loader
Dstv Habarileo  Mobile
JPM, JK, Mwinyi wataka kifo cha Mzee Mkapa kuimarisha umoja wa kitaifa

JPM, JK, Mwinyi wataka kifo cha Mzee Mkapa kuimarisha umoja wa kitaifa

RAIS John Magufuli na marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi na Jakaya Kikwete, wametaka kifo cha Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, kitumike kuimarisha umoja wa kitaifa.

Wamesema Mkapa alitumia hekima na busara kujenga umoja wa kitaifa na pia alikuwa kiongozi wa mfano kwa kuwapenda watu wa nyumbani kwake.

Akitoa salamu za rambirambi kwa waombolezaji kijijini hapo jana, Rais Magufuli alisema Mkapa alipenda watu wa nyumbani kwake na alipenda kwao.

Alisema kuwa Mzee Mkapa alipoulizwa azikwe wapi, alikataa kuzikwa makaburi ya viongozi mjini Dodoma, badala yake alichagua kijijini kwake, jambo alilosema linapaswa kuigwa na Watanzania wote hasa viongozi waliopewa dhamana ya kuhudumia watu.

"Kwenye hili Watanzania tujifunze maana angeweza kusema azikwe Dar es Salaam au azikwe Lushoto au popote pale, lakini alichagua hapa, ndani ya dhamira yake alitaka azikwe kijijini alipozaliwa. Mzee Mkapa alipenda kwao, tujifunze upendo mkubwa aliouonesha,"alisema Magufuli.

Akifafanua kuhusu hilo la kuzikwa kijjijini, alisema miaka miwili au mitatu iliyopita Mkapa alimuuliza serikali imepanga kumzika wapi atakapokufa, akamuuliza yeye anataka azikwe wapi, akasema asizikwe Dodoma kwenye makaburi ya viongozi, bali azikwe Lupaso.

Magufuli alisema hilo alilianzisha Mkapa, ambapo Kikwete ametaka azikwe kwao Msoga na hata yeye atakapofariki dunia atapenda azikwe Chato. Alitoa utani kwamba maeneo ya kuzika viongozi ya Dodoma amemuachia Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela kwa kuwa kwao ni huko huko Dodoma.

Rais Magufuli alisema baada ya kila kiongozi kutaka azikwe kijijini kwake, eneo la makaburi lililotengwa na serikali mjini Dodoma alilirejesha kwa wananchi.

"Niliogopa wakati ule kumuuliza Mwinyi (Rais mstaafu) maana alikuwa na miaka zaidi ya tisini, nikaona isije kuwa uchuro," alisema Magufuli na kusababisha waombolezaji kucheka.

Magufuli katika hotuba hiyo aliwashukuru maaskofu, kamati ya maandalizi chini ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Watanzania wote kwa walivyoshiriki kikamilifu na kufanikisha maziko ya Mzee MkapaAwali akitoa salamu za pole, Rais mstaafu Kikwete alisema Mkapa aliitoa nchi kwenye hali mbaya ya kiuchumi na aliratibu upatikanaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, iliyoifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati.

Alisisitiza kuwa ana imani Rais Magufuli ataifikia ndoto ya Mkapa ya kufikia pato la kati la kila Mtanzania la Dola za Marekani 3,000 alilotamani lifikie kabla ya 2025.

"Rais Magufuli ametufikisha kwenye uchumi wa kati, hatua aliyoianza mwenyewe Mkapa, nami nikaendeleza na sasa Magufuli anaendelea vizuri sana, bado hatujafikia ndoto ya Mkapa ya pato la kati la Dola 3,000 kwa kila Mtanzania na Rais Magufuli naamini atatufikisha huko," alisema Kikwete.

Alitaja mambo aliyojifunza kwa Mkapa kuwa ni pamoja na namna alivyojali wananchi wake wakati akiwa Mbunge wa Nanyumbu na yeye akiwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Masasi.

Hivyo, alisema na yeye alipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje, kila alipopata nafasi alikwenda jimboni na kusikiliza kero za wananchi wake.

Kikwete alisema yeye alijaribu alipokuwa Mbunge wa Chalinze na Bagamoyo, lakini hana hakika kama alifanikiwa kama Mkapa.

Rais mstaafu Mwinyi alisema Mkapa alikuwa mtu mzuri, haneni sana lakini mwenye kufanya kazi sana kwa manufaa ya nchi. Alitaka watu wamuombee kwa Mungu kama alikuwa na dhambi, asemehewe na kupokelewa pema kwa kuwa naye alikuwa mwanadamu.

Mwinyi alimpa pole Rais Magufuli na kumuingiza rasmi katika cheo cha uzee na kumuita "Mzee Magufuli".

Pia Mwinyi alisema kuwa Rais Magufuli anafanya kazi nzuri, aliyoagizwa na Mungu kuitekeleza kuwaondolea watu umasikini, dhiki na mashaka.

Alisisitiza kuwa kazi hiyo ndio aliyotumwa kila kiongozi na Mkapa pia aliifanya. Aliwaasa vijana wanaokua na watakaokuja kuchukua uongozi kuwa amesikitishwa na namna watu wote walivyovaa viatu.

"Mimi nimezaliwa mwaka 1925, nimeona mengi, jambo dogo kwenu kwangu si dogo, limenisikitisha hapa wote mmevaa viatu.

Mimi mara ya kwanza kuvaa viatu ni jandoni na baadaye nikiwa na miaka 13 niliuza karafuu nikanunua viatu lakini nilivitundika bila kuvivaa ili visiishe, " alisema na kufanya umati kucheka.

Alisisitiza namna alivyotunza viatu vyake visiishe na kwamba kiongozi anatakiwa kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha hali ya wananchi wake inakuwa njema na hicho ndicho leo anachokifanya Rais Magufuli. Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein alisema Mkapa ni shujaa aliyelinda na kuhifadhi umoja wa kitaifa na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Salamu kutoka kwa Papa Francis zilizosomwa na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), zilimuelezea Mkapa kama kiongozi aliyejali watu wake na nchi yake na muumini mzuri wa Kanisa Katoliki.

foto
Mwandishi: Gloria Tesha, Masasi

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi