loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Zijue sifa, masharti ya kuteuliwa kugombea uongozi

ULE mwaka uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu na wapenda demokrasia wa kupata viongozi wengine wa nchi yetu kwa miaka mitano ijayo umefi ka na tayari tarehe za tukio zimeshatangazwa rasmi.

Ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu, ambao kwa mara nyingine unawapa fursa watanzania wenye sifa kuwachagua viongozi wao. Ni muhimu ikakumbukwa kwamba jukumu hili la kusimamia, kuratibu na kuendesha uchaguzi wa rais, wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na madiwani wa Tanzania Bara limekabidhiwa kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) chini ya Ibara ya 74 (6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tayari Tume kupitia Mwenyekiti wake, Jaji Semistocles Kaijage imetangaza ratiba ya uchaguzi mkuu ikiwa ni pamoja na tarehe ya uchaguzi huo.

Jaji Kaijage anasema fomu za uteuzi kwa ajili ya wagombea wa kiti cha urais zitaanza kutolewa na Tume kuanzia tarehe 5 hadi 25 Agosti, 2020 katika ofisi za Tume zilizopo eneo la Njedengwa, Jijini Dodoma. Kwa upande wa wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani, Jaji Kaijage anasema fomu zitaanza kutolewa kuanzia tarehe 12 hadi 25 Agosti, 2020 katika ofisi za Wasimamizi wa Uchaguzi kwenye makao makuu ya halmashauri na kata husika.

Alitangaza tarehe ya uchaguzi mkuu kuwa ni 28 Oktoba, 2020 na kwamba Tume itafanya uteuzi wake wa wagombea tarehe 25 Agosti, 2020. Kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 37 (1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, fomu hizo sharti ziwasilishwe si zaidi ya saa 10:00 jioni siku ya uteuzi.

Msimamizi wa Uchaguzi anatakiwa awepo ofisini kuanzia saa 1:30 asubuhi hadi saa 10:00 jioni siku ya uteuzi ili kukamilisha zoezi hilo.

Ratiba ya Uchaguzi Mkuu inaonesha kwamba kampeni za uchaguzi katika nafasi zote zitaanza tarehe 26 Agosti, 2020 hadi 27 Oktoba, 2020 na Uchaguzi Mkuu utafanyika siku ya Jumatano, tarehe 28 Oktoba, 2020.

IDADI YA MAJIMBO:

Tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, ni vyema tukajikumbusha kwamba Tume pia kwenye Ibara ya 74 (6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepewa jukumu la kuchunguza mipaka na kuigawa Jamhuri ya Muungano katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya uchaguzi wa wabunge, kutokana na jukumu hili la Tume, watanzania walikuwa na shauku kubwa ya kutaka kujua endapo Tume imeongeza au imepunguza majimbo ya Uchaguzi.

Akifafanua jambo hilo Jijini Dodoma hivi karibuni, Jaji Kaijage alisema kwamba Tume haijafanya mapitio wala haijaongeza au kupunguza majimbo ya uchaguzi na kwamba majimbo yanabakia kuwa yaleyale ya mwaka 2015 ambayo ni 264.

“Kwa kuwa Tume haijagawa majimbo, jumla ya idadi ya majimbo ya uchaguzi yanabaki kuwa 264 kama ilivyokuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ambapo Tanzania Bara ina idadi ya majimbo 214 na Tanzania Zanzibar ina idadi ya majimbo 50. Hali kadhalika, jumla ya kata 3,956 za Tanzania Bara zitafanya uchaguzi wa madiwani wa mwaka 2020,” anasema Jaji Kaijage.

TARATIBU ZA UTEUZI WA RAIS:

Kutokana na Tume kupuliza kipenga, ni vyema sasa tukajikumbusha mambo mbalimbali yanayohusiana na taratibu za uteuzi wa wagombea kwa nafasi ya kiti cha rais, makamu wa rais, wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na madiwani wa Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa Kanuni ya 37 (1) na (2) ya kanuni za uchaguzi wa rais na wabunge za mwaka 2020, wagombea wa nafasi ya kiti cha rais na makamu wa rais watatakiwa kujaza Fomu Na 8A na Fomu Na. 10 za maadili ya uchaguzi ili kutimiza masharti ya kuteuliwa.

Kifungu cha 30 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, kimeweka utaratibu unaopaswa kufuatwa ili mtu aweze kuteuliwa kuwa mgombea wa kiti cha rais na makamu wa rais.

Kwa mujibu wa kifungu hicho, sifa za mgombea wa kiti cha rais au makamu wa rais ni pamoja na kuwa raia wa kuzaliwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, awe ametimiza umri wa miaka arobaini (40), awe mwanachama na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa, awe anazo sifa za kumwezesha kuwa mbunge au mjumbe wa baraza la wawakilishi na asiwe ametiwa hatiani na mahakama yoyote kwa kosa la kukwepa kulipa kodi yoyote ya serikali katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya uchaguzi.

Pamoja na sifa hizo, mgombea wa kiti cha rais au makamu wa rais ni lazima awe amedhaminiwa na watu wasiopungua 200 waliojiandikisha kupiga kura katika kila mkoa kwa mikoa 10 na kati ya hiyo angalau mikoa miwili iwe ya Tanzania Zanzibar.

Awe ameweka dhamana ya shilingi milioni moja 1,000,000 Tume ya Taifa ya Uchaguzi, dhamana hiyo itarejeshwa kwa mgombea baada ya Uchaguzi endapo atakuwa amepata sehemu moja ya kumi (1/10) au zaidi ya kura zote halali zilizopigwa na awe amekula kiapo mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufaa kwamba anazo sifa zinazotakiwa, hajapoteza sifa hizo na kwamba anakubali kuwa mgombea.

Aidha wagombea kwa nafasi hizo wanatakiwa kuwa na wadhamini ambao wamejiandikisha kuwa wapiga kura kwenye mikoa wanayoishi, hawajamdhamini mgombea mwingine yeyote wa kiti cha urais au umakamu wa rais.

Si lazima wawe wanachama wa chama kilichompendekeza; wala si lazima wawe wanachama wa chama chochote cha siasa na wawe wamewadhamini wagombea kwa kutumia fomu ya uteuzi.

KUTEULIWA UBUNGE:

Kwa mujibu wa Ibara ya 67 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mtu yeyote atakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa mbunge endapo ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ametimiza umri wa miaka 21.

Sifa nyingine ni kujua kusoma na kuandika kwa Kiswahili au Kiingereza, ni mwanachama na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa na hajawahi kutiwa hatiani na mahakama yoyote kwa kosa lolote la kukwepa kulipa kodi yoyote ya serikali katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya uchaguzi.

Sharti lingine ni awe amedhaminiwa na wapiga kura wasiopungua 25 walioandikishwa kuwa wapiga kura katika jimbo husika.

Ni muhimu ikumbukwe kwamba mgombea haruhusiwi kujidhamini yeye mwenyewe na mpiga kura anatakiwa kudhamini mgombea ubunge mmoja tu. Mgombea kwa nafasi hiyo pia anatakiwa awe ametoa tamko mbele ya hakimu kuthibitisha kwamba anazo sifa zinazotakiwa kugombea ubunge na hajapoteza sifa hizo.

Pia anatakiwa aweke dhamana ya shilingi 50,000 kwa msimamizi wa uchaguzi kupitia akaunti ya amana ya halmashauri atakayopatiwa siku atakayochukua fomu za uteuzi. Taratibu za uteuzi zinamtaka mgombea wa ubunge kujaza fomu namba 8B inayohusu taarifa zake binafsi, na zithibitishwe na chama kilichomteua ngazi ya mkoa, wilaya au jimbo kwamba ni za kweli.

Pia anaatakiwa kujaza fomu namba 10 ya tamko la kuheshimu na kutekeleza maadili ya uchaguzi.

Aidha mgombea anatakiwa awasilishe nakala nne za fomu ya uteuzi kwa msimamizi wa uchaguzi si zaidi ya saa 10:00 jioni siku ya uteuzi.

MGOMBEA UDIWANI:

Kwa upande wa wagombea wa udiwani, kifungu cha 39 (2) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, kinaainisha sifa za mgombea udiwani kuwa ni pamoja na kuwa raia wa Tanzania, awe ametimiza umri wa miaka 21, awe anajua kusoma na kuandika kwa Kiswahili au Kiingereza, awe mkazi wa kawaida wa halmashauri anayogombea, awe mwanachama na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa chenye usajili wa kudumu.

Mgombea huyo pia awe na kipato halali kinachomwezesha kuishi na awe hajatiwa hatiani na mahakama yoyote kwa kosa lolote la kukwepa kulipa kodi yoyote ya serikali katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya uchaguzi.

Mgombea udiwani anapaswa atimize masharti kadhaa ikiwa ni pamoja na kudhaminiwa na wapiga kura wasiopungua 10 walioandikishwa katika kata anayogombea, awe ametoa tamko mbele ya hakimu kuthibitisha kwamba anazo sifa za kugombea udiwani na hajapoteza sifa hizo.

Pia mgombea udiwani anatakiwa awe ameweka dhamana ya shilingi 5,000 kwa msimamizi wa uchaguzi kupitia akaunti ya amana ya halmashauri atakayopatiwa siku ya kuchukua fomu za uteuzi.

 

Mwanaidi Bilali, mkazi wa kijiji cha Matandu, wilayani ...

foto
Mwandishi: Abdulwakil Saiboko

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi