loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Uchambuzi wa Kitabu cha Mkapa My Life, My Purpose

MTOTO Benjamin William Mkapa alifundishwa kupika chakula na mama mzazi Stephania akiwa mdogo. Alipokwenda shule hapo kijijini Lupaso, Ndanda na hatimaye St Francis Pugu na kisha Makerere, alifundishwa kupika, kufinyanga, kubuni na kuchambua mawazo na kuyaweka sawa kama msomi mbunifu na mwandishi.

Kitabu hiki ni zao la mpishi wa mawazo mahiri aliyebobea. Ni kitabu cha kurasa 319, katika sura 16. Kuna utangulizi ulioandikwa na Mheshimiwa Joaquim Chissano, Rais mstaafu wa Msumbiji, pia kuna picha nyingi nzuri, na viambatanisho viwili.  Mchapaji Mkuki na Nyota wamefanya kazi nzuri sana, sikubaini kosa hata moja.

Wasilisho hili linamega simulizi hii katika sehemu kuu tatu. Kwanza, tunapewa vionjo vitamu tukielezwa kuzaliwa kwake, kukua na kwenda shule. Hii ilikuwa matayarisho ya kufikia nia au azma yake ya maisha. Kisha tunaletewa mlo wenyewe (main course) uliosheheni kumbukumbu na ngano za huyo kijana sasa mtu mzima akiwa kazini, mpaka akaukwaa urais wa Tanzania. Mwisho tunaelezwa kwa ufupi maisha yake baada ya kumaliza ngwe yake ya miaka kumi ya urais.

 

KUZALIWA, MALEZI NA ELIMU

 

Baba yake mzazi Mheshimiwa Mzee William Matwani alikuwa mpishi msaidizi huko Mission Ndanda. Wamisionari wakambatiza, wakamfundisha kusoma, kuandika na kuhesabu, na kumfanya Katekista. Alipelekwa Lupaso, ambapo alieneza dini na kufundisha Bush school ya Wamisionari.

Alimwoa Bibi Stephania Nambanga ambaye hakujua kusoma wala kuandika. Walijaliwa watoto wanne; Benjamin akiwa wa mwisho. Kama ilivyo kwa kabila la Makua, Benjamin alipewa jina la ujombani, Mkapa. Mama hakuwa na muda wa kujifunza kusoma na kuandika kwani yeye ndiye alikuwa msingi wa familia, akihakikisha analima, kulisha familia, na kuwalea watoto.  Alikuwa mkali lakini msikivu na mpenda haki. Wazazi hawa ndio vinara wa sehemu hii ya kwanza ya simulizi hii. Waliishi pamoja kwa uadilifu na heshima kubwa, na mapenzi ya pamoja kwa watoto wao.

Ingawa wazazi hawakwenda shule, walipenda sana watoto wao wote waende shule. Hii pamoja na kwamba Mzee Matwani alikuwa na kipato kidogo lakini cha uhakika kila mwezi, kiliifanya familia ionekane iko tofauti. Hii ilisababisha wivu na hatimaye chuki kutoka kwa jamii. Wivu huu na chuki ulisababisha tukio moja baya sana ambalo Mkapa analikumbuka kwa uchungu.

Mwaka 1947, kulitokea ukame mkali, basi watu wakamleta mganga wa kienyeji akaamua kuwa mama mzazi, mama yake na bibi yake ndio walikuwa wameloga na kuzuia mvua. Walipigwa na kuteswa sana hadi Padri Mzungu alipofanikiwa kuwanasua. Bibi wa mama aliaga dunia muda mfupi baada ya tukio hilo.

Kijana Benjamini na mwenzie mmoja ndiyo waliopata bahati ya kuendelea na masomo ya sekondari, kutoka darasa la watoto 25 hadi 30.   Kuchaguliwa ilikuwa bahati nasibu.

Shule ya sekondari ya Ndanda ilikuwa kilometa 60 kutoka Lupaso. Yeye na wenzie walitembea kwa miguu, bila viatu, kwa siku mbili, wakiwa wamebeba kichwani vitu vyao ambavyo vilikuwa vimefungwa katika mkeka. Baadae alipata sanduku la chuma.

Walimu wa Ndanda walikuwa wamisionari na walikazia sana sala na kazi Ora et labora’’.  Wanafunzi walipika chakula chao wenyewe. Kwa kuwa kijana Benjamini alikuwa mdogo sana alipewa kazi ya kuosha vyombo. Kawaida alivibeba vyombo kichwani mpaka mahali pa kuvioshea, na kuvirudisha. Anasema pengine kubeba vyombo hivyo ndiyo sababu ana upara hadi leo!

Mwaka 1952, akiwa na umri wa miaka 15, aliamua kwenda Seminari darasa la nane. Baada ya muda mfupi aliamua kuwa upadre haukuwa wito wake, akarudi Ndanda kuendelea na shule. Mwaka 1957, alichaguliwa kwenda St. Francis College Pugu ikiwa ni shule kuu ya Wakatoliki Tanganyika.

Akiwa Pugu, kijana Benjamin alianza kupata mwamko wa kisiasa. Aliunga mkono harakati za kupata uhuru kwa kuandika barua kwa Mhariri wa Gazeti la Tanganyika Standard ambalo sasa ni Daily News akiunga mkono hoja ya Uhuru. Barua ilichapishwa. Ila kijana Benjamin alitumia jina bandia!

 

Mkapa alishinda mitihani yake ya kujiunga Chuo Kikuu Makerere, kwa kupata daraja la kwanza, akiwa kati ya wanafunzi watatu bora katika darasa la wanafunzi 51.

Makerere alikumbana na mambo mengi mapya: Alikuwa darasani na wanafunzi wa rangi tofauti, kwa mara ya kwanza alikwenda kucheza dansi ya kisasa, alipangiwa chumba cha kulala.

Mwamko wake wa kisiasa uliendelea.  Alijiunga na Bodi ya Wahariri ya gazeti la Transition; alikuwa mwanachama hai wa kikundi cha wanafunzi cha TANU, akiwa katibu na hatimaye mwenyekiti wake. Alishiriki kwenye siasa za wanafunzi hapo chuoni. Aligombea urais na ingawa hakushinda, wanafunzi wa kike walimpigia kura nyingi si kwa sababu alikuwa na rafiki wa kike, ila kwa jinsi alivyoweza kujieleza kuliko mpinzani wake.

Alikuwa more articulate! Aliteuliwa Makamu wa Rais wa Serikali ya wanafunzi, na hatimaye alikuwa mwenyekiti wa Baraza la wawakilishi la wanafunzi hapo Makerere. Alihitimu masomo yake Aprili 1962, miezi minne baada ya Tanganyika kupata Uhuru. Alipata shahada ya lugha na fasihi ya kiingereza na fonetiki.  Alikuwa tayari kuifukuzia nia na ndoto yake.

MAISHA NA KAZI

Simulizi ya maisha ya utu uzima iko katika sehemu mbili.  Kwanza ni alipoanza kazi mpaka alipogombea urais.  Pili ni maisha ya urais.  Sehemu hii ya simulizi imejaa sifa heshima na upendo mwingi kwa Mwalimu. Anastaajabu kwa jinsi Mwalimu alivyoiunganisha nchi katika kupigania vita vya ukombozi wa bara la Afrika.

Kama wazazi wake mzee Matwani na Bibi Nambanga walikuwa mashujaa wa sehemu ya kwanza ya maisha yake, hakika Mwalimu ndiye shujaa katika sehemu hii ya pili.  Anamueleza Mwalimu kama labda alitumwa na Mungu kwa makusudi (almost divine intervention).

Akiwa mtu mzima na mhitimu wa Chuo Kikuu Makerere, Mkapa alipenda kuajiriwa kwenye Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje: Kwanza ilishindikana lakini, baadae akaambiwa, itawezekana kama ataajiriwa kwanza kama bwana shauri mkufunzi wa wilaya, wakati akisubiri. Kwa hiyo aliajiriwa hivyo huko Dodoma Aprili 1962.

 

Baada ya miezi minne, Agosti 1962 aliitwa Dar es Salaam aende kujifunza masuala ya Diplomasia Columbia, Marekani.

Baada ya mwaka mmoja alirudi nchini akaajiriwa wizarani. Kazi yake kubwa ilikuwa kuchukua muhtasari wa mazungumzo ya Waziri wake au Rais, Mwalimu Nyerere alipopata wageni. Anamsifia kwa ujasiri pale alipovunja uhusiano na Uingereza. Wakati huu Mkapa alitumia muda wake binafsi ama kusoma habari Radio Tanzania Dar es Salam, ama kumchumbia Bi Anna.

Siku moja aliambiwa anaitwa Msasani kwa Mwalimu. Walipaita Msasani nyumbani kwa Mwalimu The Clinic.  Mwalimu akamwambia anamteua kuwa Mhariri Mtendaji wa gazeti la The Nationalist. Ilibidi aende Uingereza kujifunza mambo ya magazeti kwenye magazeti ya The Mirror.

Alirudi na kuanza kazi chini ya Mwalimu kama Mhariri Mkuu. Mkapa alikuwepo Arusha wakati wa Azimio na mwenzie Nsa Kaisi ndiye aliyebuni neno la Arusha Declaration, walilitumia kwenye The Nationalist, Mwalimu akalipenda, basi hayo maamuzi yakaitwa hivyo.

Mkapa aliruhusiwa kuhudhuria mikutano ya kamati kuu ya TANU, ambayo wakati ule ilitawaliwa na malumbano ya hoja na uchambuzi yakinifu ambao umepotea. Alihusika katika kutayarisha sera mbalimbali za chama kutokana na umahiri wake wa kumudu lugha.

Mwalimu na msaidizi wake, Joan Wicken ndio waliomfundisha ujamaa na alivutiwa na msimamo wa usawa na umuhimu wa kujitegemea. Aliunga mkono wazo la Jeshi la Kujenga Taifa na akamwomba Mwalimu akamkubalia ajiunge kwa hiari. 

Alijiunga na kuhitimu.  Siku ya kuhitimu Mwalimu alikuwa ndie mgeni rasmi.  Mheshimiwa Mkapa alichaguliwa na wenzie kusoma risala na Mwalimu alicheka sana alivyomtambua kuwa ni yeye kwani alikuwa amepoteza ratili nyingi za uzito.  Alikuwa slim fit.  Mheshimiwa Mkapa aliitwa huko The Clinic Msasani mara kadhaa.

April 1972 Mwalimu alimteua kuwa Mhariri Mtendaji wa Daily News, muda mfupi baadaye Mwalimu alimteua kuwa mwandishi wa Rais. Anasema huu ndio ulikuwa mwanzo wa maisha yake kama mwanasiasa. Mwaka huohuo, Mwalimu alimuagiza aanzishe Shirika la Habari Tanzania SHIHATA na kuwa Mtendaji Mkuu wake.

Itaendelea kesho

 

MAOFISA Waandamizi wa Sekta ya Sheria wa Jumuiya ya Maendeleo ...

foto
Mwandishi: Profesa Rwekaza Mukandala

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi