loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Umeondoka, tunashukuru umetuachia kitabu

KUFARIKI dunia kwa Rais wa Awamu ya Tatu ya uongozi wa Tanzania, Benjamini Mkapa kumewashitua watanzania wengi ambao walimwona mapema mwezi huu akiwa na afya njema alipohudhuria kwenye msiba wa Balozi Job Lusinde.

Je, Ben Mkapa alikuwa mtu wa aina gani?

Hivi ndivyo baadhi ya viongozi mbalimbali nchini waliofika nyumbani kwake jijini Dar es Salaam kuhani msiba wake wanavyomzungumzia huku wakishauri Watanzania kusoma kitabu chake ili kumjua vyema.

ALIWEKA NCHI YAKE MBELE:

Kate Kamba, Mwenyekiti huyo wa CCM mkoa wa Dar es Salaam anasema Mkapa alikuwa kaka yake, rafiki na mshauri wake.

Mwenyekiti huyo anasema alipokuwa mbunge wa Masasi katika kipindi cha mwaka 1980 hadi mwaka 1985, alimpokea Mkapa alipoamua kuja kugombea ubunge jimboni humo mwaka 1985.

“Tulishirikiana vyema na kwa karibu… Ninachoweza kusema siku zote aliweka nchi yake mbele,” anasema.

Anasema aliimarisha uchumi, aliwezesha kurudi kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, alianzisha miradi mbalimbali, yote ikilenga kuwakomboa Watanzania kiuchumi.

Anasema Mkapa alikuwa mzalendo aliyewajali Watanzania na hakuwa na ubaguzi wa ina yoyote.

ALIPENDA KUSAIDIA JAMII:

Anne Makinda, Spika wa zamani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anasema kwamba Mkapa ambaye alifanya kazi kwa muda mrefu na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, alijifunza mengi kutoka kwa Mwalimu hususani uzalendo kwa nchi yake na Afrika kwa ujumla na kupenda kusaidia jamii.

“Viongozi vijana wanalo la kujifunza.

Mimi nawashauri wajifunze mambo kabla ya kuingia kwenye uongozi, waache mihemuko, wawe na utulivu,” anasema.

Anasema hata yeye alipotoka masomoni na kupewa uongozi, kwa kipindi cha miezi sita alikuwa anasoma na kuifunza.

ALIKUWA MKWELI, MWAZI: 

Fredrick Sumaye, Waziri Mkuu Mstaafu anasema Mkapa alitekeleza mambo kwa ukweli na uwazi.

“Mimi nilikuwa waziri wake mkuu katika kipindi chote cha utawala wa wake. Mkapa hakutaka mambo ya kificho, kila kitu kilikuwa wazi ili wananchi waelewe nini kimefanywa na serikali yao na nini kimefanikiwa na nini kimefeli.

“Alileta mabadiliko makubwa nchini kwani katika kipindi chake ndio wakati sura ya uendeshaji wa taasisi nyingi kibiashara nchini zilianzishwa na nchi ikabadilika.

“Tulikuwa tunatoka kwenye biashara iliyohodhiwa na serikali na kuingia kwenye biashara huria na marekebisho yaliyofanyika yakavutia sana wawekezaji,”

Anataja baadhi ya mambo alioanzisha Mkapa na hadi leo yana tija kubwa kwa taifa kuwa ni pamoja na kuanzisha mamlaka kadhaa kama ile ya mapato (TRA), mamlaka ya usafiri wa nchi kavu na majini (Sumatra na sasa Latra) na kadhalika.

Kuhusu huduma za jamii anasema Mkapa alianzisha Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) akiamini kwamba bila wananchi kuwa na elimu bora ilikuwa vigumu kupata viongozi wazuri wa baadaye.

“Tulianzia shule ya msingi na tulipoanza mwaka wa kwanza upande wa sekondario muda wake wa uongozi ukawa umeisha,” anasema Sumaye.

Anasema Mkapa pia aliboresha sana huduma za afya ikiwa ni pamoja na kuhakikisha hospitali zote kuanzia za wilaya zinakuwa na X-ray na vifaa vya maabara.

“Alihakikisha walimu wanafundishwa na alihakikisha vifaa vya elimu vinaongezeka mashuleni,” anasema Sumaye na kuongeza kwamba uongozi wao pia ulihakikisha unaongeza madawati ya kutosha mashuleni.

WAGOMBEA SOMENI KITABU CHAKE:

Profesa Lipumba, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), anasema: “Nilipokuwa msaidizi wa Rais Ali Hassan Mwinyi katika masuala ya uchumi, nilimfahamu Mkapa akiwa waziri lakini pia nilishiriki naye kugombea urais wa Tanzania nikiwakilisha chama changu cha CUF.

“Tuliingia naye kwenye mdahalo lakini hatimaye yeye alichaguliwa kuwa rais,” anasema.

Anamshukuru kwa kuunda Tume ya Brigedia Hashim Mbita kuchunguza kuhusu kilichojiri Zanzibar baada ya machafuko yaliofuatia uchaguzi wa mwaka 2000.

Lipumba anamshukuru pia kwa kuanzisha hatua za kukaribisha wapinzani Ikulu kuzungumza nao na pia wageni waliotembelea Tanzania alikuwa pia akiwakaribisha wapinzani kukutana nao.

“Ninaomba sana wote tunaogombea urais wa nchi yetu tusome kitabu chake,” anasema.

ALIJENGA MISINGI INAYOTUNUFAISHA LEO:

Masanja Kadogosa, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) anasema Mkapa atakumbukwa kwa mengi ikiwa ni pamoja na kujenga taasisi nyingi kama Sumtra, TRA, Bima ya Afya na kadhalika.

“Hizi ni taasisi ambazo zimejenga misingi mingi ambayo sasa hivi inaisaidia nchi kukusanya matrilioni ya pesa,” anasema.

Anasema Mkapa ndiye pia alieanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ambao umekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii.

Kadogosa anawahimiza vijana kusoma kitabu cha mkapa. Wajifunze uadilifu na uzalendo na kusimamia mambo kwa ukamilifu.

ALIKUWA JABALI LA DIPLOMASIA:

Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima anasema: “Mkapa alikuwa jabali la diplomasia nchini. Aliifanya Tanzania ikang’ara kimatiafa. Alipoingia madarakani alisema uungwana ni kulipa madeni.

Alifanya hivyo hali iliyotujengea heshima kubwa” anasema.

Gwajima anashauri vijana nchini kujifunza diplomasia ya uchumi na hususani wanaotaka uongozi wa nchi.

CCM TUNA HAZINA YAKE KUBWA:

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally, anasema: “Tusome kitabu chake, hasa sura za kwanza tano. Ni maelezo yanayoweza kusaidia sana katika kuwaandaa vijana,” anasema

Siku saba za maombolezo zilizowekwa ni muhimu sana na kwamba baada ya siku hizo saba Watanzania ni muhimu kuendelea kunzi mitazamo yake na kuifanyia kazi. 

“CCM Tulimhitaji sana wakati huu tunapoingia kwenye uchaguzi mkuu lakini ndio mipango ya Mungu. Hata hivyo, tunayo hazina yake nyingi,” anasema.

TUMEPOTEZA MTU MUHIMU:

Mussa Azzan Zungu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) anasema Tanzania imepoteza mtu muhimu aliyesimamia demokrasia na uchumi.

“Sisi sote tumuige Mkapa kama mfano wa majabali ya demokrasia duniani,” anasema.

AMEIPA NCHI HESHIMA KIMATAIFA:

Balozi Idd Seif, Makamu huyo wa pili wa Rais Zanzibar anasema kwamba Mkapa ametufundisha mengi na kutuachia kama hazina.

“Ametufundisha mengi hata mimi ninandelea kujifunza kwake licha ya kuondoka duniani. Alifanya kazi nyingi za diplomasia ikiwemo kutatua migogoro kwa niaba ya nchi yetu, na hivyo ameipatia nchi yetu heshima kubwa,” anasema.

Balozi Iddi pia anahimiza Watanzania kusoma kitabu chake kwani ameeleza mengi aliyofanya na makosa aliyopitia. “Ninaomba vijana wasome kitabu chake. Wote wanaoingia katika diplomasia na uongozi wajifunze kupitia kitabu chake kwani ni mwalimu mzuri wa viongiozi,” anasema

AMETUACHIA KITABU:

Palamagamba Kabudi, Waziri hyo wa Mambo ya Nje anasema: “Nilimfahamu Mkapa nikiwa kijana mdogo, wakati huo nikiwa mwandishi wa habari wa gazeti la Uhuru na yeye akiwa Mhariri Mtendaji wa gazeti la Daily News.

“Nimejifunza kwake matumizi ya lugha na usahihi. Nilijifunza pia kwake kufanya utafiti kabla ya kuandika na hata kusema.

“Mkapa alikua mzalendo na ndio maana Mwalimu alimwamini sana. Alikuwa mchapa kazi, alikuwa amwaminifu na mwadilifu sana kwa nchi yake.

Alitumikikia taifa hili kwa nguvu zake zote. Bahati nzuri ametuachia kitabu chake ambacho pia anaeleza kuhusu Tanzania anayotamani iwe kama utasoma katika sura za mwisho mwisho za kitabu.

MENGI ALIYAANZISHA:

Japhet Hasunga, Waziri wa Kilimo anasema msingi wa nchi yetu kuwa na uchumi wa kati tunaojivunia sasa ulijengwa na Mkapa.

“Alipoingia madarakani matumizi ya serikali hayakuwa mazuri sana hivyo alianza kwa kubana matumizi ili kuhakikisha matumizi yanaelekezwa kwenye sekta ya uzalishaji. “Kimsingi mambo mengi ambayo serikali ya awamu ya tano inafanya sasa yalianzishwa na yeye Mkapa.

ALIKUWA MLEZI WETU:

Paul Makonda, Mkuu wa zamani wa mkoa wa Dar es Salaam anasema Mkapa alikuwa mlezi wa watu wengi.

“Vijana wengi wamefika nyumbani kwake na alikuwa tayari kuwasaidia. Mwaka 2012 wakati natafuta umakamu mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM, nilifika nyumbani kwake.

Nikamweleza ndoto niliokuwa nayo na yeye akanipa ushauri. Alinipokea wakati nikiwa sijulikani na mtu yeyote.

“Aliingia mfukoni mwake na kunipa pesa iliyoanzaisha mchakato wangu wa kisiasa na aliendelea kunipa msaada na ushauri,” anasema Makonda.

OKTOBA 28, 2020 Tanzania itafanya Uchaguzi Mkuu kuchagua rais, wabunge ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi