loader
Ushindi asilimia 100 CCM, Nyota njema kwa JPM Oktoba

Ushindi asilimia 100 CCM, Nyota njema kwa JPM Oktoba

MWENYEKITI wa CCM, Rais John Magufuli ndiye mgombea urais ambaye atapeperusha bendera ya CCM akishindana na wagombea wa upinzani ambao wengi wakati makala haya yanaandikwa walikuwa bado kwenye mchakato wa kumtafuta.

Mwishoni mwa wiki iliyoishia Julai 11, mwaka huu, Mkutano Mkuu wa CCM, ulimpitisha Rais Magufuli kuwa mgombea wa chama hicho kwa kumpa kura zote 1822, sawa na asilimia 100 bila kuwepo ya kuharibika na kura ya hapana.

Ushindi huo wa Magufuli ndani ya chama, umempa faraja naye akalithibitisha hilo wakati wa kufunga mkutano huo kwamba hakutegemea kupata kura asilimia 100, kitendo kinachoonesha wana-CCM wana imani naye.

Inaelezwa kwamba ushindi huo wa asilimia 100 haukuonekana wakati wakigombea kwa mara ya pili, Marais wastaafu Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete huku wakiwa wagombea pekee katika vipindi vyao.

Magufuli pia amepata uungwaji mkono wa aina yake wakati akitafuta wadhamini ambapo zaidi ya Watanzania milioni 1.1 walijitokeza kumdhamini, huku akiacha malalamiko kwa baadhi ya wajumbe waliotaka kumdhamini lakini fomu hazikutosha.

Ushindi huo ni nyota nyema kwa chama hicho na dalili njema, hata kama yeye mwenyewe anasema, wana-CCM wanatakiwa kujiandaa kwenda kunadi sera za chama, hata kama hawatapata ushindi wa asilimia 100 katika uchaguzi mkuu Oktoba 25, mwaka huu.

Katika uchaguzi wa mwaka 2015 ambao ni dhahiri sura ya CCM mbele ya Watanzania ilikuwa imeshuka kiasi, Dk Magufuli aliibuka mshindi kwa kupata asilimia 58 ya kura huku msjindani wake wa karibu aliyegombea kupitia upinzani, Edward Lowassa, akipata kura asilimia 39.

Lakini swali la kujiuliza ni hili. Kwa nini Magufuli amepigiwa kura zote za ndiyo na wajumbe wote wa Mkutano Mkuu wa CCM? Kuna sababu nyingi? Wajumbe na viongozi waliopewa fursa ya kuzungumza katika Mkutano huo Mkuu wa CCM Julai 11, 2020, waliweka wazi bila kumung’unya maneno kwamba kazi alizofanya zinamtambulisha bayana kwamba taifa bado linamhitaji kukamilisha mengi aliyoyaanzisha.

Rais mstaafu wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi anasema amefanya mambo mengi na kutekeleza miradi ambayo wakati wa uongozi wake na wengine waliofuatia ilishindikana.

Mwinyi ametaja miradi michache kama vile ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na mradi wa Umeme wa Julius Nyerere katika Bonde la Rufiji akasema kutokana na mradi huo Tanzania itakuwa bepari wa umeme kwa maana itakuwa na umeme mwingi wa kutosha na hata kuuza nje ya nchi.

Naye Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa alisema hakuna ubishi tangu Rais Mafuguli ameshika madaraka amefanya mambo mengi makubwa na hasa kurudisha nidhamu ya kazi katika sekta ya umma.

Lowassa ambaye alikuwa mgombea mwenzake katika uchaguzi wa 2015 kwa tiketi ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) uliounganisha vyama kadhaa na kuibuka akiwa mshindi wa pili, amemwomba Rais Mabasi aendelee kuchapa kazi na ‘kufinya’ zaidi ili kudumisha nidha kwa wanaokiuka maadili ya kazi.

Katibu Mkuu wa CCM mstaafu, Abdulrahman Kinana ambaye katika Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM alisamehewa adhabu aliyopewa na chama na ametumikia miezi minne tu, aliwaomba wajumbe wa mkutano huo kumpigia kura zote Rais Magufuli na isiwepo kura ya hapana ili Rais Magufuli apate faraja ya kuendelea kuchapa kazi katika kutekeleza miradi ya maendeleo nchini, ushauri ambao waliutekeleza.

Kinana pia aliwaonya wana CCM kwamba hakuna uchaguzi mwepesi, hivyo akawaka kushikamana wote na kufanya bidii katika kutafuta kura za rais, wabunge na madiwani ili chama kishinde na pia kuwataka wageuke makundi baada ya kura za maoni.

Kinana pia anaungana na wote wanaosema kwamba mambo aliyofanya Rais Magufuli tangu ameingia madarakani yanajieleza yenyewe na hiyo ana hakika atashinda na anamtakia heri nyingi katika kutafuta kura ili ashinde kwa kishindo.

Kwa lugha nyingine, Kinana anasema ushindi kwa Magufuli katika uvchaguzi wa Oktaba siyo suala la kujadili, bali ukubwa wa ushindi ndicho kitu kinachopasawa kufanyiwa kazi Kwa upande wake, Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya anampongeza Rais Magufuli kwa kuingiza nchi katika Uchumi kwa Kati kabla ya mwaka 2025, hivyo anawaomba wajumbe wa Mkutano Mkuu wakirudidi majimbo kumchagulia wabunge na madiwani bora ili kumsaidia katika kuchapa kazi.

Mwenyekiti wa chama cha upinzani cha Tanzania Labour Party (TLP), Augustino Mrema anasema chama hicho kimeamua kumuunga kumuunga mkono Rais Magufuli na hivyo hakitasimamisha mgombea kwani anatosha kutokana na utendaji wake bora.

Anaahidi kwamba watafanya kampeni nchi nzima kumpigia debe Magufuli ili achaguliwe kwa kura nyingi. Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba anapomngeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri anazofanya na hasa kuingiza nchi katika uchumi wa kati, lakini anaomba wakati wa kampeni zitakapofika basi zifanyike kwa ustaarabu na usawa. Profesa Lipumba anasema wapo tayari kushiriki katika uchaguzi na kwamba agenda ya katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu ni: “Furaha kwa Watanzania inawezekana.”

Naye mwanachama wa CCM, Sofia Simba anasema Rais Magufuli amepata mafanikio mengi kupitia ujenzi wa miradi nchini hasa ya maji na afya ambayo kwa kiasi kikubwa inawa- nufaisha wan- awake.

Hivyo, Sofia anamshukuru Rais Magufuli na hivyo anaahidi kwamba ili aendelee kujenga miradi ya kuwanufaisha wanawake, yeye na wanawake wenzake nchi nzima watamuunga mkono kwa kumpa kura nyingi na za kutosha.

Aliyekuwa Mbunge wa Momba kwa tiketi ya Chadema na kuhamia CCM, David Silinde anasema Magufuli amefanya mambo makubwa kwa kutekeleza miradi mingi nchini na hata jimboni kwake. Silinde anasema Rais Magufuli amethubutu na kutekeleza ahadi za Ilani ya CCM 2015 kwa vitendo, akaahidi kwamba atazunguka naye nchi nzima kutangaza mazuri hayo.

“Asante Rais Magufuli kwa kusambaza umeme vijijini, asante kwa kuhamishia makao makuu ya Serikali Dodoma, asante kwa kuondoa rushwa, asanate kwa kuongeza uwajibikaji serikalini, asante kwa kujenga flyover jijini Dar es Salaam,” anasema Silinde.

Silinde anasema hivi sasa Tanzania inaheshimika mbele ya mataifa mengi duniani hasa kwa kitendo cha kuivusha nchi kutoka nchi masikini hadi ya uchumi wa kati. Aliyekuwa Katibu wa Chadema kwa miaka miwili hivi, Dk Visenti Mashinji naye anasifia maendeleo makubwa yanayofanywa na Magufuli katika kipindi cha miaka mitano.

Anasema hajaona chama kingine ambacho kinaweza kufanya maendeleo makubwa kama hayo. Mama Getrude Mongela ambaye aliwahi kuwa mwenyekiti wa Mkutano wa Wanawake duniani uliofanyika Beijing, China anawataka wanawake kumuunga mkono Magufuli ili kupeleka mbele Tanzania na kushikana bega kwa bega naye kama walivyofanya wakati wa kupigania uhuru.

Mongela anasema wanawake wapo pamoja na Rais Magufuli na ana baraka zote za wanawake nchini na watampa kura nyingi za kung’ara. Kazi alizofanya Rais Magufuli ambazo viongozi mbalimbali wamethibitisha zinambeba na zinamhakikishia kwamba atashinda kwa kishindo kwa kweli ni nyingi hata zilizotamkwa na wajumbewa mkutano mkuu na hata yeye mwenyewe Magufuli wakati wa ufunguzi wa mkutano huo ni chache tu.

Mpaka makala haya yaanandikwa, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilikuwa hakijatangaza mgombea wake lakini majina ya watia nia walikuwa takribani 11 huku majina makubwa yakiwa Tundu Lissu, Freeman Mbowe, Lazaro Nyalandu na Peter Msigwa.

Juzi pia mitandao ya kijamii ilimwonesha Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani, Benard Membe aliyefukuzwa CCM akiwa pamoja na viongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, hatua inayoonesha kwamba pengine ndiye atasimamishwa na chama hicho kupambana na Magufuli.

Hivi karibuni akizungumza na BBC, Membe alisema yuko tayari kwenda upinzani lakini akawa anataka vyama hivyo viungane kuweka mgombea mmoja.

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi