loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tumuage Mkapa tukienzi mazuri yake

KWA siku tatu kuanzia jana, Watanzania na watu wengine kwa ujumla wanapata wasaa wa kumuaga Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa aliyefariki dunia Alhamisi usiku jijini Dar es Salaam.

Mwili wa Rais mstaafu Mkapa umewekwa kwenye Uwanja wa Uhuru ambako jana baada ya misa maalumu, wananchi walianza kutoa heshima zao za mwisho kwa Rais huyo aliyeiongoza Tanzania kwa miaka 10 kuanzia Novemba 23, 1995 hadi Desemba 21, 2005.

Ni Rais ambaye amefanya mengi makubwa kwa nchi yetu tangu alipoanza kazi za utumishi wa umma hadi kuwa Rais na hata baada ya kustaafu, amekuwa nguzo muhimu kwa nchi na nje ya mipaka ya Tanzania.

Wakati tukiendelea kuwahimiza Watanzania hasa wale walioko mkoani Dar es Salaam na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kumuaga shujaa huyu wa Tanzania, hatuna budi kusisitiza mambo kadhaa ambayo Rais mstaafu Mkapa aliyatilia mkazo wakati wa uhai wake.

Rais mstaafu Mkapa alisisitiza sana suala la kufanya kazi na kujituma pamoja na kujali nidhamu, mambo ambayo yalijidhihirisha wazi wakati wa utawala wake, kwa kuifanya nchi ipige hatua kubwa za kimaendeleo kwa sababu alisimamia kazi, uwajibikaji, nidhamu na zaidi uthubutu kwa kila jambo chini ya falsafa ya Uwazi na Ukweli.

Suala la rushwa pia lilikuwa moja ya ajenda zake kuu na ndio maana chini ya uongozi wake ikaanzishwa Taasisi ya Kuzuia Rushwa (PCB) na ambayo baadaye ikajulikana kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kama njia mojawapo ya kukabiliana na suala hilo ovu katika jamii.

Hakuishia hapo Rais mstaafu Mkapa, pia alifanya kazi kubwa ya kuwaunganisha Watanzania na watu wa nje ya mipaka kwa kujenga uhusiano mzuri na majirani pamoja na mataifa mengine, kiasi cha kushuhudia Tanzania ikiwa na marafiki wengi wanaokuja kututembelea na kutusaidia kwa hali na mali.

Mambo haya pamoja na mengine mengi aliyoyafanya katika uhai wake, ni muhimu Watanzania wakayaenzi na kuyadumisha katika njia ya kumuenzi kiongozi huyo aliyetumia muda wake mwingi wa maisha kuwatumikia wananchi wenzake wa Taifa hili akitanguliza mbele uzalendo na utaifa kwa nchi yake.

Rais mstaafu amekamilisha yale aliyoyamudu kuyafanya kwa uhai wake aliojaliwa na Mwenyezi Mungu hapa duniani, lakini kwa sisi tuliobaki, ni jukumu letu kuhakikisha Tanzania inaendelea kupiga hatua kubwa za kimaendeleo kwa kuunga mkono yale yote aliyoyaanzisha na kuyafanya akiwa hai.

KUMEKUWAPO na habari za kufurahisha kuhusu mashirika zaidi ya ndege ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi