loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mawakili badilikeni, mkabiliane na uchache wa ajira – Jaji Mkuu

Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma amewataka mawakili kubadilika na kuwa tayari kukabiliana na uchache wa ajira katika nyakati hizi.

Amesema ni jambo la kawaida kwa wanasheria wanaomaliza mafunzo ya vitendo katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria Kwa Vitendo na kukubaliwa kuwa mawakili, kukosa ajira katika taasisi za umma, ambazo awali ndizo zilikuwa zikiajiri asilimia kubwa ya wahitimu hao. Jaji Mkuu aliyasema hayo jana wakati wa Hafla ya 62 ya Kuwakubali na Kuwapokea Mawakili Wapya 601.

Alieleza kuwa tatizo la mawakili kukosa ajira rasmi, si la Tanzania peke yake, bali hata mataifa makubwa kama Australia na Marekani, hutoa elimu ya sheria yenye ubora wa hali ya juu, wanakabiliana nayo kutokana mabadiliko tofauti, ikiwemo watu wa fani nyingine kusoma sheria pia.

“Siku hizi fani zingine na wanataaluma wengine kama wahandisi, wahasibu na wachumi wanasoma sheria na hivyo kazi nyingi za kisheria wanafanya wenyewe bila kutafuta huduma za mawakili,” alisema.

Aliongeza kuwa hata taasisi za serikali na mashirika ya umma, hayatafuti tena huduma za kisheria na uwakili, kutoka kwa makampuni binafsi ya mawakili. Alisema hali hiyo inatokana na siku hizi ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kufanya kazi nyingi za kiuwakili, ambazo zamani zilikuwa zinafanywa na makampuni ya mawakili wa kujitegemea.

Kwa hiyo, alisema ajira za zamani ambazo mawakili walikuwa wanapata, sasa hazipo tena. Aliwataka mawakili hao, kuwa tayari kufanya kazi katika Karne ya 21 yenye ushindani mkubwa. Alisema Karne ya 21 imeipa kazi ya uwakili msukosuko mkubwa, ambao taaluma ya sheria haijawahi kukumbana nao katika karne zilizopita.

“Katika miaka 20 ya mwanzo baada ya Uhuru wa Tanzania Bara mwaka 1961, mwanasheria aliyekuwa anamaliza masomo chuo kikuu alikuwa na uhakika wa kupata ajira bila ushindani wowote. Serikali kuu, serikali za mitaa na mashirika ya umma walikuwa na nafasi tele za ajira bila ushindani wowote. Tanzania hiyo iliyo iliyokuwa na ajira hizo zisizo za ushindani haipo tena, na kila mmoja wenu afahamu hilo,” alisema Jaji Mkuu.

Pia Jaji Mkuu aliwataka mawakili hao, kusoma Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 kwani inaielezea Karne ya 21 kuwa yenye sifa kubwa ya ushindani na itakayomilikiwa na wenye teknolijia. Alisema wakiisoma vizuri Dira hiyo ya Taifa, wataendana na mabadiliko makubwa ya teknolojia katika utendaji wa kisheria.

“Mabadiliko makubwa na ya haraka ya kiuchumi, teknolojia, siasa, kijamii na hata kiutamaduni, yamefanyika kwa kasi kubwa zaidi ya uwezo wa sheria, uwezo wa wanasheria na uwezo wa mawakili kuhimili mabadiliko hayo. Ili muweze kuelewa ushindani ambao kila wakili atakayefanya kazi katika Karne ya 21 atarajie. Someni Dira ya Taifa ya Maendeleo na msome mkijua mnaingia katika soko la ushindani ambalo tayari lina maelfu ya mawakili waliojiimarisha,” alisema.

Aidha, Jaji Mkuu aliwataka mawakili hao, kufanya kazi zao za uwakili kwa uaminifu, kusimamia haki, kuepuka rushwa na kutimiza haja za wananchi ; na siyo kusubiri kupeleka mashauri mahakamani.

“Rushwa inaweza kutumika kama silaha mbaya kunyima, kudidimiza na hata kuchelewesha haki. Kwa umri wenu, mkijaaliwa uhai na Mwenyezi Mungu, bado mnayo miaka zaidi ya ishirini na tano mbele yenu ya kusaidia kubadili na kuiboresha Tanzania kupitia taaluma yenu ya Sheria. Tendeni haki,” alisema.

KAMPUNI ya uzalishaji wa vifaa mbalimbali vya umeme cha Kilimanjaro ...

foto
Mwandishi: Anna Mwikola

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi