loader
Dstv Habarileo  Mobile
Nchi nne EAC zaomboleza kifo cha Mkapa

Nchi nne EAC zaomboleza kifo cha Mkapa

NCHI nne za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Kenya, Burundi, Uganda na Rwanda zimetangaza maombolezo ya siku tatu na bendera kushushwa nusu mlingoti kutokana na kifo cha Rais mstaafu wa serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa (81) kilichotokea Ijumaa.

Mkapa alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kuanzia mwaka 1995 hadi 2005. Alifariki dunia hospitalini Dar es Salaam usiku wa Julai 24. Kenya baada ya tu ya Rais John Magufuli kutangaza kifo cha rais huyo mstaafu, nayo asubuhi ilitangaza maombolezo ya siku tatu.

Rais wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta alisema maombolezo hayo ni heshima kwa hayati Mkapa kumshukuru kwa utumishi uliotukuka.

“Alikuwa Rais mwenye hekima, busara na akili aliyejitolea maisha yake kutumikia taifa lake kwa hadhi, heshima na weledi,” alisema Rais Uhuru Kenyatta.

Uganda, kupitia ukurasa wake wa Twitter, Rais wa nchi hiyo, Yoweri Museveni alitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya wananchi wa Uganda, kwa mke wa Mkapa, Anna Mkapa na Watanzania kwa ujumla kutokana na msiba huo.

Alisema kutokana na msiba huo mzito nchi hiyo itakuwa kwenye maombolezo kwa siku tatu na bendera kushushwa nusu mlingoti ikiwa ni ishara ya kuenzi maisha ya kiongozi huyo.

Rais Museveni alisema Mkapa alikuwa kaka yake waliyefanya naye kazi tangu mwaka 1967 wakiwa wanafunzi ambapo pia Mkapa alikuwa ni Mhariri Mkuu wa gazeti la Nationalist.

“Wakati (Mkapa) alipokuwa Rais wa Tanzania, tulifanya naye kazi kwa pamoja kwa ushirikiano kuunganisha Jumuiya ya Afrika Mashariki. Afrika imempoteza mtu muhimu.

Namuomba Mungu roho yake ipumzike kwa amani,” alisema Museveni katika rambirambi zake. Nchini Rwanda, Rais Paul Kagame, alitangaza pia siku tatu za maombolezo kuanzia leo kuomboleza kifo cha Rais Mstaafu Mkapa.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya Waziri Mkuu Rwanda, wakati wa maombolezo hayo, bendera ya taifa ya nchi hiyo na ile ya Jumuiya ya Afrika Mashariki zitapepea nusu mlingoti.

Mwishoni mwa wiki Rais Kagame aliagiza nchi hiyo iungane na wananchi wa Tanzania kuomboleza kifo cha Mkapa hadi keshokutwa ambapo pia ni siku ya maziko ya kiongozi huyo.

Baada ya kutolewa taarifa za kifo cha Mkapa, Rais Kagame alieleza kuwa hisia za kifo hicho zitaligusa bara zima la Afrika. “Tumesikitishwa na kifo cha Rais Mstaafu Mkapa. Natoa pole kwa familia na wananchi wa Tanzania na rafiki yangu Rais Magufuli,” alisema Kagame.

Alisema kifo cha Mkapa kimegusa bara zima la Afrika kwani alikuwa ni mzalendo ambaye mchango wake haukuishia tu nchini kwake Tanzania bali ulivuka mipaka ya nchi hiyo.

Alisema akiwa Rais na baada ya kumaliza kipindi chake cha urais Mkapa aliongoza vikao mbalimbali vya upatanishi ndani ya Afrika. Aidha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi, Balozi Albert Shingiro alitangaza nchi hiyo pia kuanza maombolezo leo na kushusha bendera nusu mlingoti hadi keshokutwa ikiwa ni ishara ya urafiki na umoja baina ya nchi hiyo na Tanzania kipindi hiki cha msiba huo mzito.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi