loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Simba vs Yanga Ni mechi ya kisasi na heshima

NUSU fainali ya Kombe la shirikisho la Azam (FA) inatarajiwa kuchezwa kesho mabingwa wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara Simba wakitarajiwa kuchuana na mabingwa wa kihistoria Yanga kwenye dimba la taifa, Dar es Salaam.

Mchezo huo ni muhimu hasa kwa Yanga wanaotafuta nafasi ya uwakilishi kimataifa tofauti na wenzao Simba ambao wanatafuta kujenga heshima kutwaa makombe yote ambapo tayari wana uhakika wa kushiriki ligi ya mabingwa Afrika baada ya kutwaa ubingwa wa ligi.

Mechi ya kisasi Pamoja na kwamba ni mchezo ambao Yanga anatakiwa ashinde ili kutinga fainali na kutafuta nafasi hiyo ya kimataifa, mchezo huo unaweza kuwa mgumu tofauti na walipokutana huko nyuma.

Msimu huu wamekutana mara mbili, Yanga ikiibuka kidedea kwa kushinda mchezo mmoja kwa bao 1-0 na kutoka sare ya mabao 2-2. Kwa matokeo hayo, wekundu hao wa Msimbazi wana hasira wanataka kulipiza kisasi kwa kushinda na kutinga fainali.

Wao wala hawana shida ya kutafuta nafasi ya uwakilishi kwasababu tayari wamejihakikishia kupitia ubingwa wa ligi wanachoangalia ni kuwafunga watani zao na kutinga fainali ili hatimaye kuchukua kombe la pili msimu huu.

Iwapo watafanikiwa kuweka rekodi hiyo ya kuchukua taji itakuwa ni furaha kwao na watakuwa wametimiza malengo waliyojiwekea msimu huu kuchukua mataji zaidi ya moja.

Timu hizi zinapokutana furaha kubwa ya mashabiki wao wanataka kuona mmoja anakufa kwa maana lazima ashinde au afungwe. Je, Simba watafanikiwa kulipiza kisasi?

Yanga wanatamani kuendeleza rekodi yao bora msimu huu ya kutofungwa na Simba lakini pia, ni mechi ya presha kwao wanahitaji kushinda ili kusonga mbele na kutafuta nafasi ya kuwakilisha nchi kimataifa mwakani.

Mechi hiyo unaweza kusema ni kama vile mtu anaweka roho mkononi, presha ya kupanda na kushuka kwani Yanga akifungwa ndoto zake za uwakilishi wa kimataifa mwakani zitaishia taifa hivyo ana kazi kubwa ya kupambana kufa au kupona kumng’oa Simba.

Historia Ukiachilia mbali historia za timu hizo kukutana miaka kadhaa, wanatengeneza rekodi nyingine mpya ya kukutana hatua ya nusu fainali kwenye michuano hiyo iliyorejea miaka ya karibuni.

Hawajawahi kukutana katika hatua hiyo, baada ya Simba kuchukua ubingwa wa FA msimu wa 2016/2017 kwa kumfunga Mbao mabao 2-1 kwenye fainali, miaka iliyofuata walikuwa wanaishia hatua za awali.

Tofauti na Yanga ambao licha ya kuchukua ubingwa msimu wa mwaka 2015/2016 walikuwa wakijitahidi na kutolewa kuanzia robo fainali na nusu fainali. Ila timu zote mbili hazijawahi kuchukua ubingwa huo mara mbili hivyo kama kuna atakayetinga fainali basi itakuwa ni historia nyingine mpya inatengenezwa.

Ubora Mpaka sasa Simba ina kikosi bora ukilinganisha na Yanga ingawa katika mchezo huu hata kama mmoja ni mbovu matokeo yao huwa hayatabiriki. Kwanza kila mmoja humwogopa mwenzake na kucheza kwa presha na hofu kwa mashabiki wao, kila mmoja akipambana apate matokeo mazuri yatakayowanufaisha.

Simba ina kikosi kipana chenye wachezaji wanaojituma mwanzo hadi mwisho bila kukata tamaa. Akitoka mchezaji mwenye ubora anaingia mwingine. Ukitizama safu yao ya ushambuliaji inaongozwa na John Bocco na Meddie Kagere ambao wote wamewahi kuifunga Yanga kwa vipindi tofauti. Siku za karibuni Bocco amekuwa moto wa kuotea mbali akihusika katika ushindi katika baadhi ya mechi zao zilizopita.

Safu ya mabingwa hao wa Ligi Kuu ndio inaongoza kwa kufunga mabao mengi msimu huu yakifika 69 ikiwa ni timu iliyofungwa pia mabao machache 16. Pia, ina viungo wengi wenye ubora wakiongozwa na Cleatous Chama na wengine.

Kwa upande wa Yanga licha ya kusuasua katika baadhi ya mechi zao zilizopita kutokana na upinzani mkali, sio timu ya kubezwa imekuwa ikionyesha soka la kuvutia hasa inapojua inakutana na mtani wake.

Lakini ukweli, Yanga bado kwenye safu ya ushambuliaji haiko vizuri sana wamekuwa wakitengeneza nafasi nyingi lakini umaliziaji mbaya. Siku za karibuni baada ya kukosekana kwa mchezaji wao tegemeo Bernard Morrison mtu waliyekuwa wanamtegemea ni David Molinga.

Lakini hatimaye wamemrejesha kundini mshambuliaji huyo wa Ghana waliyekuwa na matatizo naye hivo anatarajiwa kuwabeba tena kama ilivyokuwa kwenye mechi ya watani iliyopita.

Je, Morrison atafanikiwa kuibeba timu yake? Mchezaji huyo mwenye kasi anasubiriwa kuona kama ataendeleza kile alichokuwa anafanya au atawaliza kwasababu amekuwa akiwasumbua waajiri wake.

Pia, Mohamed Banka aliyekosekana katika baadhi ya mechi zilizopita naye amerejeshwa kundini. Huenda akachezeshwa kwani ni miongoni mwa wachezaji wanaoaminiwa kwenye kikosi hicho.

Katika michezo karibu miwili iliyopita wamekuwa wakiruhusu kuongozwa kwa kufungwa kisha hupambana kurejesha. Safu yao ya ulinzi ni kama iliyumba kidogo hivyo wana kazi ya kurekebisha mapungufu yao la sivyo wanaweza kuadhibiwa na watani zao ambao muda wote huonyesha uchu wa kutaka kufunga.

Makocha Makocha wote wanafahamiana kwasababu walishakutana katika michezo iliyopita ya ligi, wanajua ubora na udhaifu wa timu zao. Kocha wa Simba Sven Vandebroek anazungumzia mchezo huo na kusema hawatabadilisha mfumo, atawatengeneza wachezaji wake kisaikolojia kuhakikisha wanashinda.

Anasema kama watapata ushindi itasaidia kunogesha sherehe zao za ubingwa wa ligi hivyo kwa kutambua na umuhimu wa mchezo huo ni lazima kikosi chake kipambane. Nae Kocha wa Yanga Luc Eymael anasema hawaiangalii Simba bali kutafuta ushindi utakaowapa nafasi ya kusonga mbele na kuwakilisha nchi kimataifa.

Mashabiki Ni kawaida mashabiki wa timu hizi mbili kutambiana kutokana na jinsi wanavyoamini vikosi vyao. Wamekuwa wakicheka kwa matokeo mazuri na kulia kwa matokeo mabaya.

Baada ya dakika 90 za mchezo huo itajulikana ni mashabiki wa timu gani wataondoka na shangwe lakini kubwa wanachotakiwa ni kujiandaa kisaikolojia kwani mechi hii haina matokeo matatu, ni mawili tu kushinda ana kufungwa.

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi

Kila mchezaji wa kigeni mil 4

masaa 3 yaliyopita Rahel Pallangyo

KLABU ya ...

Kila mchezaji wa kigeni mil 4

masaa 3 yaliyopita Rahel Pallangyo

KLABU ya ...

Simba yamuwekea kizuizi Senzo Yanga

masaa 4 yaliyopita Mohammed Mdose

SIKU moja ...