loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ulaji wa samaki ulivyo na faida mwilini

KUNA usemi kwamba, mwili wako usipoupatia lishe bora, basi jiandae kuupa mbadala ambao ni dawa nyingi! Lishe bora maana yake ni kuupa mwili vyakula vyenye kujumuisha makundi yote ya vyakula kama vile protini, wanga, vitamini, madini, nyuzi lishe na maji.

Kimsingi namna mwanadamu anavyozingatia lishe bora, ndivyo anavyoweza kujizuia kupata maradhi mbalimbali. Moja ya vyakula hivi bora kwa afya ya mwanadamu ni samaki.

Ingawa wengi hutumia samaki kama kitoweo lakini ni wachache wanaofahamu umuhimu wa chakula hicho katika afya ya mwanadamu. Wataalamu wa tiba na lishe wanaeleza kuwa, samaki wana mafuta yenye kiambata aina ya Omega 3 chenye faida kubwa kwa mwili na hivyo kwa maisha ya binadamu.

Kiambata hiki kinamwezesha mlaji wa samaki wa mara kwa mara kuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri, kutunza kumbukumbu, kutibu matatizo ya kukosa usingizi, kuishi kwa muda mrefu na kusaidia mfumo wa ubongo na neva.

Hali kadhalika wataalamu wanasema samaki pia huweza kuimarisha uwezo wa mtu kuona na kuimarisha nuru ya macho, mwili kupata nguvu pamoja na kinga ya kukabiliana na baadhi ya magonjwa.

Uchunguzi uliofanywa na watafiti wa Chuo Kikuu cha Kuopio nchini Finland umebaini kuwa samaki husaidia pia katika kutibu maradhi mengi kama vile shinikizo la damu, baridi yabisi, homa ya mapafu, maumivu makali ya kichwa na pumu.

Watafiti hao wanasema kula samaki mara mbili kwa wiki, hupunguza kwa asilimia 37 uwezekano wa kupata ugonjwa wa msongo wa mawazo na kumpunguzia mtu asilimia 43 fikra za kujidhuru.

Katika utafiti mwingine uliofanyiwa watu 265,000 nchini Japan kwa muda wa miaka 17, ilithibitika kuwa, hatari ya kujiua miongoni mwa wanaotumia samaki kila siku ni ndogo ikilinganishwa na wale wasiotumia samaki.

Watafiti wa Kitivo cha Tiba cha Chuo Kikuu cha Harvard, Marekani, wanaamini kuwa watu wanaoishi katika visiwa na ambao hutumia samaki mara kwa mara katika kitoweo chao huwa wamesalimika pakubwa na hatari ya kupata tatizo la kiakili la hofu iliyopitiliza.

Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, wataalamu wa akili wanasema ili kuondoa matatizo mbalimbali ya kiakili kama vile msongo wa mawazo, hofu, iliyopitiliza, fikra za kujidhuru na nyinginezo watu wote wanashauriwa kutumia samaki au mafuta ya samaki mara kwa mara.

Kwa kutambua umuhimu na faida ya ulaji samaki, Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Nazael Madalla anaeleza juu ya faida hiyo hasa ulaji wa samaki wabichi mara kwa mara baada ya kuvuliwa.

Dk Madalla anasema tafiti zimeonesha samaki wana virutubisho vingi ambavyo ni pamoja na vitamini A, vitamini D, vitamini B12, iron, zinc, calcium, iodine, omega 3 fatty acids, protini na selenium. Anasema kuwa, miongoni mwa faida kubwa ya ulaji samaki wabichi mara kwa mara baada ya kuvuliwa ni kuzuia udumavu na matatizo mengine ya lishe kwa binadamu hususani miongoni mwa watoto.

Dk Madalla, anasema samaki anapoliwa mara tu baada ya kuvuliwa huwa ana virutibisho vingi kwa manufaa ya mwili wa binadamu.

“Ni ukweli kuwa ulaji wa samaki angalau mara moja kwa wiki hususani kwa watoto unachangia kuwa na uwezo mkubwa darasani kutokana na uwepo wa virutubisho vya ‘omega 3 fatty acids,” Dk Madalla anasema.

Tafiti mbalimbali zinaonesha kwamba watu wanaoishi maeneo ya pembezoni mwa bahari, maziwa na mito mikubwa na hivyo mlo wao mkubwa kuwa samaki wamekuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri na akili nyingi.

Na pia wamekuwa wakiishi kwa muda mrefu kutokana na kutokuzeeka mapema. Dk Madalla, anasema wingi wa madini ya chuma katika samaki una faida kubwa kwa wajawazito katika kuzuia upungufu wa damu, na virutubisho vingine vinavyopatikana kwenye samaki ni muhimu pia kwa ukuaji sahihi wa mimba.

“Ninashauri Watanzania tule samaki angalau mara moja kwa wiki ili kuweza kupata lishe bora kutokana na wingi wa virutubisho katika samaki,” anasema Dk Madalla.

Anasema ili kuongeza upatikanaji wa samaki nchini, wananchi wanashauriwa pia kufuga samaki katika mabwawa, matangi na hata majaruba ya mpunga, kwani ufugaji wa samaki pia ni chanzo cha kipato na ajira.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Rashid Tamatamah (sekta ya uvuvi) anasema licha ya mikakati inayochukuliwa kukuza sekta ya uvuvi na Tanzania kubarikiwa kuwa na bahari, maziwa na mito, bado ulaji samaki kwa wananchi umekuwa wastani kilo 8.2 kwa mtu mmoja kwa mwaka.

Katibu Mkuu aliyasema hayo wakati wa ziara ya makatibu wakuu na naibu makatibu walipotembelea mradi wa ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere wilayani Rufiji, mkoani Pwani. Dk Tamatamah, anasema ulaji huu ni tofauti na kiwango kilichowekwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) la ulaji kilo 20 kwa kila mtu mmoja kwa mwaka.

“Ili kufikia kiwango hiki, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeweka mkakati kwamba katika miaka minne hadi mitano ijayo kuhakikisha ulaji wa samaki unaongezeka kufikia kilo 10 kwa mtu mmoja kwa mwaka,” anasema Dk Tamatamah.

Anaongeza: “Ukichukulia wastani kwa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara ni kama kilo 10 za samaki kwa kila mtu mmoja kwa mwaka kiwango ambacho ni cha chini sana,” anabainisha Dk Tamatamah.

Dk Tamatamah anasema sekta ya uvuvi itafaidika na kujengwa kwa Bwawa la Nyerere kwani licha ya kuongeza kiwango cha upatikanaji wa umeme wa kutosha, litatoa fursa kubwa kwa walaji wa samaki kutokana na kuongezeka kwa samaki.

Dk Tamatamah pia anaeleza kuwa kwa sasa uzalishaji wa samaki nchini umefikia tani 448,000 na endapo utaongezeka kufikia tani 700,000 kuna uwezekano mkubwa ulaji wa samaki kwa kila mtu mmoja ukaongezeka kufikia au kukaribia lengo lililowekwa na FAO.

Anasema kufikiwa kwa lengo hilo kunachangiwa pia na mkakati mwingine uliochukuliwa kwenye Ziwa Victoria ni wa kusimamia na kukomesha uvuvi haramu. Dk Tamatamah anasema hatua hiyo imewezesha samaki wameanza kuongezeka na watu wengi wameingia katika ufugaji wa samaki.

Kwa kutambua umuhimu wa kipekee wa sekta ya uvuvi nchini, Serikali ya Awamu ya Tano ya chini ya Rais Dk John Magufuli imeweka mkakati maalumu wa kukuza uchumi na hasa uchumi wa viwanda. Sekta ya uvuvi ni miongoni mwa sehemu ya mkakati huo ukiwa na lengo la kuwezesha upatikanaji wa samaki kwa wingi kwa matumizi ya ndani na wengine kuuzwa nje ya nchi na Taifa kujipatia fedha za kigeni.

Dk Madalla anasema Wizara ya Mifugo na Uvuvi imefanya maboresho ya mazingira katika sekta ya uvuvi iliyosababisha ongezeko la wavuvi wapatao 202,000 ambao wameajiriwa moja kwa moja kwenye sekta hiyo.

Anasema mafaniko hayo yametokana usimamizi mzuri wa sera, sheria, kanuni, miongozo na taratibu mbalimbali. Kutokana na ongezeko la wavuvi katika sekta hii imezalisha zaidi ya watanzania milioni 4.5 kuendelea kupata kipato cha kila siku kutokana na shughuli zinazohusiana na sekta ya uvuvi.

Anasema mapato hayo yanatokana na kuwepo kwa biashara ya samaki na mazao yake, kuunda na kutengeneza boti, kuuza na kushona nyavu na ukuzaji viumbe maji. Licha ya mikakati inayochukuliwa kukuza sekta ya uvuvi na Tanzania kubarikiwa kuwa na bahari, maziwa na mito, bado ulaji samaki kwa wananchi umekuwa wastani kilo 8.2 kwa mtu mmoja kwa mwaka.

Kwa upande wake Dk Tamatamah anabainisha kuwa hivi sasa kwenye vijiji vingi watu wanakula dagaa waliokaushwa na samaki waliokaushwa pia. Lakini anasema kwa kuongeza maghala na umeme kupatikana sehemu nyingi nchini itasaidia uongezekaji wa walaji wa samaki na hivyo kufikia kiwango cha FAO.

Anasema wakati wizara ipo kwenye mikakati endelevu ya kuona upatikanaji wa samaki unakuwa wa kutosha nchini, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza ICE kinatamani kuona watanzania wanajitosheleza kupata kitoweo cha samaki.

Profesa Sebastian Chenyambuga kutoka Idara ya Sayansi za Wanyama, Ufugaji wa Viumbe Majini na Nyanda za Malisho, anawashauri wadau mbalimbali wanaopata mafunzo ya ufugaji samaki kutumia mbinu bora za ufugaji.

SIGARA ina kemikali zaidi ya 4,000 ...

foto
Mwandishi: John Nditi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi