loader
Dstv Habarileo  Mobile
Mwili wa Mkapa kuagwa kesho Dar, kuzikwa Lupaso

Mwili wa Mkapa kuagwa kesho Dar, kuzikwa Lupaso

MWILI wa Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa unatarajiwa kuagwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kuanzia kesho hadi Jumanne huku serikali ikitoa fursa kwa wananchi wote kuaga mwili kabla ya kuzikwa kijiji kwake Lupaso, Mtwara.

Kifo cha Mkapa kilitangazwa juzi na Rais John Magufuli na ametangaza siku saba za maombolezo ya kitaifa kuanzia jana. Bendera zote zitapepea nusu mlingoti huku. Rais aliomba Watanzania kuendelea kuwa watulivu, wastahimilivu na wamoja katika kipindi hiki kigumu cha majonzi ya kuondokewa na mpendwa wao.

Akitangaza ratiba ya mazishi jana nyumbani kwake jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema pamoja na kamati ya mazishi ya kitaifa kuendelea na shughuli ya maandalizi, Mkapa atazikwa kijijini kwake Alhamisi ijayo.

Alisema wanaendelea kupokea waombolezaji nyumbani kwa mjane Mama Anna Mkapa, jijini Dar es Salaam wanaofika kutoa salamu za pole. Alisema fursa kwa watanzania kuaga mwili wa Mkapa, itatolewa kuanzia kesho hadi Jumanne katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam .

“Fursa itatolewa kwa watanzania wote kuaga mwili wa Rais mstaafu Mkapa, tutaanza kuaga Jumapili Julai 26 , 2020 kwenye uwanja wa Uhuru na tutaaga kwa siku tatu mfululizo ikibidi hadi usiku mpaka Jumanne Julai 28, mwaka huu,”alisema.

Aidha Jumanne itakuwa siku ya kitaifa kuaga na misa itaongozwa na Kanisa Katoliki nchini na viongozi wa kitaifa na wa dini, wataongoza kuaga kisha fursa itatolewa kwa wananchi wa Dar es Salaam na wengine watakaohudhuria.

“Tunawakaribisha watumishi wote wa umma kwenda kuaga mwili wa Rais mstaafu Mkapa hiyo Jumanne, kisha wakimaliza watarejea kwenye maeneo yao ya kazi na mwili utasafirishwa mchana huo kwenda Lupaso na Jumatano mwili utaagwa kijijini huko na baadaye mchana yatafanyika maziko,”alisema Majaliwa.

Alisema kwa abiria watakaopenda kutumia usafiri wa anga, kutakuwa na ndege zitakazotua kwenye viwanja vya ndege vya Mtwara na Nachingwea .

“Hivyo Watanzania wanaotaka kwenda kuzika wanaweza kusafiri kwa ndege au mabasi au usafiri binafsi na hata viongozi wa mataifa mbalimbali ambao watapenda kushiriki msiba huu wanakaribishwa na taarifa zao nchi itazipata kupitia balozi zao hapa nchini ili kuyatarisha uwepo wao,”alisema.

Awali, Majaliwa alisema kamati ya mazishi ya serikali inaendelea na maandalizi ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na viongozi kutoka katika nchi marafiki ambao Rais mstaafu Mkapa alifanya nao kazi ili kutoa fursa ya kushiriki.

Wakati huo huo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikwenda kusaini kitabu cha maombolezo na kutoa pole kwa familia kwa niaba ya Rais John Magufuli pamoja na serikali.

Akiwa nyumbani kwa marehemu Masaki, jijini Dar es Salaam aliwasihi wanafamilia na watanzania kwa ujumla, waendelee kumuombea marehemu kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu yote ni mapenzi yake. Kwa upande wake, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alisema kifo hicho ni pigo kubwa kwa taifa.

“Tutamkumbuka daima kwa mchango wake kwa taifa letu kwenye nyanja za siasa; uchumi, diplomasia na jamii,” alisema.

Kutokana na msiba huu wa kitaifa, uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam umeahirisha duru ya kwanza ya Mahafali ya 50.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa William Anangisye ilisema kuwa mahafali hayo yalikuwa yafanyike jana .

Pia Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania (NDC) kilichopo Kunduchi, kimeahirisha hafla ya kufunga kozi ya nane ya NDC-2019/20 zilizokuwa zifanyike leo kutokana na msiba huo. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ndiye alipaswa kuwa mgeni rasmi.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi