loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ilani ya CCM yawezesha uzalishaji chakula kuimarika

UZALISHAJI wa chakula umeimarika na hivyo kuwezesha nchi kujitosheleza kwa chakula kwa kiwango kikubwa, huku ikiwa na ziada ya maelfu ya tani ndani ya miaka mitano tangu mwaka 2015.

Hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na serikali, ikiwamo kuwezesha mikopo kwa wakulima wadogo na wa kati inayotolewa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), ni sehemu ya hatua za kuboresha sekta na wakulima kama alivyoahidi Rais John Magufuli alipoingia madarakani kwamba hatawaangusha.

Akizungumzia uzalishaji wa mazao ya chakula, Waziri Kilimo, Japhet Hasunga alisema umeendelea kuimarika na hivyo kuwezesha nchi kujitosheleza kwa chakula kwa wastani wa asilimia 121 na kuwa na wastani wa ziada ya tani 2,798,700.6.

Waziri Hasunga alisema mafanikio hayo makubwa yametokana na serikali kutekeleza kikamiilfu Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyoelekeza yafanyike mambo mbalimbali, ikiwamo kuwezesha taifa kujitosheleza kwa chakula tofauti na awali.

Kwa mujibu wa Waziri, chama kupitia ilani yake, kilielekeza serikali kutilia mkazo utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Programu ya Kuendeleza Kilimo (ASDP II) kufikia malengo makuu ya kufanya kilimo kuwa cha kisasa na cha kibiashara; chenye tija na ambacho mazao yake yatakuwa yameongezewa thamani.

Ilani ilisema lengo la kutekeleza programu ni kuhakikisha kuwa taifa linajitosheleza kwa chakula; kuimarisha uchumi; kuongeza kipato cha wakulima; kuwa kichocheo cha kukua kwa viwanda; na kuongeza ajira.

Alisema katika kutekeleza azma hiyo kwa kipindi cha miaka mitano tangu 2015, mafanikio mengine yaliyojitokeza ni upatikanaji wa mbegu bora ambao umeongezeka kutoka tani 36,614.28 mwaka 2015/2016 hadi tani 76,725.52 mwaka 2019/2020 sawa na ongezeko la asilimia 110.

Lipo pia ongezeko la uzalishaji wa ndani wa mbegu bora kutoka tani 20,604.97 mwaka 2015/2016 hadi tani 61,703.72 mwaka 2019/2020 na hivyo kupunguza uingizaji wa mbegu kutoka nje ya nchi kwa asilimia 53.

Serikali imeimarisha upatikanaji wa mbolea kwa kuanzisha mfumo wa ununuzi wa pamoja ambao umewezesha kuongeza upatikanaji wa mbolea kutoka tani 302,482 mwaka 2015/2016 hadi tani 604,978 mwaka 2019/2020 na kuwezesha wakulima kupata mbolea kwa wakati na bei nafuu.

Matumizi ya zana bora za kilimo hususani trekta kubwa na za mkono zinazomilikiwa na wakulima zimeongezeka kutoka 14,200 na 6,348 mwaka 2015/16 hadi 18,088 na 8,883 mwaka 2019/20.

Kwa upande wa kilimo cha umwagiliaji, wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 461,326 mwaka 2015/2016 hadi hekta 694,715 mwaka 2019/2020 sawa na ongezeko la asilimia 33.6.

Katika hotuba ya kufunga Bunge la 11, Juni mwaka huu, Rais Magufuli alisema mwaka 2017 serikali ilizindua ASDP II ambao ni mpango uliolenga kufanya kilimo kiwe cha kisasa, cha kibiashara na chenye tija.

Rais Magufuli alizungumzia namna serikali ilivyoiwezesha Benki ya Maendeleo ya Kilimo kwa kuiongezea mtaji wa Sh milioni 208 ambao ni mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Serikali pia iliipatia benki hiyo Dola za Marekani milioni 25 sawa na Sh bilioni 57.8 kuendesha mfuko wa dhamana kwa wakulima wadogo wenye lengo la kuchagiza benki na taasisi za kifedha kutoa mikopo ya kilimo kwa wakulima wadogo na wa kati.

“Hii ina maana kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, serikali imeipa TADB Sh bilioni 324.8 hivyo kuiwezesha benki kutoa mikopo ya moja kwa moja kwa wakulima, wafugaji na wavuvi yenye thamani ya Sh bil 166.9 kwa riba nafuu,” alisema.

Rais Magufuli aliongeza, “kutokana na hatua hizi, mafanikio makubwa yamepatikana. Mathalani, uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kutoka tani 15,528,820 mwaka 2015/16 hadi tani 16,861,974 mwaka 2018/19. Alisema mahitaji ya tani za chakula kwa mwaka ni chini ya tani milioni 14.

Kwa upande wa mazao ya biashara, uzalishaji umeongezeka kutoka tani 796,502 hadi 1,144,163.1. Wakati akizindua Bunge la 11 mwaka 2015, Rais Magufuli aliwaahidi wakulima kuwa hatawaangusha.

Alisema lengo ni kuimarisha sekta hiyo iweze kutoa mchango katika uchumi wa nchi na wao maisha yao yabadilike. “Nataka niwahakikishie kwamba ahadi zetu kwao tutahakikisha zinatekelezwa,” alisema Magufuli.

KAMPUNI ya uzalishaji wa vifaa mbalimbali vya umeme cha Kilimanjaro ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi