loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Uchambuzi wa Kitabu cha Mkapa My Life, My Purpose-3

LEO tunamaizia uchambuzi huu kuhusu kitabi cha Mpendwa wetu, Rais wa Awamu ya Tatu ya Jamahuri wa Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa ambaye alizikwa kijijini alikozaliwa, Lupaso, Masasi mkoani Mtwara jana.

Katika sehemu ya kwanza tuliangalia kuhusu kuzaliwa kwa Rais huyu mstaafu, maisha ya utotoni na kazi.

Jana tulianza kuangalia muhtasai wa maisha yake ya urais na tutaangalia muhtasari wa maisha yake baada ya urais kabla Mwenyezi Mungu hajamchukua. Kuhusu mahusiano ya ndani na nje, Mkapa anabaini katika kitabu chake kwamba uhusiano katika ya Bara na Zanzibar ulikuwa mgumu na tete lakini alifanikwa kutatua matatizo yaliyokuwepo.

Anasema alikuwa na wasiwasi pale Rais wa Zanzibar, Salmin Amour alipotaka kubadilisha sheria na kutawala kipindi cha tatu. Lakini baadae yeye na wafuasi wake wakaamua yaishe.

Zanzibar ilianza kupeperusha bendera yake. “Vifo vya watu 22 huko Pemba Januari 2001 vilinishtua na kumhuzunisha sana,” anasema katika kitabu chake na kuongeza: “Hili litaendelea kuwa doa katika Urais wangu ingawa sikuwepo lilipotokea.”

Anabaini kuwa wakati wa utawala wake, wanadiplomasia walionesha upendeleo kwa vyama vya upinzani na kukutana nao mara kwa mara, Pia wapo walioamini walistahili upendeleo kuliko wengine.

Kwa upande wa vyombo vya habari anasema ilibidi azoee kukosolewa, kwani waliamini alikuwa dikteta ingawa alikuwa anashikilia msimamo. Anabaini kuwa alihitaji kuuza sera zake, kwa hiyo akaanzisha utaratibu wa kulihutubia Taifa kila mwezi lakini mhimili mkuu wa kupokea na kutoa mawazo na habari ilikuwa Chama chake CCM na vikao vyake mbalimbali.

Mkapa anakiri kuwa, kabla hajawa Rais, hakujua kuwa kazi moja wapo ya rais ni kutoa pole.

Moja wapo ya mapungufu yangu ni kwamba si mwepesi wa kuonesha hisia zangu. Mrithi wangu Rais Kikwete ni mzuri sana katika hili,” anasema Mkapa. Mwaka 1996 Mkapa anasimulia mafuriko yalivyosababisha maafa makubwa katika nchi.

Kuzama kwa MV Bukoba kulistua na kuhuwisha sana majanga mengine mengi.

Anasema pia kwamba katika kipindi chake aliwahurumia wafungwa wote waliostahili kunyongwa mpaka kufa. Anasema ingawa hakatai kukosolewa kisiasa au kisera, kukosolewa binafsi kuliumiza sana.

Kwa mfano madai kwamba alimpendelea Baba mkwe wa mwanae katika kubinafsisha mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira yalimuumiza sana kwa sababu haikuwa kweli.

Pia madai kuwa aliwapendelea NET GROUP Solutions Ltd wakati wa kubinafisha TANESCO kwa sababu ya shemeji yake kulimuumiza sana pia. Jambo moja lilojitokeza baada ya kumaliza muda wake ni la External payment Arrears (EPA).

Mkapa anasema anaeleza kuwa, anavyoelewa urais wake haukuwa wa kwanza kuruhusu ununuzi wa madeni kama huo. Anasema kwanza alisita ila Gavana wa Benki Kuu, Daud Bilali alimwelewesha na akasema watakaonunua hayo madeni walikuwa tayari kuchangia mfuko wa kampeni za uchaguzi wa CCM.

Wahuni walitumia uaminifu wake kwa chama kumshawishi akubali. “Ninajisikia kuwa nilitumika na kusalitiwa. Na ukweli ni kwamba mimi binafsi sikufaidika na sikupata chochote,” anasema Mkapa.

Kuna kukosolewa kuhusu matumizi ya anwani ya Ikulu wakati mimi na mke wangu tulipochukua mkopo NBC kununua nyumba. Ukweli ni kwamba wakati ule tulikuwa tunaishi Ikulu, tulichukua mkopo kwa mashart ya kawaida ya biashara.

Kabla sijaondoka Ikulu, nilimaliza malipo ya mkopo huo na mshahara wangu wa mwisho na mafao yangu, tukapewa hati ya nyumba hiyo. Anasema Mkapa.

Kulikuwa pia na suala la radar ambayo ilkuwa lazima inunuliwe ili kuimarisha ulinzi lakini manunuzi yaligubikwa na udanganyifu na hatimaye hela zilizolipwa za ziada zilirudishwa kwa Serikali.

Anafikiri ni muhimu kutazama upya suala la umiliki wa uchumi ili watu wengi zaidi wahusike.

Kuendelea kushamiri kwa umiliki hasa wa viwanda na mashamba makubwa na makampuni ya Kiasia au Kihindi inaweza ikaleta wivu, na kuleta shida kubwa.

Mkapa anaeleza wasiwasi na siku za mbeleni kwani umaskini huenda bega kwa bega na uvunjifu wa amani. Anatoa ushauri kwa viongozi wa sasa na wajao kuonesha nia na bidii kwa majukumu wapewayo.

“Uwe tayari kuwashirikisha wengine katika mawazo, mafanikio, matatizo na upimaji utekelezaji, consult more. Usifanye kazi kwa kukurupuka na kutotabirika. Fuata na tii sheria na taratibu.

Uwe tayari kusikiliza. Mtafute mlezi (mentor) kama mimi nilivyokuwa na Mwalimu,” anasema.

Pia anabainisha umuhimu wa mke wake mama Anna Mkapa katika kumshauri. Mapema kabisa katika ukurasa wa 83, Mkapa anampa saluti mama Anna kwamba yeye ndiye gundi iliyoshikilia familia.

Anakiri kuwa yeye siyo mtu rahisi kuishi naye na anamshukuru kwa kuwa mtu wa subira na uwezo mkubwa. Amevumilia mengi wakati wa safari za mara kwa mara, kutokuwepo nyumbani mara nyingi na ndiye alibeba mzigo wa kuwalea watoto wao wawili.

KUSTAAFU:

Sehemu ya tatu na ya mwisho ya simulizi hii ni maisha ya Mkapa baada ya kustaafu urais. Anasema baada ya kustaafu ametumika sana kimataifa katika nyadhifa na taasisi mbalimbali ingawa hapendi kusafiri. Taasisi hizo ni pamoja na Club de Madrid, The African Wildlife Foundation, Investment Climate Facility for Africa, UN Initiative “Delivering as One”, UNCTAD Panel of Environment Persons.

UN Commission on the Legal Empowerment of the Poor, Mwenyekiti wa Seventh Centre tangu 2006, Trustee the Aghakhan University na The Mkapa Foundation.

Anasema kote huku amejichanganya na watu wenye akili nyingi na mitazamo mbaimbali.

Pili anasema amehusika sana katika upatanisho wa migogoro huko Sudan Kusini, Burundi, Congo Mashariki na Kenya. Mkapa, anamalizia simulizi hii kwa kugusia mambo kadhaa. Kwanza, anaona Rais mstaafu anathaminiwa zaidi uongozi na uwezo wake kimataifa zaidi kuliko nyumbani, jambo ambalo hata Mwalimu aliliona.

Mara nyingi huitwa kwenye hafla ambapo anakuwa kama ua au pambo ukutani, lakini natakiwa kwenye kazi muhimu na nyeti za kitaifa.

Pili, anaongelea umuhimu wa kuanzishwa kwa baraza dogo kama sehemu ya Bunge kupitia miswada iliyopitishwa na Bunge kabla ya utekelezaji.

Tatu, anazungumzia kukosekana kwa itikadi na fikra pevu za kina juu ya mustakabali wa Taifa letu.

Anabainishwa kuwa tunahitaji ukombozi wa pili, Kisiasa, Kiuchumi, Kiutamaduni. Tunahitaji kama Taifa, na mtu mmoja mmoja kuona aibu kuwa ombaomba. Tunahitaji kujitegemea na kuthamini uendelevu (sustainability) wa maendeleo.

Nne, anagusia mwendo goigoi katika kuimarisha Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC). “Sioni juhudi kubwa, naona siasa tu, watu wamepoteza picha kubwa (Big Picture) ya Jumuiya. Tano, anagusia uongozi. Anabainisha kuwa uongozi bora ni kipaji au karama na sayansi pia.

Unazaliwa na karama hizo lakini unajifunza pia. Nia na kujitoa yaani commitment ni muhimu. Kiongozi bora ni lazima awe mfano wa kuigwa katika utendaji kazi wake, uaminifu na uadilifu.

Anatilia mkazo suala la ongezeko la vijana na kwamba hakuna sera ya namna ya kushughulikia ongezeko kubwa la watu. Anagusia pia suala la siasa halaiki yaani Populism na athari zake.

Kuhusu siasa na demokrasia, anabainisha kuwa CCM bado kinajiona kama bado kipo kwenye siasa za chama kimoja, kunahitajika siasa zaidi za kushirikiana (more political interaction and engagement). Anaendelea kusema kwamba uwepo wa vyama vingi vya siasa unadhoofisha demokrasia.

Watu wanaingia katika siasa kusaka manufaa ya kiuchumi sio kwa nia tukufu ya kuwatumikia watu na taifa. Wafanyabiashara wanasaka na kulinda maslahi, wasomi hutafuta kusafiri na posho, wabunge wachache wanajali maslahi ya jimbo, wengi wanapenda safari za nje.

Hakuna interaction ya wabunge kuhusu sera na utekelezaji wake. Mkapa anajiuliza kama tutaweza kudumisha amani na umoja wetu kama Taifa. Anagusia kuibuka hapa na pale kwa viashiria vya ukabila, udini, na ukanda.

Mwisho kabisa Mkapa, anamalizia kitabu chake kwa kusema; Nitamwachia Mungu wangu na nyinyi kuamua ni tofauti gani nimeifanya humu duniani. Huu ni muhtasari tu wa kitabu chake na hivyo ni vyema kama unaweza kukipata kabisa kitabu chenyewe na pengine ni wakati sasa wa kitabu hicho kutafsiriwa kwa Kiswahili.

MAKALA Uchambuzi wa Kitabu cha Mkapa My Life, My Purpose-3

OKTOBA 28, 2020 Tanzania itafanya Uchaguzi Mkuu kuchagua rais, wabunge ...

foto
Mwandishi: Profesa Rwekaza Mukandala

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi