Naamka asubuhi, sioni kilongalonga,
Napapasa kitandani, hamadi hiki hapa,
Nini kimetokea, naanza kuhabarika,
Lo! Mkapa si mwenzetu, tutaonana baadaye
Habari yanishtusha, Mkapa katangulia,
Natetema kwa Mshtuko, siamini nionacho,
Uhakika napata, Mkuu wa nchi katangaza,
Lo! Mkapa si mwenzetu, tutaonana baadaye
Ukweli na uwazi, hilo alilikazia,
Kuficha mambo mwiko, hilo alisitizia,
Watesi walipoibuka, msimamo aliushikilia,
Lo! Mkapa si mwenzetu, tutaonana baadaye
Mkapa umeondoka, taarifa hukutoa,
Heshima uliyoacha, watumishi watakuenzi,
Uliingia Ikulu, watumishi wakaheshika,
Lo! Mkapa si mwenzetu, tutaonana baadaye
Sekta ya elimu, taswira yako ilidhihirika,
Wengi walirudi darasani, umri haukuwa kigezo,
Hukutaka waende peku, TASAF ukawanzishia,
Lo! Mkapa si mwenzetu, tutaonana baadaye
Walafi uliwakuta, sahani wamejijazia,
Mioyoni walijinenea, mali ya umma haiumi,
Mashirika uliyanyoosha, sahani ukazitupa,
Lo! Mkapa si mwenzetu, tutaonana baadaye
Uchumi ni alama, abadani haifutiki,
Ulishusha mfumuko, dijiti moja tulifika,
Ulikunjua makucha, walafi walipoibuka,
Lo! Mkapa si mwenzetu, tutaonana baadaye
Nyayo zako duniani, kwetu ramani ya kivita,
Lazima tukuenzi, kupambana na umasikini,
Kutetea wanaosawijika, kazi pekee iliyobaki,
Lo! Mkapa si mwenzetu, tutaonana baadaye
Michezoni si kapa, uwanja ulitujengea,
Vijana hawatakuona, jina lako watalitaja,
Wakipitia kumbukumbu, twasira wataiona,
Lo! Mkapa si mwenzetu, tutaonana baadaye
Siendi mbali tena, Mkapa huishi kusimulika,
Kimya hakisaidii, mahasidi wakatamalaki,
Katuandalie kiamba, njiani twakufuata,
Lo! Mkapa si mwenzetu, tutaonana baadaye
Aliyeandika ni Sauli Giliard, Mkazi wa Mivunoni, Dar es Salaam.