loader
Dstv Habarileo  Mobile
Kikwete aeleza walivyozungumza na Mkapa saa chache kabla ya kifo

Kikwete aeleza walivyozungumza na Mkapa saa chache kabla ya kifo

“NINGEJUA Mzee Mkapa anakufa, tungeagana kabisa jana kwa sababu nilikwenda jioni kumuona hospitali tulizungumza sana, alikuwa na maumivu lakini siyo yale maumivu ambayo ukitoka kumuangalia mgonjwa unawaambia wenzako ehee, nimemuona mgonjwa lakinii!!, alikuwa na maumivu ya kawaida sana.”

Ni kauli ya maombolezo ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete (JK) wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kifo cha Rais mstaafu Benjamin Mkapa kilichotokea juzi usiku.

Kikwete ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi wengi waliofika nyumbani jana kumpa pole mjane, Mama Anna, alisema baada ya kufika hospitalini alikokuwa amelazwa, walizungumza kwa takribani saa nzima na katika kuangana, alimwambia angerudi kesho yake (jana).

Rais mstaafu Kikwete alisema baada ya kumuona Rais mstaafu Mkapa alizungumza naye kwa karibu saa moja na hakuwa mgonjwa mahututi bali alihisi maumivu, lakini ya kawaida na kisha wakaagana na kuahidi jana angerudi kumsalimia tena.

“Tuliongea mengi sana, tukaagana na leo (jana) nikaahidi nitarudi tena kumjulia hali, hakuwa mgonjwa kihivyo, sasa zile taarifa za usiku za Rais Magufuli kwamba Mzee Mkapa hatunaye tena, zilinishitua, nikasema, kumetokea nini tena kwa sababu hakuwa mgonjwa sana, na ahadi yangu kwake ilikuwa leo(jana) nikienda atoke hospitalini , nikamwambia kesho(jana) kwa hali yako ningependa nije kukusalimia ukiwa nyumbani kwa kuwa siyo wa kuendelea kukaa hospitalini ,” alisema Kikwete. A

lisema hana la kusema kuhusu kifo hicho, kwani ni siri kubwa na kama angejua wangeagana kabisa. Lakini walipatana wangekutana waendelee na mazungumzo yao. Akizungumzia mchango wa Rais Mstaafu Mkapa, Kikwete alisema taifa limempoteza mmoja wa viongozi wakubwa wa taifa na mashuhuri aliyetumikia taifa kwa uadilifu na heshima.

Aliwataka Watanzania kuendelea kuomboleza na kuwa na moyo wa subira, wakikubali kwamba kifo kimeumbwa na Mungu na wote watarejea kwa aliyewaumba. “Tuendelee kuiombea familia yake na tuishi kwa kusimamia mema na yale mazuri aliyoyaacha kwa mustakabali wa taifa letu,” alisema Kikwete.

Kwa upande wake, aliyekuwa Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Rais Mkapa, Maura Mwingira amemweleza kwamba alikuwa ni zaidi ya kiongozi, akiwapenda watu na alikuwa mtu wa kusamehe.

“Kwa ufupi, namshukuru sana Rais Mkapa kwa sababu aliniamini na kuniteua nikiwa ni mwanamke wa kwanza tangu Uhuru kushika nafasi hiyo…na hii ilifungua milango kwa wanawake wengine kuteuliwa katika nafasi hizo kwa Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Rais wa Zanzibar,” alisema Maura aliyekaa ikulu hadi Desemba 2007.

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi