loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Uwazi kutawala kura uteuzi CCM

KIVUMBI cha uteuzi wa wagombea ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) sasa kinahamia kwa wagombea ubunge, udiwani na wawakishili ambapo leo chama hicho kinaanza kutoa fomu za wanaowania nafasi hizo, huku kikitangaza mchakato wa kura za uteuzi utafanyika hadharani.

Pamoja na hayo, chama hicho kimebainisha wazi kuwa kwa mujibu wa kanuni zake za uchaguzi mtu yeyote mwenye cheo zaidi ya kimoja ndani ya chama hicho akigombea na endapo kugombea kwake kutasababisha uhai wa chama hicho kuzorota kwa namna yeyote hatoteuliwa.

Aidha, wagombea na watia nia wote walioandaa mabango na vipeperushi na kusambaza kwenye mitandao ya kijamii wameonywa na kutakiwa kuacha mara moja kusambaza vipeperushi hivyo, kwa kuwa kufanya hivyo ni kosa linalostahili adhabu.

Hayo yalibainishwa mjini Dodoma jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Humphrey Polepole alipozungumza na waandishi wa habari, kuhusu kuanza kwa mchakato wa uteuzi wa wagombea watakaowakilisha chama hicho katika nafasi za ubunge, udiwani na uwakilishi.

Alisema katika moja ya marekebisho ya katiba yaliyopitishwa na Mkutano Mkuu wa chama hicho uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma, suala la uteuzi wa wagombea na upigaji wa kura za maoni za ubunge, udiwani na uwakilishi sasa litafanyika hadharani.

Kura za maoni “Mchakato mzima wa kura za maoni sasa utawekwa hadharani shairi. Masunduku yote ya kura yatawekwa mbele ya wajumbe na wagombea watashiriki kuhesabu…,”

“Tunataka mchakato wa uchaguzi uwe huru, wazi na wa haki. Kama mmejipanga kata na jimbo mko huru kutafuta watu pembeni kuwasimamia katika uchaguzi wenu wa wagombea,” alieleza Polepole.

Alisema pamoja na kwamba kanuni za uchaguzi za chama hicho zinabainisha kuwa ni haki ya mwanachama kugombea nafasi yeyote, lakini pia kanuni hizo zimebainisha sasa wazi kuwa endapo mgombea mwenye nafasi nyingi za uongozi atagombea na kusababisha chama kuzorota, hatoteuliwa.

“Wewe ni mwenyekiti wa kata, ndio mkuu wa siasa wa kata, ndio unayesimamia serikali, ukaona ukagombee, ikiwa kugombea kwako kutazorotesha chama chetu nasema wazi hatutakuteua,”alisisitiza na kuongeza kuwa “Chama chetu uimara wake ni katiba na kanuni tulizojiwekea tukizifuata tuTAkuwa imara,”

Aidha, alifafanua kuwa kanuni za uteuzi wa wagombea uongozi katika vyombo vya dola za chama hicho, pia zinazungumzia makatazo ya vitendo fulani fulani katika uchaguzi. “Matendo hayo yanayozungumziwa kukatazwa na kulalamikiwa ukiyafanya haya utakuwa mtuhumiwa,”

“Sasa wale watuhumiwa wa vitendo havihusiani na rushwa lakini bado wanakiuka na kufanya vitendo kama vile mabango, vipeperushi wale wanaoweka mitandoani kutangaza nia ni kosa, unafanya kampeni unajipitisha,” alisema.

Aidha, alisema matendo kama vile kampeni chafu, vurugu za wapambe, wapigadebe, upotoshaji wa makusudi wa sifa za wagombea wengine nayo ni makossa ambayo yataadhibiwa na kuonywa na kamati ya siasa mara moja.

Mabango marufuku

“Kwa niaba ya CCM ninawaonya mara moja kuacha kutumia mabango na vipeperushi kabla ya mchakato wa uchaguzi, fomu zinatolewa kesho (leo) wewe unatoa mabango mtandaoni tuwe na nidhamu. Wale waliochapa waache mara moja,” alisisitiza na kuzitaka kamati za siasa za maeneo husika kukemea mara moja.

Alisema kanuni hizo pia zinasema ni mwiko kwa kiongozi au mwana CCM yeyote kutoa au kupokea rushwa. Kiongozi au mgombea yeyote akithibitika hatateuliwa. “Nyie toeni rushwa sisi tunafuatilia tumejipanga tangu 2017,”

Alisema jana ndio ilikuwa mwisho wa wabunge wa CCM kuwa wabunge katika majimbo yao ambao leo wako sawa na wagombea wengine na kuitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kutofumbia macho mgombea yeyote atakayejihusisha na rushwa.

Pamoja na hayo, katibu huyo wa uenezi alisema chama hicho kinazuia michango holela katika kipindi hiki cha uchaguzi, na kwamba michango yote lazima ipitishwe na Kamati za siasa na inabaki kuwa ni michango ya hiyari.

“Ni marufuku mwana CCM kulazimishwa kutoa michango labda kwa hiyari yake mwenyewe. Pia, Kamwe mchango usiwe ni kigezo cha kumnyima au kumpa mgombea fomu. Wagombea wapewe fomu sawa na kiwango kilichoainishwa katika kanuni,” alisema.

Alisema kwa mujibu wa kanuni za chama hicho, fomu ya udiwani ngazi ya kata au wadi Zanzibar ni Sh 10,000. Ubunge au uwakilishi Zanzibar ni Sh 100,000.

“Fomu ya mgombea ubunge Bunge la Afrika Mashariki (EALA) ni Sh 100,000, fomu ya Spika ni Sh 500,000 na fomu za urais ni Sh milioni moja,”alisema.

Ratiba ya uchaguzi

Akizungumzia ratiba, alisema kwa nafasi ya ubunge Julai 20-22 itafanyika mikutano mikuu ya CCM ya majimbo au wilaya na wawakilishi na kupiga kura za maoni za wagombea wa ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi. Julai 30, vikao vya kamati za siasa za jimbo vitafanyika ili kuwajadili wagombea na kutoa mapendekezo yake kwa kamati za siasa za wilaya.

Agosti mosi na pili, vikao vya kamati za siasa za wilaya vitakaa kujadili wagombea na kutoa mapendekezo yake kwa kamati za siasa za mikoa.

Agosti 4 hadi 5, vikao vya kamati za siasa za mikoa vitakaa na kujadili wagombea na kutoa maoni yake kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa kwa Tanzania Bara na kwa upande wa Zanzibar watatoa mapendekezo kwa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa Zanzibar.

Vilevile kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi siku ya kuchukua fomu ni sawa na wabunge wa jimbo bara.

Pia tarehe za mikutano ya CCM majimbo au wilaya na vikao vya kamati za siasa majimbo zinafanana na bara. Pia vikao vya kamati za siasa wilaya na vikao vya kamati za siasa za CCM zitafanya vikao vyake sasasawa na bara kati ya Agosti 4 na 5.

Tofauti ipo katika ubunge na ujumbe wa Baraza la wawakilishi viti maalumu ambapo tarehe ya kuchukua fomu na kurudisha inalingana na wabunge lakini wao Julai 23 itafanyika mikutano ya UWT mkoa.

Katika mikutano hiyo itapigwa kura ya maoni kwa wagombea wa viti vya mikoa na makundi mengine isipokuwa kundi la vijana na wazazi. Julai 30 Baraza la Vijana mkoa litapiga kura za maoni kwa wagombea wa viti maalumu wa kundi hilo.

Julai 31 Baraza la Wazazi Mkoa litapiga kura za maoni kwa wagombea wa viti maalumu kundi la wazazi. Kati ya Agosti 4 na 5, kamati za siasa za mikoa zitatoa mapendekezo na kuwasilisha kwenye Baraza Kuu la UWT Taifa.

Agosti 8, Baraza Kuu la Vijana litapiga kura za maoni kwa wagombea wa ubunge na uwakilishi viti maalumu wa kundi hilo. Agosti 9, Baraza Kuu la Wazazi litapiga kura za maoni kwa wagombea wa ubunge na uwakilishi viti maalumu wa kundi hilo.

Agosti 10, Baraza Kuu la UWT litapiga kura za maoni kwa wagombea wa ubunge na uwakilishi viti maalumu na kuandaa mapendekezo ya kuwasilishwa kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa.

Kuhusu udiwani wa kata au wadi, Polepole alisema watachukua fomu tarehe hizo na Julai 27 itafanyika mikutano ya kata au wadi ya kupiga kura ya maoni.

Julai 29, vikao vya kamati za siasa za CCM kata au wadi vitafanyika kujadili wagombea na kutoa mapendekezo kwa kamati za siasa za Jimbo kwa Zanzibar na wilaya Tanzania Bara. Julai 30, vikao vya Kamati za siasa za CCM jimbo Zanzibar vitajadili wagombea na kutoa mapendekezo kwa Kamati za siasa za wilaya. Vilevile vikao vya wilaya vitajadili na kupeleka mapendekezo kamati za siasa mikoa.

Vya mikoa nitapeleka mapendekezo yake Halmashauri Kuu ya Mikoa ambazo zitajadili wagombea ns kufanya uteuzi wa mwisho wa wagombea wa udiwani mmoja katika kila kata na wadi iliyopo mkoani.

Kuhusu udiwani wa viti maalumu, fomu zitachukuliwa Julai 14 na kurudishwa Julai 17 saa 10:00 jioni kwa wagombea wengine. Vikao vyote vitafanyika na kupiga kura za maoni na kupeleka kikao cha juu yake.

Julai 25 mkutano wa UWT wilaya utafanyika kupiga kura za maoni, Agosti 1-2 vikao vya kamari vya wilaya, Agosti 4-5 vikao vya kamati za siasa za CCM mkoa na Agosti 6 vikao vya Halmashauri Kuu za CCM mkoa vitajadili na kufanya uteuzi wa mwisho.

Mfumo kubadilishwa Wakati mchakato huo ukianza, chama hicho kilieleza kubadili mifumo yake hususani mfumo wa kupata wagombea wa ubunge na uwakilishi katika uchaguzi mkuu, baada ya kubaini uliotumika mwaka 2015 ulikuwa na upungufu. Mfumo huo mpya unajumuisha majina ya wagombea kupitia vikao mbalimbali vikiwemo vya kamati ya siasa ya halmashauri kuu ngazi ya jimbo, wilaya, mkoa na sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa kuchuja majina matatu yatakayopigiwa kura.

Aidha, kutakuwa na mchakato wa pili ambapo taarifa hizo zitakwenda makao makuu ya CCM na kuanza mchakato wa kujadili majina hayo yatakayojadiliwa tena na vikao vya awali na kisha Halmashauri Kuu ya Taifa iliyoko chini ya Mwenyekiti, Rais Magufuli itafanya uteuzi wa jina moja la mwana CCM atakayekuwa ameteuliwa kupeperusha bendera ya chama kwenye ubunge.

Akitoa taarifa hivi karibuni wakati Rais Magufuli akirejesha fomu ya kuwania urais kupitia chama hicho, Katbu Mkuu wa CCM Taifa, Dk Bashiru Ally aliwataka watia nia katika majimbo na waende majimboni si kufanya kampeni bali kujipitisha pitisha kwa wagipakura ili kuwaona.

Pia aliwataka waende kwa wasimamizi wa uchaguzi na kuulizia utaratibu wa uchukuaji na urudishaji fomu wakati utakapofika na sasa wakati huo umefika.

Aliwataka wasiende kufanya kampeni, akisema kwamba Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula (mzee wa mafaili) atakuwa akiwafuatilia nyendo zao kama wataanza kampeni kabla ya muda rasmi uliopangwa na wakakaokiuka utaratibu huo watakatwa majina Magufuli aonya makundi Naye, Rais Magufuli wakati akifunga Mkutano Mkuu wa CCM Julai 11, mwaka huu aliwataka wana-CCM kwenda kugombea nafasi hizo na watakaokosa wasiendeleze makundi baada ya uchaguzi.

Rais Magufuli alionya kwamba CCM imekuwa ikipoteza majimbo mengi na wapinzani kushinda katika majimbo na kata kutokana na ukweli kwamba wana CCM huendeleza makundi mara baada ya uchaguzi kwisha.

Wakati dirisha hilo likifunguliwa kumekuwa na kasi kubwa ya wana CCM katika maeneo mbalimbali kutangaza nia ya kugombea kwenye majimbo mbalimbali.

Miongoni mwa watia nia ni watu wa kada tofauti wakiwamo wasomi, viongozi wa dini, waandishi wa habari, wanasheria, wabunge waliomaliza muda wao, mawaziri na watendaji wa serikali. Baadhi yao waliotia nia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Profesa Palamagamba Kabudi aliyetangaza nia ya kuwania jimbo la Kilosa mkoani Morogoro. Kabudi alikuwa ni mbunge wa kuteuliwa na rais.

Katika jimbo hilo pia Mkurugenzi wa Mipango na Sera ya Taasisi ya Kumbukumbu ya Hayati Edward Moringe Sokoine, Edward Tunyon anawania nafasi hiyo ya ubunge.

Wengine ni Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe, Ally Kasinge aliyetangaza nia kugombea ubunge katika jimbo la Kilwa Kusini na Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ni miongoni mwa viongozi wa dini ambaye picha yake imesambaa kwenye mtandao wa kijamii akieleza nia ya kugombea jimbo la Kawe, Dar es Salaam.

Kwa wagombea hao wanatafuta nafasi 384 za bungeni ambapo katika Bunge la 11 kulikuwa na wabunge 275 wa CCM, bila wa kuteliwa na rais, wabunge wa Chadema 70, CUF 42, ACT mmoja, NCCR mmoja na mwanasheria Mkuu wa Serikali hata kama baadaye idadi ya wabunge wa upinzani walipungua baada ya wengi kuhamia CCM.

Takwimu za Tume ya Uchaguzi zinaonesha kwamba katika uchaguzi wa mwaka 2015 kulikuwa na idadi ya majimbo ni 214 Tanzania Bara na 54 Tanzania Visiwani lakini uchaguzi wa mwaka huu majimbo manne ya Zanzibar yamefutwa na kubaki 50.

akwimu za Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) zilizotolewa mwaka 2014 zinaonesha kwamba kuna kuna kata 3,337, zinasimamia vijijini 12,423 na mitaa 3,741 huku vitongoji 64,616. Hivyo idadi ya madiwani wanaotakiwa ni 3,337 kutokana na kata zilizopo nchini. Imeandikwa na Magnus Mahenge, Dodoma na Halima Mlacha Dar.

KATIBU Tawala wa Wilaya ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

1 Comments

  • avatar
    Mwana Msuya
    15/07/2020

    bwana huyu naye anaongeaga utopolo tu kila siku [removed][removed]

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi