loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

CCM yataja sababu Magufuli kuendelea

JINA la Rais John Magufuli leo linawasilishwa kwenye Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), umchague awe mgombea wa urais, atakayepeperusha bendera ya chama huku zikitajwa sababu lukuki za kupitisha jina lake pekee.

“Kila mwana CCM ameridhika na utendaji wake na kukubali kwamba anatosha na chanda chema huvikwa pete,” ilisema sehemu ya rasimu ya tamko, lililosomwa mjini Dodoma jana na Katibu Mkuu wa chama, Dk Ally Bashiru.

Tamko hilo linawasilishwa leo katika Mkutano Mkuu, mjini humo. Rasimu hiyo iliyotaja sababu za msingi lukuki zilizosukuma chama kupendekeza jina pekee la Rais Magufuli kupeperusha bendera yake kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, ilisomwa mbele ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Chini ya uenyekiti wa Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais Dk Ali Mohamed Shein, wajumbe waliridhia kwa kauli moja, baada ya Dk Bashiru kutaja sababu hizo, ikiwamo ya kwamba Rais Magufuli ameweza kukidhi vigezo vinavyohitajika kwa mujibu wa sheria za nchi, katiba ya nchi na ya CCM na kanuni zake.

Alisema Magufuli anakidhi sifa zote bila kutiliwa shaka huku kukiwapo nyingine za ziada kwa upande wake, ambazo ni pamoja na kiwango cha utumishi uliotukuka kwa wananchi siyo tu ni cha uzalendo, bali ni mfano wa kuigwa ndani na nje ya mipaka ya nchi.

Alimtaja Magufuli kuwa ni mchapakazi, mfuatiliaji makini, mzalendo wa kweli, mwaminifu, mwadilifu kwa nchi yake, mlinzi wa rasilimali za taifa, mpenda haki na mwenye ujasiri na utashi wa kuongoza mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa, uzembe, uvivu , wizi wa mali za umma na zaidi ya yote ni kipenzi cha wananchi na mtetezi wa wanyonge.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake, ameliongoza taifa kwa heshima na mafanikio makubwa, ambayo hayakuwahi kushuhudiwa. Alisema amesimamia Ilani ya CCM kwa umahiri, weledi na ufanisi mkubwa.

“Tutatoa chapisho la wasifu utakaonesha sifa za utendaji wake,” alisema Dk Bashiru.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo wa CCM, wananchi wengi, wanachama na wasio wanachama, wanaridhishwa na utendaji, maono yake na utashi wa kisiasa, hasa kuhusu maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

“Uthibitisho wa hili, yeye ndiye mwanachama pekee wa CCM aliyechukua fomu ya kuomba na kuteuliwa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Maana yake ni kwamba kila mwana CCM ameridhika na utendaji wake na kukubali kwamba anatosha na ‘Chanda chema huvikwa pete’,” alisema.

Alisema, “Kutokana na sababu hizo, pamoja na nyingine Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kwa unyenyekevu mkubwa tunapenda kuwasilisha mbele ya Mkutano Mkuu wa Taifa jina la Dk John Magufuli Mwenyekiti wa CCM na kupendekeza kuwa yeye ndiye apigiwe kura za ndiyo ili awe mgombea wa CCM katika nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Tanzania.”

Akizungumza baada azimio hilo kuridhiwa wakati Rais Magufuli akiwa amepisha kikao kiendelee, Dk Shein alisema wamekubaliana jina lake liwe pekee kwa ajili ya kazi moja kubwa ya kumteua kwa kumpigia kura nyingi za ‘Ndiyo’ awe mgombea.

“Sisi wajumbe tumevutiwa sana na sifa zako, uwezo wako na namna gani umeitumika nchi hii kwa miaka mitano. Unastahili upate sifa hizo, na sote kwa kauli moja tumekubali tulipeleke jina lako kwenye Mkutano Mkuu kesho (leo) uwe peke yako, upigiwe kura za ndiyo uwe mgombea wetu, upeperushe bendera ya chama chetu kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka huu,” alisema Dk Shein.

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi