidhi vifaa vya watoto wa kike kujistiri wanapokuwa kwenye hedhi kila mwezi, hivyo kuwasaidia kutokosa masomo. Ofisa Elimu Kata ya Kiwangwa, Kaduli Mbazi, alisema nyumba hizo za walimu ni mchango mkub- wa kwa kuwa zimemgusa mwalimu moja kwa moja na kumfariji kwa kumhakikishia mahala sahihi na salama pa kuishi.

“Flaviana kupitia taasisi yake hii amekuwa rafiki mkubwa kwetu, hakika amesaidia hata ufaulu nao kuongezeka kwa kiasi kikubwa na serikali inatambua hilo hakika kadiri ambavyo walimu watakuwa wakiajiriwa kipaumbele kitaletwa hapa shule ya Msinune ili jitihada za Taasisi ya Flaviana Matata zisikwame njiani wala zisififishwe kwa namna yoyote,” alisema.

Awamu ya pili ya mradi huo inatarajiwa kuanza kutekelezwa kuanzia Oktoba, mwaka huu.

KAMPUNI ya uzalishaji wa vifaa mbalimbali vya umeme cha Kilimanjaro ...

foto
Mwandishi: Rahimu Fadhili

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi